The chat will start when you send the first message.
1Bwana alinionyesha, nikaona vikapu viwili vyenye kuyu, vilikuwa vimewekwa mbele ya Jumba la Bwana, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, alipokuwa amekwisha kumteka Yekonia, mwana wa Yoyakimu, mfalme wa Yuda, nao wakuu wa Yuda pamoja na mafundi wa seremala na wahunzi kuwatoa Yerusalemu na kuwapeleka Babeli.[#Yer. 29:2; 2 Fal. 24:14-15.]
2Kikapu kimoja kuyu zake zilikuwa nzuri kabisa, kama kuyu za malimbuko zilivyo; kikapu cha pili kuyu zake zilikuwa mbaya kabisa, hazikulika kwa ubaya wao.
3Bwana akaniuliza: Unaona nini, Yeremia? Nikamwambia: Kuyu; hizi kuyu nzuri ni nzuri kabisa, nazo hizi mbaya ni mbaya kabisa, haziliki kwa ubaya wao.[#Yer. 1:11,13.]
4Neno la Bwana likanijia kwamba:
5Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu wa Isiraeli: Kama hizi kuyu nzuri zinavyopendeza, ndivyo, nitakavyowatazama kwa kupendezwa Wayuda waliotekwa, niliowatuma kutoka mahali hapa kwenda katika nchi ya Wakasidi.
6Nitayaelekeza macho yangu, yawaangalie kwa kupendezwa nao, nitawarudisha katika nchi hii, nitawajenga, nisiwabomoe tena, nitawapanda, nisiwang'oe tena.[#Yer. 31:28.]
7Nitawapa mioyo ya kunijua, ya kuwa mimi ni Bwana, watakuwa ukoo wangu, nami nitakuwa Mungu wao, kwani watanigeukia kwa mioyo yote.[#Yer. 31:33-34.]
8Tena hivi navyo ndivyo, Bwana anavyosema: Kama zile kuyu zilivyo mbaya, zisilike kwa ubaya wao, ndivyo, nitakavyomtoa Sedekia, mfalme wa Yuda, na wakuu wake na masao ya Yerusalemu nao waliosalia katika nchi hii nao wakaao katika nchi ya Misri,[#Yer. 29:17.]
9nitawatoa, watupwe vibaya huko na huko katika nchi zote zenye wafalme huku ulimwenguni, watukanwe na kuzomelewa, wafyozwe na kuapizwa po pote, nitakapowatupa.[#Yer. 29:18.]
10Nitatuma kwao panga na njaa na magonjwa mabaya, mpaka watakapomalizika na kutoweka katika nchi, niliyowapa wao na baba zao.