Yeremia 13

Yeremia 13

Mfano wa mshipi.

1Hivi ndivyo, Bwana alivyoniambia: Nenda kujinunulia mshipi wa amerekani, ujifunge viunoni! Lakini usiutie majini!

2Nikaununua mshipi, kama Bwana alivyoniagiza, nikajifunga viunoni.

3Neno la Bwana likanijia mara ya pili kwamba:

4Uchukue mshipi, ulioununua, ulio viunoni pako! Kisha inuka, uende kwenye Furati, uufiche kule katika ufa wa mwamba!

5Nikaenda, nikauficha kule Furati, kama Bwana alivyoniagiza.

6Ikawa, siku nyingi zilipopita, ndipo, Bwana aliponiambia: Inuka, uende Furati, uuchukue kule mshipi, niliokuagiza kuuficha huko.

7Nikaenda Furati, nikauchimbua, nikauchukua ule mshipi mahali hapo, nilipouficha; lakini nilipoutazama ule mshipi, ulikuwa umeharibika, haukufaa kitu cho chote.

8Ndipo, neno la Bwana liliponijia kwamba:

9Bwana anasema hivi: Hivi ndivyo, nitakavyoyaharibu majivuno ya Yuda nayo majivuno ya Yerusalemu yaliyo mengi.

10Watu wa ukoo huu mbaya wamekataa kuyasikia maneno yangu, wakajiendea kwa ushupavu wa mioyo yao, wakafuata miungu mingine wakiitambikia na kuiangukia; basi, watakuwa kama mshipi huu usiofaa kitu cho chote.[#Yer. 11:8.]

11Kwani kama mshipi unavyoambatana na viuno vya mtu, ndivyo, nilivyowaambatanisha na mimi wote walio wa mlango wa Isiraeli nao wote walio wa mlango wa Yuda, wawe ukoo wangu wa kulikuza Jina langu, wakilishangilia na kulitukuza, lakini hawakusikia; ndivyo, asemavyo Bwana.

12Basi, utawaambia neno hili: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Viriba vyote na vijazwe mvinyo! Wakikuuliza: Hatujui, ya kuwa viriba vyote hujazwa mvinyo?

13ndipo, utakapowaambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtaniona, nikiwajaza ulevi wote wakaao katika nchi hii, wafalme wanaokikalia kiti cha kifalme cha Dawidi na watambikaji na wafumbuaji nao wote wakaao Yerusalemu.[#Yer. 25:15-18; Yes. 51:17.]

14Kisha nitawaponda kila mtu kwa ndugu yake, hata wababa na wana pamoja, sitawaonea uchungu, wala sitawachagulia, wala sitawahurumia, nisiwaangamize; ndivyo, asemavyo Bwana.

Kutekwa kwa Wayuda.

15Sikieni na kusikiliza vema! Msijikweze! Kwani Bwana anasema:

16Mtukuzeni Bwana Mungu wenu, akingali hajaleta giza bado, mkingali hamjajikwaa miguu yenu milimani penye giza! Maana mtangoja, pawe mwanga, naye ataugeuza kuwa kivuli kiuacho akiufunikiza mawingu meusi.

17Lakini msiposikia, roho yangu itayalilia majivuno yenu mafichoni, nayo macho yangu yatachuruzika machozi pasipo kukoma, kwa kuwa kundi la Bwana limetekwa.[#Yer. 9:1.]

18Mwambie mfalme na mama yake: Jinyenyekezeni, mkae chini! Kwani vichwani penu vilemba vya urembo vimeanguka chini![#Omb. 5:16.]

19Miji ya upande wa kusini imefungwa, tena hakuna anayeifungua, Wayuda wote wametekwa, kweli wote pia wametekwa.

20Yainueni macho yenu, mwaone wanaokuja toka kaskazini! Kundi ulilopewa liko wapi, wale kondoo wako wenye utukufu?

21Utasemaje, akikuwekea wale kuwa wakuu wako, uliowazoeza kuwa rafiki zako wapendwa? Wao watakapokuwa wakuu, hautakushika uchungu kama wa mwanamke anayetaka kuzaa?

22Kama unauliza moyoni mwako: Mbona haya yamenitukia? ujue: Kwa mabaya yako mengi, uliyoyafanya, nguo zako zenye mapindo marefu zimefunuliwa, hata miguu yako ikatokezwa nje kwa kukorofishwa hivyo.[#Yes. 47:2-3; Ez. 16:37.]

23Je? Mtu mweusi anaweza kuigeuza ngozi yake? Au chui anaweza kuyaondoa madoadoa yake? Kama ndivyo, mngeweza kufanya mema nanyi mliofundishwa kufanya mabaya.[#Sh. 55:20.]

24Kwa hiyo nitawatawanya kama makapi yapeperushwayo na upepo wa nyikani.

25Haya ndiyo, uliyopatiwa na kura, ni fungu lako, ulilopimiwa na mimi, kwa kuwa umenisahau, ukaegemea mambo ya uwongo; ndivyo, asemavyo Bwana.

26Kwa hiyo mimi nami nitazipandisha nguo zako zenye mapindo marefu na kuziweka usoni pako, yako yenye soni yaoneke.[#Yer. 13:22.]

27Uzinzi wako na vilio vyako vya utongozi na uovu wako wa kuziwaza njia za ugoni za kwenda vilimani au mashambani, nimeyaona hayo matapisho yako. Yatakupata, wewe Yerusalemu, usieuliwe! Yatakuwa hivyo mpaka lini?

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania