The chat will start when you send the first message.
1Hili ndilo neno lililomjia Yeremia likitoka kwake Bwana kwamba:
2Yasikieni maneno ya agano hili, myaambie watu wa Yuda nao wakaao Yerusalemu!
3Utawaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Ameapizwa kila asiyeyasikia maneno ya agano hili,[#5 Mose 27:26.]
4niliyowaagiza baba zenu siku ile, nilipowatoa katika nchi ya Misri katika tanuru ya kuyeyushia vyuma kwamba: Isikilizeni sauti yangu, myafanyize yote, nitakayowaagiza! Ndivyo, mtakavyokuwa ukoo wangu, nami nitakuwa Mungu wenu,
5kusudi nikitimilize kiapo, ambacho niliwaapia baba zenu cha kwamba: Nitawapa nchi ichuruzikayo maziwa na asali, kama ilivyo na siku hii ya leo. Ndipo, nilipojibu nikisema: Amin, Bwana.[#2 Mose 3:8.]
6Bwana akaniambia: Yatangaze maneno haya yote katika miji ya Yuda namo barabarani mwa Yerusalemu kwamba: Yasikilizeni maneno ya agano hili, myafanyize!
7Kwani nimeyashuhudia baba zenu siku ile, nilipowatoa katika nchi ya Misri, mpaka siku hii ya leo sikuchoka kuwashuhudia na kuwahimiza kwamba: Isikieni sauti yangu!
8Lakini hawakuisikia, wala hawakuyatega masikio yao, wakaendelea kila mmoja kwa ushupavu wa mioyo yao mibaya, kwa hiyo nikawatimizia maneno yote ya hilo agano, nililowaagiza, walifanye, lakini hawakulifanya.[#Yer. 7:24,26.]
9Bwana akaniambia: Yameonekana mapatano mabaya ya watu wa Yuda nao wakaao Yerusalemu:
10wameyarudia mabaya ya baba zao wa kale walikataa kuyasikiliza maneno yangu, wakafuata miungu mingine, waitumikie. Walio mlango wa Isiraeli nao walio mlango wa Yuda wamelivunja agano langu, nililolifanya na baba zao.
11Kwa hiyo Bwana anasema hivi: Kweli wataniona, nikiwaletea mabaya, wasiyoweza kuyatoka. Ndipo, watakaponililia, lakini sitawasikia.[#Fano. 1:28; Yes. 1:15.]
12Kisha miji ya Yuda nao wakaao Yerusalemu watakwenda kuililia miungu, waliyoivukizia, lakini haitawaokoa siku za kupatwa na mabaya.[#Yer. 2:28; 5 Mose 32:37-38.]
13Kwani kama miji yako ilivyo mingi, ndivyo, miungu yako, Yuda, ilivyo mingi nayo. Tena kama barabara za Yerusalemu zilivyo nyingi, ndivyo, palivyo pengi napo, mlipopatengeneza pa kuitambikia iliyo yenye soni, ndipo pa kumvukizia Baali.
14Wewe nawe usiwaombee wao wa ukoo huu! Wala usipaze sauti kunilalamikia kwa ajili yao! Kwani mimi sisikii, wanaponiita, kwa ajili ya ubaya wao.[#Yer. 7:16; 14:11.]
15Waliokuwa wapenzi wangu wanataka nini Nyumbani mwangu? Mkiyafanya mawazo yenu mabaya yaliyo mengi, nyama takatifu zitayaondoa, yawatoke ninyi? Nanyi mnapofanya mabaya, ndipo, mnapofurahi.
16Bwana alikuita jina lako mchekele wenye majani mengi wa kupendeza macho kwa kuzaa vizuri, lakini sasa wengi wanaupigia makelele makubwa, maana ameuwashia moto wa kuuchoma, nayo matawi yake yamevunjika.
17Kwani Bwana Mwenye vikosi aliyekupanda amesema mabaya yatakayokujia kwa ajili ya mabaya, wao wa mlango wa Isiraeli nao wa mlango wa Yuda waliyonifanyizia, wanikasirishe, wakimvukizia Baali.
18Bwana akanijulisha, ndipo, nilipojua, kisha akanionyesha matendo yao.
19Mimi nikawa kama mwana kondoo mwanana anayepelekwa kuchinjwa, sikujua, ya kama walikuwa wameniwazia mimi mawazo ya kwamba: Na tuuangamize mti na matunda yake! Na tuung'oe katika nchi yao walio hai, jina lake lisikumbukwe tena![#Yes. 53:7.]
20Lakini wewe Bwana Mwenye vikosi, unakata mashauri yaongokayo, unajaribu mafigo na mioyo; na nione, jinsi unavyowalipiza, kwani nimekusukumia wewe shauri langu.[#Sh. 7:10.]
21Kwa hiyo Bwana anasema hivyo kwa ajili ya watu wa Anatoti walioitafuta roho yako wakisema: Usitufumbulie kwa Jina la Bwana, usiuawe na mikono yetu![#Yer. 1:1.]
22Kwa hiyo Bwana Mwenye vikosi anasema hivi: Utaniona, nikiwapatiliza: vijana wao watakufa kwa panga, nao watoto wao wa kiume na wa kike watakufa kwa njaa.
23Lakini masao hayatakuwako, kwani watu wa Anatoti nitawaletea mabaya mwaka ule, watakapopatilizwa.