Yeremia 15

Yeremia 15

Wayuda hawana budi kuangamia.

1Bwana akaniambia: Ijapo Mose na Samweli wanitokee, Roho yangu haitawaelekea wao wa ukoo huu. Waondoe usoni pangu, wajiendee![#Sh. 99:6; Ez. 14:14.]

2Kama wanakuuliza: Twende kwenda wapi? utawaambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kama ni kufa, nendeni kufa! Kama ni kuuawa na panga, nendeni kwenye panga! Kama ni kufa kwa njaa, nendeni kwenye njaa! Kama ni kutekwa, nendeni kutekwa![#Yer. 43:11; Zak. 11:9.]

3Nitawapatia namna nne za mapatilizo; ndivyo, asemavyo Bwana: Panga za kuwaua, mbwa wa kuwakokotakokota, ndege wa angani na nyama wa porini wa kuwala na kuwamaliza.[#Ez. 14:21.]

4Nitawatoa, watupwe huko na huko katika nchi zote zenye wafalme kwa ajili ya mambo yote, Manase, mwana wa Hizikia, mfalme wa Yuda, aliyoyafanya Yerusalemu.[#2 Fal. 21:11-16; 23:26.]

5Yuko nani atakayekuhurumia, Yerusalemu? Yuko nani atakayekulilia? Au yuko nani atakayekufikia kukuuliza, kama unakaa vema?

6Ndivyo, asemavyo Bwana: Wewe umenitupa, ukarudi nyuma; ndipo, nilipoukunjua mkono wangu, ukukamate, nikakumaliza, maana nilikuwa nimechoka kuona uchungu.

7Kwa hiyo nimewapepeta ungoni kwenye malango ya nchi hii, nikawaua watoto wao, nikawaangamiza waliokuwa ukoo wangu, lakini hawakurudi katika njia zao.[#Mat. 3:12.]

8Nikiwahesabu wajane wao, ni wengi kuliko mchanga wa baharini; maana mwenye kuua mchana nimemleta kwao kwa mama wenye vijana, mara nikawaangushia mastuko na mashangao.

9Aliyezaa wana saba akazimia kwa uchungu, akakatika roho yake, kwa kuona soni na kujifunika jua lake likachwa, mchana ungaliko bado. Nayo masao yao nitayatoa, wauawe na panga za adui zao; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Amo. 8:9.]

Yeremia anajililia mwenyewe.

10Nilikuwa nimeapizwa, mama yangu aliponizaa! Nikawa mtu wa kugombezwa na wa kusutwa katika nchi hii yote nzima, nami sikukopesha wala sikukopa, nipate faida; nao wote huniapiza.[#Yer. 20:14.]

11Bwana amesema: Nitakutia nguvu kweli, uone mema! Kweli nitakupa kuwachokesha adui, siku zikiwa mbaya kwa kusongwa.

12Je? Yuko awezaye kuvunja chuma? kile chuma chenye shaba kitokacho kaskazini?

13Lakini kwanza nitazitoa mali zenu zote na vilimbiko vyenu vyote, wakunyang'anye pasipo kulipa cho chote kwa ajili ya makosa yenu yote, mliyoyafanya katika mipaka yenu yote.

14Nitawahamisha kwenda na adui zenu katika nchi, msiyoijua; kwani moto umewashwa na makali yangu, nao unataka kuwala.

Yeremia anatulizwa.

15Bwana, wewe unanijua, nikumbuke! Unipatilizie na kunilipizia wanaonikimbiza! Usiwavumilie! Nipokee mimi! Ujue, ya kuwa ninatukanwa kwa ajili yako!

16Maneno yako yalipooneka yalikuwa chakula changu; hayo maneno yako yakaufurahisha moyo wangu na kuuchangamsha. Kwani ninakwita kwa Jina lako, Bwana uliye Mungu Mwenye vikosi.[#Ez. 3:1-3.]

17Sikukaa kwenye wafyozaji kucheka nao; kwa kushikwa na mkono wako nilikaa peke yangu, kwani walinijaza machafuko.

18Mbona maumivu yangu hayakomi? Mbona kidonda changu ni kibaya sana kwa kukataa kupona? Utaniwia kama kijito kidanganyacho au kama maji yasiyotegemeka?[#Yer. 30:12.]

19Kweli hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Utakaporudi, ndipo, nitakapokurudisha, usimame tena usoni pangu! Nao wapaswao na macheo utakapowatoa kwao wasiofaa, ndipo, utakapokuwa kama kinywa changu, ndipo, wale watakaporudi upande wako, wewe usiporudi upande wao.

20Nami nitakupa kuwawia wao wa ukoo huu boma la shaba lenye nguvu, wasikushinde wakikupelekea vita, kwani mimi niko pamoja na wewe, nikuokoe na kukuponya; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yer. 1:18.]

21Nitakuponya mikononi mwao wabaya, nitakukomboa mikononi mwao wakorofi.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania