Yeremia 16

Yeremia 16

Vinyago vyao vinawaponza Wayuda.

1Neno la Bwana likanijia kwamba:

2Usijichukulie mke, usizae wana wa kiume wala wa kike mahali hapa!

3Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema kwa ajili ya wana wa kiume na wa kike wanaozaliwa mahali hapa na kwa ajili ya mama zao waliowazaa na kwa ajili ya baba zao waliowazaa katika nchi hii:

4Watakufa kwa magonjwa mabaya, hawataombolezewa, wala hawatazikwa, ila watakuwa tu kama kinyesi juu ya nchi; wengine watauawa kwa panga na kwa njaa, nayo mizoga yao itakuwa chakula cha ndege wa angani na cha nyama wa porini.

5Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Usiingie nyumbani mwenye maombolezo, wala usiende kuwalilia, wala usiwakalie matanga! Kwani nimeuondoa utengemano wangu kwao walio ukoo huu, nisiwagawie chema, wala nisiwahurumie; ndivyo, asemavyo Bwana.

6Watakufa wakubwa na wadogo katika nchi hii pasipo kuzikwa, tena hakuna watakaowalilia wala watakaojikata chale wala watakaonyoa vichwa.

7Wala hakuna watakaowagawia vyakula, wakikaa matanga, wala watakaowatuliza mioyo kwa ajili ya mfu, wala hakuna watakaowanywesha vikombe vya kuwatuliza mioyo wakifiwa na baba au mama.

8Namo nyumbani mwenye karamu usimwingie kukaa nao, mkila, mkinywa!

9Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Mtaniona na macho yenu siku hizi zenu, nikikomesha mahali hapa sauti za vicheko na sauti za furaha, hata sauti za wachumba wa kiume na wa kike.[#Yer. 7:34.]

10Itakuwa, utakapowapasha wao wa ukoo huu habari hizi zote, watakuuliza: Kwa sababu gani Bwana anatutakia haya mabaya yote yaliyo makuu? Tumekora manza gani? Bwana Mungu wetu, tumekosa makosa gani?

11Ndipo, utakapowaambia: Ndivyo, asemavyo Bwana: Kwa kuwa baba zenu waliniacha, wakafuata miungu mingine, wakaitumikia na kuiangukia, lakini mimi waliniacha, hawakuyashika Maonyo yangu.

12Nanyi hamkufanya mabaya kuliko baba zenu? Ninawaona, mkiufuata kila mtu ushupavu wa moyo wake mbaya pasipo kunisikia mimi.[#Yer. 7:24-26.]

13Kwa hiyo nitawaondoa katika nchi hii na kuwabwaga katika nchi, msiyoijua ninyi wala baba zenu! Ndiko, mtakakoweza kuitumikia miungu mingine mchana na usiku, kwa kuwa sitaki kuwahurumia tena.

Mungu atawaokoa Wayuda huko, walikotupiwa.

14Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaona kweli, siku zikija, watu watakapoacha kuapa wakisema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima aliyewatoa wana wa Isiraeli katika nchi ya Misri![#Yer. 23:7-8.]

15Ila wataapa wakisema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima aliyewatoa wana wa Isiraeli katika nchi ya upande wa kaskazini na katika nchi zote, alikowatupia! Maana nitawarudisha katika nchi yao, niliyowapa baba zao.

16Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaniona, nikituma wavuvi wengi, wawavue! Kisha nitatuma wawinda wengi, wawawinde katika milima yote na katika vilima vyote na katika nyufa zota za miamba.

17Kwani macho yangu huziona njia zenu zote, hazifichiki usoni pangu, wala manza zao, walizozikora, hazifunikiki machoni pangu.

18Lakini kwanza nitawalipisha mara mbili manza zao na makosa yao, kwa kuwa wameichafua nchi yangu kwa mizoga ya matapisho yao, fungu langu wakalijaza machukizo yao.

19Bwana ndiwe nguvu yangu na ngome yangu na kimbilio langu siku ya masongano; wewe watakujia wamizimu wakitoka mapeoni kwa nchi, watakuambia: Baba zetu waliyokuwa nayo, ni mambo ya uwongo tu yasiyo maana, yasiyowafalia kitu.

20Je? Mtu atawezaje kujitengenezea miungu? Kweli siyo miungu!

21Mtaona kweli, nikiwajulisha mara hii, nikiwapa kuujua mkono wangu na uwezo wangu; ndipo, watakapojua, ya kuwa Jina langu ni Bwana.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania