Yeremia 19

Yeremia 19

Mfano wa mtungi uliovunjwa.

1Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Nenda, ujinunulie mtungi kwa mfinyanzi! Kisha chukua wazee wa watu na wazee wa watambikaji,

2utoke nao kwenda katika bonde la Mwana wa Hinomu lililoko mbele ya Lango la Vigae, utangaze huko maneno, nitakayokuambia![#Yer. 7:31; 19:11.]

3Uwaambie: Lisikilizeni neno la Bwana, ninyi wafalme wa Yuda nanyi mkaao Yerusalemu! Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Mtaniona, nikipaletea mahali hapa mabaya; kila atakayeyasikia masikio yake yatavuma.[#1 Sam. 3:11; 2 Fal. 21:12.]

4Ni kwa sababu wameniacha, mahali hapa wakampa mgeni, wakavukizia hapa miungu mingine, wasiyoijua wenyewe, wala baba zao, wala wafalme wa Yuda, wakapajaza mahali hapa damu zao wasiokosa.

5Wakamjengea Baali pa kumtambikia vilimani juu, wateketeze wana wao motoni kuwa ng'ombe za tambiko za Baali; nami sikuwaagiza hivyo, wala sikuvisema nao, wala havikunijia moyoni.[#Yer. 7:31-32.]

6Kweli ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaona, siku zikija, mahali hapa pasiitwe tena Tofeti wala Bonde la Mwana wa Hinomu, ila Bonde la Uuaji.

7Ndipo, nitakapoiumbua miungu ya Wayuda na ya Wayerusalemu mahali hapo nikiwatoa, waangushwe na panga machoni pa adui zao kwa mikono yao waliozitafuta roho zao, nayo mizoga yao nitawapa ndege wa angani na nyama wa porini, iwe chakula chao.[#Yer. 7:33.]

8Nao mji huu nitaugeuza kuwa mapori tu, uzomelewe kabisa; kila atakayepapita ataustukia, atauzomea kwa ajili ya mapigo yake yote.[#Yer. 18:16.]

9Nitawalisha nyama za wana wao wa kiume na nyama za wana wao wa kike, watazila kila mtu nyama za mwenziwe kwa kusongeka na kwa kuhangaika, adui zao wanaozitaka roho zao wakiwahangaisha.[#5 Mose 28:53.]

10Kisha utauvunja mtungi machoni pao waume waliokwenda na wewe,

11ukiwaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Hivi ndivyo, nitakavyowavunja walio wa ukoo huu nao mji huu, kama mtu anavyokivunja chombo cha mfinyanzi kisichowezekana kuwa kizima tena. Nako Tofeti ndiko, watakakozikia, kwa kukosa pengine pa kuzikia.[#Yes. 30:14; Yer. 7:32.]

12Ndivyo, asemavyo Bwana: Hivi ndivyo, nitakavyopafanyizia mahali hapa nao wakaao hapa nitakapoutoa mji huu, uwe kama Tofeti.

13Ndipo, nyumba za Yerusalemu na nyumba za wafalme wa Yuda zitakapokuwa zimetiwa uchafu kama mahali pa Tofeti, Zitakazokuwa hivyo ni nyumba zote, walimovukizia vikosi vyote vya mbinguni madarini juu, walimomwagia miungu mingine vinywaji vya tambiko.[#Yer. 32:29; Sef. 1:5.]

14Yeremia aliporudi toka Tofeti, Bwana alikomtuma kuwafumbulia watu, akaja kusimama uani pake Nyumba ya Bwana, akawaambia watu wote waliokuwako:

15Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Mtaniona, nikiuletea mji huu navyo vijiji vyake vyote mabaya yote, niliyoyasema, kwani wamezishupaza kosi zao, wasiyasikie maneno yangu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania