The chat will start when you send the first message.
1Hili ndilo neno la Bwana lililomjia Yeremia kwa ajili ya kupotea kwa mvua:
2Yuda huomboleza, nao waliomo malangoni mwake wamefifia kwa kukaa mchangani na kuvaa nguo nyeusi, navyo vilio vya Yerusalemu hupanda juu.
3Wakuu wao huwatuma walio wadogo kwao kwenda majini; lakini wakifika visimani hawaoni maji, hurudi wenye mitungi mitupu, huona soni na masikitiko, hufunika vichwa vyao,
4kwani nchi imeatukaatuka; kwa kuwa haikuwako mvua katika nchi, wakulima huona soni, huvifunika vichwa vyao.[#Yoe. 1:11.]
5Kwani kulungu nao wakizaa porini huwaacha watoto, kwa kuwa hakuna majani.
6Navyo vihongwe husimama vilimani juu, hutwetea upepo kama mbwa wa mwitu, macho yao huzimia kwa kuwa hakuna majani.
7Kweli manza, tulizozikora, zimetusuta; lakini, Bwana, yafanye yalipasayo Jina lako! Kwani tumekuacha mara nyingi, tukarudi nyuma, tumekukosea kweli.[#Dan. 9:4-14.]
8Wewe ndiwe, Waisiraeli wamngojeaye, ndiwe mwokozi wao, siku zinapokuwa mbaya. Mbona unataka kuwa kama mgeni katika nchi hii au kama mpitaji apigaye kambi tu kulala usiku?
9Mbona unataka kuwa kama mtu aliyeshindwa au kama fundi wa vita asiyeweza kuokoa? Wewe, Bwana, uko kwetu katikati, nasi huitwa kwa Jina lako, usituache![#Yer. 15:16; Yes. 43:7.]
10Hivi ndivyo, Bwana anavyosema kwa ajili ya watu wa ukoo huu: Hupenda kwenda huko na huko, hawaizuii miguu yao; kwa hiyo Bwana hapendezwi nao, sasa anayakumbuka mabaya yao, waliyoyafanya, ayapatilize makosa yao.
11Naye Bwana akaniambia: Usiwaombee wao wa ukoo huu, niwafanyizie mema![#Yer. 7:16; 11:14.]
12Wakifunga mfungo, siwasikii malalamiko yao; hata wakitoa ng'ombe au vipaji vingine vya tambiko, sipendezwi nao. Kwani mimi nitawamaliza kwa panga na kwa njaa na kwa magonjwa mabaya.[#Yer. 6:20; Yes. 58:3.]
13Nikasema: E Bwana Mungu, tazama! Wako wafumbuaji wanaowaambia: Hamtaona upanga, wala njaa haitakuwa kwenu, kwani nitawapa kutengemana kweli mahali hapa!
14Bwana akanijibu: Ni uwongo tu, hao wafumbuaji wanaofumbua katika Jina langu sikuwatuma, wala sikuwaagiza neno, wala sikusema nao. Wanayoyafumbua ni ndoto za uwongo na maaguaji ya bure na madanganyifu ya mioyo yao.[#Yer. 23:21; 27:14-15; 29:8-9.]
15Kweli hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Wafumbuaji hao wanaofumbua katika Jina langu mimi sikuwatuma, wao wanaosema: Hakuna upanga wala njaa itakayokuwa katika nchi hii, basi, wafumbuaji hao watamalizwa kwa panga na kwa njaa![#5 Mose 18:20.]
16Hata watu waliofumbuliwa nao watakuwa wametupwa barabarani mwa Yerusalemu wakiuawa kwa njaa na kwa panga, hatakuwako atakayewazika wao na wake zao na wana wao wa kiume na wa kike; ndivyo, atakavyowamwagia mabaya yao.[#Yer. 8:2.]
17Nawe na uwaambie neno hili: Macho yangu yanachuruzika machozi usiku na mchana, hayakomi, kwani wanawali walio wazaliwa wa ukoo wangu wamevunjika mavunjiko makuu, ni pigo lisilopona kabisa.[#Yer. 9:1.]
18Nikitoka kwenda shambani ninaona waliouawa na panga; nikiingia mjini ninaona waliozimia kwa njaa. Kwani nao wafumbuaji pamoja na watambikaji wanahamia nchi, wasiyoijua.
19Umemtupa Yuda kabisa? Roho yako imetapishwa na Sioni? Mbona umetupiga? Lakini hakuna atakayetuponya. Tunangojea utengemano, lakini hakuna chema; tunangojea siku za kupona, lakini tunayoyaona ni mastuko.[#Yer. 8:15.]
20Tunajua, Bwana, ya kuwa hatukukucha, tukakora manza, baba zetu walizozikora; kweli tumekukosea wewe.[#Yer. 14:7.]
21Lakini kwa ajili ya Jina lako usitukatae na kututweza! Usiache, kiti cha utukufu wako kibezwe! Likumbuke Agano lako, ulilolifanya na sisi, usilivunje!
22Je? Katika miungu ya wamizimu isiyo kitu imo iwezayo kunyesha mvua? Au ni mbingu zitoazo zenyewe manyunyu tu? Si wewe, Bwana Mungu wetu? Kwa hiyo tunakungojea, kwani wewe ndiwe ayafanyaye haya yote.