Yeremia 25

Yeremia 25

Wayuda watatumikishwa Babeli miaka 70.

1Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kwa ajili ya ukoo wote wa Yuda katika mwaka wa nne wa Yoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, nao ulikuwa mwaka wa kwanza wa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli.

2Naye mfumbuaji Yeremia akaliambia wao wote wa ukoo wa Yuda nao wote wakaao Yerusalemu kwamba:

3Kuanzia mwaka wa kumi na tatu wa Yosia, mwana wa Amosi, mfalme wa Yuda, mpaka siku hii ya leo, hii miaka ishirini na mitatu yote neno la Bwana limenijia, nikawaambia pasipo kuchoka kila kulipokucha, lakini hamkusikia.

4Naye Bwana alituma kwenu watumishi wake wote waliokuwa wafumbuaji, naye aliwatuma pasipo kuchoka kila kulipokucha, lakini hamkusikia, wala hamkuyatega masikio yenu, mpate kusikia.

5Nao wakasema: Rudini kila mtu katika njia yake mbaya na kuyaacha matendo yenu mabaya! Ndipo, mtakapokaa katika nchi, Bwana aliyowapa ninyi na baba zenu, iwe yenu ya kale na kale kabisa.[#Yer. 18:11.]

6Msiifuate miungu mingine kuitumikia na kuiangukia, wala msinikasirishe kwa matendo ya mikono yenu, nisiwafanyizie mabaya.

7Lakini hamkunisikia, mkataka kunikasirisha kwa matendo ya mikono yenu, yakawapatia mabaya; ndivyo, asemavyo Bwana.

8Kweli hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Kwa kuwa hamkuyasikia maneno yangu,

9mtaniona, nikituma wa kuzichukua koo zote za watu wa upande wa kaskazini. Ndivyo, asemavyo Bwana: Nitatuma hata kwa mtumishi wangu Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, nitamleta katika nchi hii kuwapiga wakaao huku nayo mataifa haya yote ya nchi ziwazungukazo; nitawatowesha nikiwatoa, wamalizwe kabisa na kuzomelewa, pawe mavunjiko ya kale na kale.[#Yer. 27:6.]

10Nitapoteza kwao sauti za vicheko na sauti za furaha, hata sauti za wachumba wa kiume na wa kike, hata milio ya mawe ya kusagia, hata mwanga wa taa.[#Yer. 16:9.]

11Nchi hii yote itakuwa mavunjiko kwa kukaa peke yake. Nao watu wa mataifa haya watamtumikia mfalme wa Babeli miaka 70.[#Yer. 29:10; 2 Mambo 36:21; Ezr. 1:1; Dan. 9:2.]

Kuangamia kwa Babeli.

12Ndivyo, asemavyo Bwana: Itakuwa, miaka 70 itakapopita, nitampatilizia mfalme wa Babeli na lile kabila lote mabaya yao, waliyoyafanya; hata nchi yao Wakasidi nitaigeuza kuwa peke yake tu kale na kale.

13Nitailetea nchi ile maneno yangu yote, niliyoyasema ya kuifanyizia, yaliyoandikwa humu kitabuni, mfumbuaji Yeremia aliyoyafumbua kwamba: Yatawajia hawa wamizimu wote.

14Kwani mataifa yenye watu wengi na wafalme wakuu watawatumikisha hawa nao, nami nitawalipisha kazi zao na matendo ya mikono yao.

Makali yatakayoyatokea makabila ya watu.

15Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli alivyoniambia: Kitwae mkononi mwangu kinyweo hiki cha mvinyo yenye ukali wa moto, ukinyweshe makabila yote ya watu, ambao nitakutuma kwenda kwao.[#Yer. 51:7; Yes. 51:17; Ufu. 14:10.]

16Watakapokinywa watapepesuka kwa kuingiwa na wazimu kwa ajili ya upanga utakaotumwa kwao.

17Nikakitwaa hicho kikombe mkononi mwake Bwana, nikakinywesha makabila yote ya watu, ambao Bwana alinituma kwenda kwao.

18Yerusalemu na miji ya Yuda na wafalme wao na wakuu wao kikawapatia mavunjiko na maangamizo na mazomeo na maapizo, kama vilivyo hata leo.

19Kisha nikamnywesha Farao, mfalme wa Misri, na watumishi wake na wakuu wake na watu wake wote,

20nao wote waliochangana nao wafalme wote wa nchi ya Usi na wafalme wote wa nchi ya Wafilisti, hata Askaloni na Gaza na Ekroni na masao ya Asdodi,

21hata Waedomu na Wamoabu na wana wa Amoni,

22nao wafalme wote wa Tiro na wafalme wote wa Sidoni na wafalme wa nchi za pwani ng'ambo ya bahari,

23Wadedani na Watema na Wabuzi nao wote wakatao nywele za panjani,[#Yer. 9:26.]

24nao wafalme wote wa Arabuni na wafalme wote wa watu waliochangana nao wakaao nyikani,

25na wafalme wote wa Zimuri na wafalme wote wa Elamu na wafalme wa Wamedi,

26na wafalme wote wa nchi za upande wa kaskazini, walioko karibu nao walioko mbali, kila mtu na ndugu yake; hivyo nikawanywesha wote wenye nchi za kifalme zilizoko huku ulimwenguni; lakini mfalme wa Sesaki (Babeli) atakunywa nyuma yao wote.[#Yer. 51:41.]

27Nawe utawaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Nyweni, mpaka mlewe na kutapika! Mtaanguka, msiweze kuinuka tena kwa ajili ya upanga, mimi ninaotaka kuutuma kwenu.

28Kama wanakataa kukitwaa hicho kikombe mkononi mwako, wasikinywe, ndipo, utakapowaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Hamna budi kukinywa!

29Kwani mmeona, nilivyoanza kuufanyizia mabaya ule mji ulioitwa kwa Jina langu, nanyi mpone kabisa? Hamtapona, kwani upanga, ninaouita mimi, utawajia wote wakaao ulimwenguni; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi.[#Yer. 49:12; 1 Petr. 4:17.]

30Kisha wewe utawafumbulia maneno haya yote ukiwaambia: Bwana atanguruma huko juu na kupaza sauti yake katika Kao lake takatifu akiyangurumia malisho yake; atapiga yowe kama wakamuliaji wa zabibu atakapowajia watu wote wakaao huku ulimwenguni.[#Hos. 11:10; Yoe. 3:16; Amo. 1:2.]

31Mlio wake utakwenda kufika mapeoni kwa nchi, kwani Bwana atawakatia makabila ya watu shauri lake, yeye atawahukumu wote wenye miili, nao wasiomcha atawatoa, wauawe na upanga ule; ndivyo, asemavyo Bwana.

32Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Mtaona, mabaya yakitoka kwa kabila moja kufikia jingine, nao upepo wenye nguvu nyingi utainuka mapeoni kwa nchi, utokee.

33Siku ile itakuwa, waliouawa na Bwana walale po pote toka mwanzo wa nchi kuufikia mwisho wa nchi, hawataombolezewa, wala hawataokotwa, wala hawatazikwa, watakuwa kinyesi tu juu ya nchi.[#Yer. 7:33.]

34Pigeni makelele, ninyi wachungaji, na kulia sana! Gaagaeni mavumbini, ninyi viongozi wa makundi! Kwani siku zenu zimetimia za kuchinjwa, nami nitawaponda, mwanguke chini kama chombo kilichopendeza.[#Yer. 23:1.]

35Ndipo, kimbilio litakapowapotelea wachungaji, nao viongozi wa makundi hawatapata pa kuponea.

36Sauti za vilio vya wachungaji na makelele ya viongozi wa makundi yatasikilika hapo, Bwana atakapoyaharibu malisho yao.

37Nazo mbuga zile nzuri za kutulia hapo zitakuwa kimya pasipo sauti yo yote kwa ajili ya moto wa makali yake Bwana.

38Atakuwa ametokea kama simba akiondoka kichakani. Kweli nchi yao itakuwa imegeuka kuwa mapori tu kwa ukali wa moto wa Mwenye nguvu, ndio moto wa makali yake.[#Yer. 4:7.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania