The chat will start when you send the first message.
1Yatawapata wachungaji wanaowaangamiza na kuwatawanya kondoo, niliowapa kuwachunga! ndivyo, asemavyo Bwana.[#Ez. 13:2-16; 34; Zak. 11:5.]
2Hivi ndivyo kweli, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema kwa ajili ya wachungaji. Ninyi mnaowachunga walio ukoo wangu, mmewatawanya kondoo wangu na kuwakimbiza, hamkuwaangalia; mtaniona, nikiwapatilizia ubaya wa matendo yenu; ndivyo, asemavyo Bwana.
3Nami nitawakusanya masao ya kondoo wangu na kuwatoa katika nchi zote, nilikowaendesha na kuwakimbiza, Nitawarudisha katika makao yao, wazae, wawe wengi tena.
4Kisha nitawawekea wachungaji, wawachunge; hawataogopa tena, wala hawatastuka, wala hawatapotea hata mmoja wao; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yer. 3:15.]
5Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaona, siku zitakapokuja, nikimwinulia Dawidi chipuko lenye wongofu, naye atakuwa mfalme ajuaye vema kutawala, maana atafanya katika nchi yaliyo sawa yaongokayo.[#Zak. 3:8; 6:12; Yes. 32:1.]
6Yuda ataokolewa katika siku zake, naye Isiraeli atakaa salama. Jina lake, watakalomwita, ni hili: Bwana ni wongofu wetu![#Yer. 33:16.]
7Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaona kweli, siku zikija, watakapoacha kuapa wakisema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima aliyewatoa wana wa Isiraeli katika nchi ya Misri,[#Yer. 16:14-15.]
8ila wataapa wakisema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima aliyewaleta wazao wa mlango wa Isiraeli akiwatoa katika nchi ya upande wa kaskazini na katika nchi zote, nilikowaendesha na kuwakimbiza; ndipo, watakapokaa huku katika nchi yao.
9Kwa wafumbuaji. Moyo wangu umevunjika kifuani mwangu, mifupa yangu yote ikatetemeka; nikawa kama mlevi au kama mtu ashindwaye na mvinyo, nilipoyasikia yaliyotoka kwake Bwana, hayo maneno yake matakatifu kwamba:
10Nchi hii imezaa wazinzi, kwa hiyo nchi hii inakaa matanga kwa kuapizwa, mbuga za nyikani zimekauka, kwa kuwa ni mabaya, wanayoyakimbilia, nayo nguvu yao siyo ifaayo.
11Kwani nao wafumbuaji pamoja na watambikaji ni wapotovu, namo Nyumbani mwangu nimeuona ubaya wao; ndivyo, asemavyo Bwana.
12Kwa sababu hii njia yao itakuwa inateleza, penye giza watateleza na kuanguka hapohapo, kwani nitawaletea mabaya, ndio mwaka wa kupatilizwa kwao; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yer. 13:16; Sh. 35:6.]
13Hata kwa wafumbuaji wa Samaria nimeona upumbavu, wakifumbua kwa nguvu ya Baali, wakawapoteza nao walio ukoo wangu wa Isiraeli.
14Lakini kwa wafumbuaji wa Yerusalemu nimeona mastusho: huzini, huendelea na kudanganya, huitia mikono ya wabaya nguvu, wasiuache kila mtu ubaya wake, wote pia wameniwia kama Wasodomu, nao wakaao humo kama Wagomora.[#Ez. 13:22; Yes. 1:10.]
15Kwa hiyo Bwana Mwenye vikosi anasema hivyo kwa ajili ya wafumbuaji: Mtaniona, nikiwalisha majani machungu na kuwanywesha maji yenye sumu! Kwani kwa wafumbuaji wa Yerusalemu kumetoka upotovu, ukaziingia nchi zote.[#Yer. 9:15.]
16*Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Msiyasikie maneno ya wafumbuaji wanaowafumbulia maneno wakiwaegemeza mambo yaliyo ya bure tu! Huyasema, waliyoyaona mioyoni mwao, hawasemi yaliyotoka kinywani mwa Bwana.[#Yer. 6:14.]
17Huwaambia wanibezao: Bwana amesema: Mtakaa na kutengemana! Kila mtu aufuataye ushupavu wa moyo wake humwambia: Hakuna kibaya kitakachowafikia![#Yer. 7:24.]
18Kwani yuko nani aliyesimama penye njama ya Bwana, akimwona au akilisikia neno lake? Yuko nani aliyeliangalia Neno lake, akilisikia?[#Yes. 40:13.]
19Mtakiona kimbunga cha Bwana, hata makali yenye moto, yakitoka kwake, nao upepo wa chamchela wenye nguvu utawaangukia vichwani wao wasiomcha Mungu.[#Yer. 30:23.]
20Ukali wake Bwana hautatulia, mpaka ukiyafanya na kuyatimiza mawazo ya moyo wake; siku za mwisho mtayatambua haya.
21Sikuwatuma wafumbuaji hawa, nao hupiga mbio; sikuwaambia neno, nao hufumbua.[#Yer. 14:14.]
22Kama wangalikuwa wamesimama penye njama yangu, wangeyasema maneno yangu masikioni pao walio ukoo wangu, wangewarudisha wabaya katika njia zao, wauache ubaya wa matendo yao.
23Ndivyo asemavyo Bwana: Je? Mimi ni Mungu akaaye karibu tu? Si Mungu akaaye hata mbali?
24Ndivyo, asemavyo Bwana: Kama mtu anajificha mafichoni, mimi sitamwona? Si mimi azijazaye mbingu na nchi? ndivyo, asemavyo Bwana.
25Nimeyasikia, wafumbuaji waliyoyasema, wakifumbua maneno ya uwongo katika Jina langu wakisema: Nimeota! Nimeota!
26Hivyo vitakuwa mpaka lini mioyoni mwao wafumbuaji wafumbuao uwongo tu, walio wafumbuaji wa udanganyifu wa mioyo yao?
27Huwaza, ya kuwa watawasahaulisha walio ukoo wangu Jina langu kwa ajili ya ndoto zao, wakizisimuliana kila mtu na mwenziwe, kama baba zao walivyolisahau Jina langu kwa ajili ya Baali.
28Mfumbuaji aliyeota na asimulie ndoto! Naye aliyelisikia Neno langu na aliseme Neno langu, lilivyo kweli! Kumvi na mpunga ziko na fungu gani lililo lao pamoja? ndivyo, asemavyo Bwana.
29Ndivyo, asemavyo Bwana: Neno langu si kama moto au kama nyundo ipasuayo miamba?*[#Ebr. 4:12.]
30Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaniona kweli, nikiwajia wafumbuaji, kwa kuwa wanaliiba Neno langu kila mtu kwa mwenziwe!
31Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaniona, nikiwajia wafumbuaji, kwa kuwa huzitumia ndimi zao za kusema: Asema!
32Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaniona, nikiwajia wafumbuaji wa ndoto za uwongo. Huzisimulia walio ukoo wangu, wakawapoteza kwa uwongo wao na kwa mambo yao makuu, nami sikuwatuma, wala sikuwaagiza neno, nao walio wa ukoo huu hawawafalii kitu hata kidogo; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yer. 23:21.]
33Kama watakuuliza walio wa ukoo huu au mfumbuaji au mtambikaji kwamba: Tamko zito la Bwana ni nini? ndipo, utakapowajibu: Hili ndilo tamko zito la Bwana, akisema: Nitawabwaga ninyi! ndivyo, asemavyo Bwana.
34Lakini mfumbuaji na mtambikaji nao walio wa ukoo huu watakaolitumia neno hilo la kwamba: Tamko zito la Bwana, mtu huyo nitampatiliza pamoja na mlango wake.
35Hivyo ndivyo, mtakavyoulizana mtu na mwenziwe, hata mtu na ndugu yake kwamba: Bwana amejia nini? au: Bwana amesema nini?
36Tamko zito la Bwana wasilitaje tena! Kama wanalitaja, basi, kila mtu neno lake litamgeukia kuwa tamko zito, kwani ninyi huyageuza maneno ya Mungu aliye Mwenye uzima, aliye Bwana Mwenye vikosi, Mungu wetu.
37Hivi ndivyo, utakavyomwuliza mfumbuaji kwamba: Bwana amejibu nini? au: Bwana amesema nini?
38Lakini mkisema: Tamko zito la Bwana, basi, itakuwa hivyo, Bwana alivyosema: Kwa kuwa mnalisema neno hilo la kwamba: Tamko zito la Bwana, nami nilituma kwenu kuwakataza, msiseme: Tamko zito la Bwana!
39basi, mtaniona, nikiwaacha kabisa na kuwabwaga ninyi pamoja na mji huu, niliowapa ninyi na baba zenu, mtoke usoni pangu.
40Hivyo nitawatia soni za kale na kale na matusi ya kale na kale yasiyosahaulika.[#Yer. 20:11.]