Yeremia 26

Yeremia 26

Kufungwa na kufunguliwa kwake Yeremia.

1*Katika mwanzo wa ufalme wa Yoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, ndipo, neno hili lilipotoka kwake Bwana kwamba:

2Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Simama uani pa Nyumba ya Bwana, nao watu wa miji yote watakaopaingia kutambika Nyumbani mwa Bwana uwaambie maneno yote, niliyokuagiza kuwaambia, usipunguze hata neno moja.

3Labda watasikia, warudi kila mmoja katika njia yake mbaya, nipate kugeuza moyo kwa ajili ya mabaya, niliyoyawaza kuwafanyizia kwa matendo yao mabaya.[#Yer. 36:3.]

4Nawe utawaambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Msiponisikia, msipoendelea kuyashika Maonyo yangu, niliyowapa ninyi, yawe machoni penu,

5msipoyashika maneno ya wafumbuaji walio watumishi wangu, mimi ninaowatuma kwenu pasipo kuchoka kila kunapokucha, msipowasikia,[#Yer. 25:4.]

6nitaigeuza Nyumba hii kuwa kama Silo, nao mji huu nitautoa, uapizwe na mataifa yote yaliyoko ulimwenguni.[#Yer. 7:12-14; 1 Sam. 4:4,12.]

7Watambikaji na wafumbuaji na watu wote wa ukoo huu wakamsikia Yeremia, alipoyasema maneno haya katika Nyumba ya Bwana.

8Yeremia alipokwisha kuyasema yote, Bwana aliyomwagiza kuwaambia watu wote wa ukoo huu, ndipo, watambikaji na wafumbuaji na watu wote wa ukoo huu walipomkamata wakisema: Sharti ufe kabisa!

9Mbona umetufumbulia katika Jina la Bwana kwamba: Nyumba hii itakuwa kama Silo, nao mji huu utakuwa mavunjiko, usikae mtu? Kisha watu wote wa ukoo huu wakamkusanyikia Yeremia katika Nyumba ya Bwana.

10Wakuu wa Yuda walipoyasikia maneno haya wakatoka nyumbani mwa mfalme, wakapanda kwenda katika Nyumba ya Bwana, wakakaa kwenye mlango mpya wa Bwana.

11Watambikaji na wafumbuaji wakawaambia wakuu na watu wote wa ukoo huu, wakasema: Mtu huyu anapaswa na hukumu ya kuuawa, kwani mji huu ameufumbulia maneno, kama mlivyosikia ma masikio yenu.[#Tume. 6:13.]

12Yeremia akawaambia wakuu wote na watu wote wa ukoo huu, akasema: Bwana amenituma kuyafumbua hayo maneno yote yatakayoijia Nyumba hii na mji huu, mliyoyasikia.

13Sasa fanyeni mwenendo mwema na matendo mema mkiisikia sauti ya Bwana Mungu wenu! Ndipo, Bwana atakapogeuza moyo, asiwafanyizie hayo mabaya, aliyoyasema![#Yer. 7:3.]

14Lakini mimi nitazameni! Nimo mikononi mwenu; nifanyizieni, mliyoyaona na macho yenu kuwa mema yanyokayo!

15Lakini jueni hili kabisa: Ninyi mtakaponiua mtafanya, damu ya mtu asiyekosa iwajie ninyi na mji huu nao wakaao humu! Kwani Bwana amenituma kweli kwenu kuyasema maneno haya masikioni penu.*

16Ndipo, wakuu na watu wote wa ukoo huu walipowaambia watambikaji na wafumbuaji: Mtu huyu hapaswi na hukumu ya kuuawa, kwani amesema na sisi katika Jina la Bwana.

17Kulikuwa na wazee wa nchi hii, wakainuka, wakauambia mkutano wote wa watu wa ukoo huu, wakasema:

18Mika wa Moreseti alikuwa mfumbuaji siku za Hizikiya, mfalme wa Yuda, akawaambia watu wote wa Yuda kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Sioni utalimwa kuwa shamba, nao Yerusalemu utageuka kuwa machungu ya mavunjiko, nao mlima wa Nyumba ya Bwana utakuwa kilima chenye mwitu.[#Mika 3:12.]

19Je? Hizikiya, mfalme wa Yuda, nao Wayuda wote walimwua? Hakumcha Bwana na kuutuliza uso wake Bwana? Naye Bwana akageuza moyo, asiwafanyizie hayo mabaya, aliyowaambia. Na sisi tufanye kibaya kilicho kikuu kama hicho, tuzikoseshe roho zetu?[#Yer. 18:8.]

Mfumbuaji Uria anauawa.

20Kulikuwa na mtu mwingine aliyefumbua katika Jina la Bwana, ni Uria, mwana wa Semaya wa mji wa Kiriati-Yearimu. Naye akayafumbua yote yatakayoujia mji huu na nchi hii sawasawa kama Yeremia.

21Mfalme Yoyakimu na watu wake wote wa vita na wakuu wote walipoyasikia maneno yake, mfalme akatafuta, jinsi atakavyomwua. Uria alipoyasikia, akaogopa, akakimbia kwenda Misri.

22Mfalme Yoyakimu akatuma watu kwenda Misri; ni Elnatani, mwana wa Akibori, na watu wengine waliokwenda naye Misri.

23Wakamtoa Uria huko Misri, wakampeleka kwake mfalme Yoyakimu, akampiga kwa upanga, mzoga wake akautupa kwenye makaburi yao waliokuwa wa ukoo huu.

24Lakini Ahikamu, mwana wa Safani, alimshika Yeremia kwa mkono wake, asitiwe mikononi mwa watu wamwue.[#2 Fal. 22:12.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania