Yeremia 20

Yeremia 20

Yeremia anawafumbulia, jinsi watakavyohamishwa kwenda Babeli.

1Mtambikaji Pashuri, mwana wa Imeri, aliyekuwa msimamizi mkuu wa Nyumba ya Bwana, akamsikia Yeremia, alipoyafumbua maneno yale.

2Ndipo, Pashuri alipompiga mfumbuaji Yeremia, akamfunga kwa mikatale iliyokuwa kwenye lango la juu la Benyamini katika Nyumba ya Bwana.

3Kulipokucha Pashuri akamfungua Yeremia tena katika mikatale; ndipo, Yeremia alipomwambia: Bwana hatakuita tena jina lako Pashuri, ila Magori-Misabibu (Kitisho po pote).

4Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Utaniona, nikikutoa kuwa kitisho kwako wewe nako kwao wote wakupendao, maana wataangushwa kwa panga za adui zao, nayo macho yako yataviona! Nao Wayuda wote nitawatia mkononi mwa mfalme wa Babeli, atawahamisha kwenda Babeli akiwapiga kwa upanga.

5Nazo mali zote za mji huu nitazitoa, na mapato yao yote na vitu vyao vyote vyenye kiasi kikubwa na vilimbiko vyote vya mfalme wa Yuda, nitavitia mikononi mwa adui zao, wavipokonye, wavichukue na kuvipeleka Babeli.[#Yes. 39:6.]

6Wewe Pashuri nawe nao wote wakaao nyumbani mwako mtakwenda kwa kutekwa, utafika Babeli, utakufa huko, utazikwa huko wewe na wapenzi wako wote, uliowafumbulia maneno ya uwongo.

Kilio cha Yeremia.

7Bwana umenishinda, nami nimeshindika; umenishika kwa nguvu, ukaniweza. Ninachekwa mchana kutwa, wote wananifyoza.[#Yer. 1:7.]

8Kwani ninaposema ninalia; sina budi kutangaza ukorofi na upotovu, kwani Neno la Bwana hunipatia kutukanwa na kufyozwa mchana kutwa.[#Yes. 49:4.]

9Kwa hiyo nilisema: Sitamkumbuka, wala sitasema tena katika Jina lake, basi, ikawa moyoni mwangu kama moto uwakao kwa kufungiwa katika mifupa yangu, nikashindwa kuuvumilia, sikuweza kabisa.

10Kwani nimesikia wengi, wakinong'onezana kwamba: Anatishwa po pote, mchongeeni! Nasi na tumchongee! Hiyo ni njama yao wote walio rafiki zangu, hunivizia, nianguke, kwamba: Labda atashindwa, tumweze nasi, tupate kujilipiza kwake.[#Sh. 31:14.]

11Lakini Bwana yuko pamoja nami kama mpiga vita mwenye nguvu; kwa hiyo wanikimbizao watajikwaa, wasiniweze, watapatwa na soni kabisa, kwani hawaerevuki, soni zao zitakuwa za kale na kale, hazitasahauliwa.[#Yer. 1:8,19; 15:20.]

12Wewe Bwana unajaribu mwongofu, unayaona mafigo na moyo; na nione, jinsi unavyowalipiza kisasi, kwani nimekusukumia wewe shauri langu.[#Yer. 11:20.]

13Mwimbieni Bwana! Mshangilieni Bwana! Kwani huiponya roho ya mkiwa mikononi mwao wafanyao mabaya.

14Siku niliyozaliwa iwe imeapizwa! Siku, mama yangu aliyonizaa, isibarikiwe![#Yer. 15:10; Iy. 3:1-10; 10:18.]

15Awe ameapizwa naye mtu aliyempasha baba yangu habari kwamba: Umezaliwa mtoto wa kiume! akamfurahisha.

16Mtu huyo na awe kama ile miji, Bwana aliyoiangamiza pasipo kugeuza moyo! Asubuhi na asikie vilio, tena makelele, jua linapofika kichwani,[#1 Mose 19:24-25.]

17kwa kuwa hakunifisha tumboni mwa mama; hivyo mama angalikuwa kaburi langu, hiyo mimba yake ingalikuwa ya siku zote.

18Mbona nilitoka tumboni kuona masumbufu na machungu, siku zangu zikamalizika, nikipatwa na soni tu?

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania