The chat will start when you send the first message.
1Ikawa mwaka uleule, ufalme wa Sedekia, mfalme wa Yuda, ulipoanzia, katika mwezi wa tano wa mwaka wa nne, ndipo, mfumbuaji Hanania, mwana wa Azuri wa Gibeoni, aliponiambia Nyumbani mwa Bwana machoni pao watambikaji napo pao wote wa ukoo huu kwamba:
2Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema kwamba: Nimeyavunja makongwa ya mfalme wa Babeli.
3Bado miaka miwili ndipo, mimi nitakapovirudisha mahali hapa vyombo vyote vya Nyumba ya Bwana, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, alivyovichukua mahali hapa na kuvipeleka Babeli.[#Yer. 27:16.]
4Naye Yekonia, mwana wa Yoyakimu, mfalme wa Yuda, nayo mateka yote ya Yuda waliokwenda Babeli mimi nitawarudisha mahali hapa, kwani nitayavunja makongwa ya mfalme wa Babeli; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yer. 27:20.]
5Mfumbuaji Yeremia akamwambia mfumbuaji Hanania machoni pao watambikaji napo pao watu wote wa ukoo huu waliosimama katika Nyumba ya Bwana,
6akasema mfumbuaji Yeremia: Amin, na yawe hivyo! Bwana na ayafanye hivyo akiyatimiza maneno yako, uliyoyafumbua, akivirudisha mahali hapa vyombo vya Nyumba ya Bwana nayo mateka yote toka Babeli!
7Lisikie tu neno hili, ninalolisema masikioni mwako, namo masikioni mwa watu wote wa ukoo huu:
8Wafumbuaji waliokuwa mbele yangu na mbele yako toka siku za kale walifumbulia nchi nyingi, hata nchi zenye wafalme wakuu vita na mabaya na magonjwa yauayo yatakayokuja.
9Lakini mfumbuaji anayefumbua mambo ya kutuliza roho atajulikana hapo, lile neno lake mfumbuaji litakapotimia, ya kuwa ni mfumbuaji, Bwana aliyemtuma kweli.
10Ndipo, mfumbuaji Hanania alipoiondoa miti ya kongwa shingoni pake Yeremia, akaivunja.[#Yer. 27:2.]
11Kisha Hanania akasema, watu wote wa ukoo huu wakimtazama, kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Hivi ndivyo, nitakavyoyavunja makongwa ya Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, shingoni pa mataifa yote, miaka miwili itakapopita. Kisha mfumbuaji Yeremia akashika njia kwenda zake.[#Yer. 28:3.]
12Neno la Bwana likamjia Yeremia, mfumbuaji Hanania alipokwisha kuivunja miti ya kongwa shingoni pake mfumbuaji Yeremia, likamwambia:
13Nenda kumwambia Hanania haya: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Miti ya kongwa, uliyoivunja, ni ya miti tu; lakini mahali pao umeweka miti ya kongwa iliyo ya chuma.
14Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Makongwa ya chuma nimetia shingoni pao haya mataifa yote, wamtumikie Nebukadinesari, mfalme wa Babeli; watamtumikia kweli, nao nyama wa porini nimempa.[#Yer. 27:6.]
15Basi, mfumbuaji Yeremia akamwambia mfumbuaji Hanania: Sikia, Hanania! Bwana hakukutuma, nawe umewaegemeza watu wa ukoo huu mambo ya uwongo.
16Hivi ndivyo, Bwana anavyosema kweli: Utaniona, nikikutuma kuondoka huku nchini, mwaka huu wewe utakufa, kwani umewakataza watu kumtii Bwana.[#Yer. 23:14; 29:32.]
17Mfumbuaji Hanania akafa mwaka uleule katika mwezi wa saba.