Yeremia 17

Yeremia 17

Mapatilizo yao watumikiao vinyago na watu na mambo madanganyifu.

1Ukosaji wa Yuda umeandikwa kwa kalamu ya chuma yenye ncha kali kama ya jiwe la almasi; mbao ulimochorwa ni mioyo yao na pembe za meza za kutambikia.

2Kwa hiyo wana wao huzikumbuka meza zao za kutambikia na vinyago vyao vya Ashera, wanapoona mti wenye majani mengi au wanapofika vilimani juu.

3Mlima wangu ulioko shambani na mali zako na vilimbiko vyako vyote vilivyoko vilimani nitavitoa, vipokonywe, kwa ajili ya makosa yako, uliyoyakosa katika mipaka yako yote.

4Nawe kwa ajili yako mwenyewe huna budi kulihama fungu lako, nililokupa, nami nitakutumikisha, uwatumikie adui zako katika nchi, usiyoijua, kwani makali yangu nimeyawakisha moto, usizimike kale na kale.[#Yer. 15:14.]

5Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Ameapizwa kila mtu amwegemeaye mtu mwenziwe akimtumia mwenye mwili kuwa mkono wake na kumwondoa Bwana moyoni mwake![#Sh. 118:8; 146:3.]

6Atakuwa kama mti wa jangwani usio na majani, hataona jema lo lote, likimjia; atakaa nyikani pakavu penyewe penye chumvi, pasipokaa mtu.[#Yer. 48:6.]

7Amebarikiwa kila mtu amwegemeaye Bwana, Bwana akiwa egemeo lake![#Sh. 146:5.]

8Atakuwa kama mti uliopandwa penye maji upelekao mizizi yake mpaka mtoni; hauogopi, ijapo jua kali liufikie; majani yake hustawi vivyo hivyo; ijapo mwaka ukose mvua, hausumbuki, wala haukomi kuzaa matunda.[#Sh. 1:3.]

9Moyo wa mtu hudanganya kuliko mengine yote, tena huponza; yuko nani aujuaye?

10Mimi Bwana ninauumbua moyo nikiyajaribu mafigo, nimpe kila mtu yazipasayo njia zake na mapato ya matendo yake.[#Sh. 7:10; Rom. 2:6.]

11Kama kwale anayelalia mayai, asiyoyataga, ndivyo, alivyo apataye mali kwa kupotoa watu; siku zake zitakapofika kati, zitampotelea, naye mwisho atapumbaa tu.[#Sh. 39:7.]

12Wewe kiti chenye utukufu umetukuka tangu mwanzo, ndipo mahali petu patakatifu,

13wewe Bwana u kingojeo cha Waisiraeli; wote wakuachao hupatwa na soni, waondokao kwako huandikwa wakingaliko nchini, ya kuwa wamemwacha Bwana aliye kisima chenye maji ya uzima.[#Yer. 2:13.]

14Niponye, Bwana! Ndivyo, nitakavyopona. Niokoe! Ndivyo, nitakavyookoka; kwani wewe ndiwe shangilio langu.

15Watazame wanaoniambia: Neno lake Bwana liko wapi? Na lije![#Yes. 5:19.]

16Mimi sikujitoa katika uchungaji, nisikufuate, wala sikutaka, siku yenye uchungu iwajie, kama wewe unavyojua; yaliyotoka midomoni mwangu yako wazi usoni pako.

17Usiniangamize, wewe uliye kimbilio langu, siku ikiwa mbaya!

18Na wapatwe na soni wanikimbizao, nisipatwe na soni mimi! Na waangamie wao, nisiangamie mimi! Uwaletee wao siku mbaya! Mara mbili uwavunje, wavunjike kweli!

Sharti waitakase siku ya Bwana!

19Hivi ndivyo, Bwana alivyoniambia: Nenda kusimama langoni mwao walio wazaliwa wa ukoo huu, wafalme wa Yuda walimopitia wakiingia au wakitoka, hata malangoni mote mwa Yerusalemu,

20kawaambie: Lisikieni neno la Bwana, ninyi wafalme wa Yuda nanyi Wayuda nyote nanyi nyote mkaao Yerusalemu mnaopitia humu malangoni!

21Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Ziangalieni roho zenu, msichukue mzigo siku ya mapumziko mkiuingiza humu malangoni mwa Yerusalemu!

22Wala msitoe mzigo nyumbani mwenu siku ya mapumziko! Wala msifanye kazi yo yote! Ila itakaseni siku ya mapumziko, kama nilivyowaagiza baba zenu![#Yes. 56:2; 58:13.]

23Lakini hawakusikia, wala hawakuyatega masikio yao, wakazishupaza kosi zao, wasisikie, wasionyeke.[#Yer. 11:8.]

24Ndivyo, asemavyo Bwana: Sasa ninyi nisikieni, msiingize mzigo malangoni mwa mji huu siku ya mapumziko! Ila itakaseni siku ya mapumziko, msipoifanyizia kazi yo yote!

25Ndipo, watakapoingia humu malangoni mwa mji huu wafalme wanaokikalia kiti cha kifalme cha Dawidi na wakuu wanaopanda magari na farasi, wao wenyewe na wakuu wao, Wayuda nao wakaao Yerusalemu, nao mji huu utakaa kale na kale.

26Tena watakuja wakitoka katika miji ya Yuda na katika nchi zizungukazo Yerusalemu na katika nchi ya Benyamini, kwenye mbuga na kwenye milima, hata upande wa kusini, wataleta ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za kuchinjwa na vipaji vingine vya tambiko na uvumba, wataviingiza Nyumbani mwa Bwana, wamshukuru.

27Lakini msiponisikia mkiacha kuitakasa siku ya mapumziko, mkaingia malangoni mwa Yerusalemu na kuchukua mizigo siku ya mapumziko, basi, nitawasha moto malangoni mwake, nao utayala majumba ya Yerusalemu pasipo kuzimika.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania