Yeremia 29

Yeremia 29

Barua ya Yeremia kwa Wayuda waliohamishwa kwenda Babeli.

1Haya ndiyo maneno ya barua ya mfumbuaji Yeremia, aliyoiandika Yerusalemu kwenda kwao wazee waliosalia kwao waliotekwa na kwa watambikaji na kwa wafumbuaji na kwa watu wote wa ukoo huu, Nebukadinesari aliowateka Yerusalemu na kuwapeleka Babeli.

2Mfalme Yekonia na mama yake walipokwisha kutoka Yerusalemu pamoja na wakuu wa nyumba ya mfalme na wakuu wa Yuda na wa Yerusalemu na mafundi wa seremala na wahunzi,[#2 Fal. 24:14-15.]

3ndipo, alipoitia mikononi mwao Elasa, mwana wa Safani, na Gemaria, mwana wa Hilkia; hawa ndio, Sedekia, mfalme wa Yuda, aliowatuma kwenda Babeli kwa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli. Akawaandikia:

4Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyowaambia mateka yote, niliowatoa Yerusalemu, wapelekwe Babeli:

5Jengeni nyumba, mkae! Limeni mashamba, mle mazao yao!

6Oeni wanawake, mzae watoto wa kiume na wa kike! Nao wana wenu wa kiume wapatieni wanawake, nao wana wenu wa kike mwaoze waume, wazae watoto wa kiume na wa kike, mwe wengi huko, msipunguke!

7Utafuteni utengemano wa ule mji, niliowahamishia ninyi! Uombeeni kwa Bwana! Kwani unapotengemana, nanyi mtapata kutengemana.

8Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Wasiwadanganye wafumbuaji walioko kwenu katikati wala waaguaji wenu! Wala msizisikie ndoto zenu, mnazoziota![#Yer. 14:14.]

9Kwani hao huwafumbulia maneno yenye uwongo katika Jina langu, sikuwatuma; ndivyo, asemavyo Bwana.

10Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwanza sharti miaka 70 ipite huko Babeli; ndipo, nitakapowatokea, niwatimizie lile neno langu jema la kwamba: Nitawarudisha mahali hapa.[#Yer. 25:11-13.]

11Kwani ndivyo, asemavyo Bwana: Mimi ninayajua mawazo, ninayowawazia, kuwa mawazo ya kuwaponya, siyo ya kuwaponza, nipate kuwapa huko nyuma myangojeayo.

12Mtakaponiita mkiendelea kunilalamikia, nitawasikia.[#5 Mose 4:29; Yes. 55:6.]

13Mtakaponitafuta, mtaniona; mtakaponitafuta kwa mioyo yote,

14nitawaonekea, nitawafungua mafungo yenu, niwakusanye na kuwatoa kwenye mataifa yote na mahali po pote, nilipowahamishia; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Sh. 126:4.]

15Kwani ninyi husema: Bwana ametuinulia wafumbuaji huku Babeli.

16Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema kwa ajili ya mfalme anayekaa katika kiti cha kifalme cha Dawidi na kwa ajili ya watu wote wa ukoo huu wanaokaa humu mjini walio ndugu zenu, wasiotoka pamoja nanyi kwenda kuhamishwa;

17hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Wataniona, nikituma kwao panga na njaa na magonjwa mabaya, nikiwageuza kuwa kuyu zitapishazo, zisizolika kwa ubaya wao.[#Yer. 24:8.]

18Nitawakimbiza kwa panga na kwa njaa na kwa magonjwa mabaya, nitawatoa, watupwe huko na huko katika nchi zote zenye wafalme huku ulimwenguni, waapizwe kwa kustukiwa, wazomelewe na kutukanwa kwenye mataifa yote, nitakakowatupa,[#Yer. 24:9-10.]

19kwa kuwa hawakuyasikia maneno yangu; ndivyo, asemavyo Bwana. Mimi nilituma kwao watumishi wangu walio wafumbuaji pasipo kuchoka kila kulipokucha, lakini hamkusikia; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yer. 25:4.]

20Lakini ninyi lisikieni Neno la Bwana, ninyi mateka yote, niliowatoa Yerusalemu na kuwatuma kwenda Babeli![#Yer. 29:4.]

21Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema kwa ajili ya Ahabu, mwana wa Kolaya, na kwa ajili ya Sedekia, mwana wa Masea, waliowafumbulia katika Jina langu mambo ya uwongo: Mtaniona, nikiwatia mkononi mwa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, awaue machoni penu.[#Yer. 29:8.]

22Nako kwao ndiko, mateka yote ya Wayuda walioko Babeli watakakochukua kiapo cha kwamba: Bwana na akufanyizie kama Ahabu na kama Sedekia, mfalme wa Babeli aliowachoma motoni!

23Kwa kuwa wamefanya yasiyofanywa kwao Waisiraeli, wakifanya ugoni na wanawake wa wenzao, wakasema neno la uwongo katika Jina langu, nami sikuwaagiza neno, Mimi ninayajua haya, ninayashuhudia.

Mapatilizo yatakayomjia Semaya.

24Kwa ajili ya Semaya wa Nehelamu utasema kwamba:

25Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema kwamba: Umetuma barua katika jina lako kwa watu wote wa ukoo huu waliomo Yerusalemu na kwa mtambikaji Sefania, mwana wa Masea, na kwa Yerusalemu na kwa watambikaji wote, za kwamba:[#Yer. 21:1; 2 Fal. 25:18.]

26Bwana amekuweka kuwa mtambikaji mahali pa mtambikaji Yoyada, mwe wasimamizi Nyumbani mwa Bwana kuwaangalia wote wenye wazimu nao wajiwaziao kuwa wafumbuaji, uwafunge mikatale na mapingu.[#Hos. 9:7.]

27Mbona sasa hukumkaripia Yeremia wa Anatoti anayewafumbulia ninyi?

28Kwa sababu hii ametuma kwetu Babeli barua ya kwamba: Siku ni nyingi bado, jengeni nyumba, mkae! Limeni mashamba, mle mazao yao!

29Mtambikaji Sefania alipoisoma barua hii masikioni pa mfumbuaji Yeremia,

30ndipo, neno la Bwana lilipomjia Yeremia kwamba:

31Tuma barua kwa mateka yote kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema kwa ajili ya Semaya wa Nehelamu: Kwa kuwa Semaya amewafumbulia ninyi, nami sikumtuma, akawaegemeza mambo ya uwongo,

32kwa hiyo Bwana anasema haya: Mtaniona, nikimpatiliza Semaya wa Nehelamu na kizazi chake: hatapata mtu wa mlango wake atakayekaa kwao wa ukoo huu, wala atakayeyaona yale mema, nitakayowafanyizia wao walio ukoo wangu, kwani amewakataza watu kumtii Bwana; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yer. 28:16.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania