Yeremia 18

Yeremia 18

Mfano wa mfinyanzi.

1Hili ndilo neno lililomjia Yeremia likitoka kwake Bwana kwamba:

2Inuka, ushuke kwenda nyumbani mwa mfinyanzi. Ndimo, nitakamokuambia maneno yangu.

3Nikashuka kwenda nyumbani mwa mfinyanzi, nikamkuta, akifanya kazi kwenye kibao chake.

4Chombo, mfinyanzi alichokifanya na mkono wake, kisipokuwa chema, basi, akakitengeneza kuwa chombo kingine, kama ilivyofaa machoni pake mfinyanzi kukifanya.

5Neno lake Bwana likanijia kwamba:

6Kama huyu mfinyanzi nami siwezi kuwafanyizia ninyi mlio mlango wa Isiraeli? ndivyo, asemavyo Bwana. Tazameni: kama udongo ulivyo mkononi mwa mfinyanzi. ndivyo, ninyi mlio mlango wa Isiraeli mlivyo mkononi mwangu.[#Yes. 45:9; Rom. 9:21.]

7Mara ninatisha taifa au ufalme kwamba: Nitawang'oa na kuwavunja na kuwaangamiza.[#Yer. 1:10.]

8Lakini taifa hilo, nililolitisha, likigeuka na kuuacha ubaya wake, nami nitageuza moyo, nisiwafanyizie hayo mabaya, niliyoyawaza kuwafanyizia.[#Yer. 26:3,19; Yona 3:10.]

9Mara ninaagiza taifa au ufalme kuwajenga na kuwapanda

10Lakini wakifanya yaliyo mabaya machoni pangu, wasiisikie sauti yangu, basi, nitageuza moyo, nisiwafanyizie hayo mema, niliyoyasema, niwafanyizie.

11Sasa uwaambie walio Wayuda nao wakaao Yerusalemu kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Tazameni, mimi ninawatengenezea mabaya kwa kuwawazia mawazo! Kwa hiyo rudini kila mtu katika njia yake mbaya, mshike njia zitakazowafaa, mfanye matendo mema![#Yer. 7:3; 25:5.]

12Lakini hujibu: Ni kazi bure! Kwani tutaendelea kuyafuata mawazo yetu, tufanye kila mtu yaupasayo ushupavu wa moyo wake mbaya![#Yer. 3:17; 6:16.]

13Kwa hiyo Bwana anasema hivyo: Ulizeni kwa wamizimu, kama yuko aliyesikia mambo kama hayo! Wanawali wa Isiraeli wamefanya mambo yazizimuayo kabisa.

14Je? Theluji ya Libanoni inaondoka katika ile miamba iliyoko kileleni juu ya kondeni? Je? Yanakauka maji yenye baridi ya vijito vitokavyo mbali?

15Lakini walio ukoo wangu wamenisahau, huvukizia miungu isiyo kitu, nayo ikawaangusha katika njia zao, walizozishika tangu kale, wakafuata mikondo isiyotengenezwa kuwa njia.

16Wakaigeuza nchi yao kuwa mapori tu, izomelewe kale na kale; kila atakayeipita ataistukia, wataitingishia vichwa vyao.

17Kama upepo utokao maawioni kwa jua unavyofanya, nitawatawanya machoni pa adui; ndio mgongo, sio uso, nitakaowaonyesha siku ya kuangamia kwao.[#Yer. 2:27.]

Njama ya kumwua Yeremia na kuomba kwake.

18Wakasema: Njoni, tumlie Yeremia njama ya kumwazia mawazo! Kwani maonyo hayampotelei mtambikaji, wala mizungu haimpotelei mjanja, wala maneno hayampotelei mfumbuaji. Haya! Tumpige tukiyatumia, ulimi wake uliyoyasema! Tusiyasikilize maneno yake yote!

19Bwana, nisikilize! Isikie sauti ya wapingani wangu![#Sh. 35:7.]

20Je? Mema yanalipwa na kufanyiziwa mabaya? Wamenichimbia mwina; kumbuka, jinsi nilivyosimama mbele yako na kuwasemea mema, niyatulize makali yako yenye moto, yasiwatokee!

21Kwa hiyo watoe wana wao, wauawe na njaa, kawabwage kwenye panga, wanawake wao wawe pasipo watoto na pasipo waume! Waume wao na wauawe na kifo, vijana wao na wapigwe na panga za vitani!

22Nyumbani na msikilike vilio, ukiwastusha kwa kuwaletea vikosi vya wapiga vita! Kwani wamenichimbia mwina, wanikamate, miguu yangu wakaitegea matanzi.

23Wewe Bwana, unaijua njama yao yote ya kuniua; usizifunike manza zao, wala usiyafute makosa yao usoni pako, wawe wameangushwa usoni pako! Siku, makali yako yatakapowakia, wapigie shauri![#Sh. 109:14-15.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania