The chat will start when you send the first message.
1Akasema: Kama mtu anampa mkewe ruhusa, ajiendee, naye akatoka kwake, akawa wa mume mwingine, je? Yule wa kwanza atamrudia? Nchi ile isingepata uchafu? Nawe wewe umezini na wenzio wengi, kisha unirudie mimi! ndivyo, asemavyo Bwana.[#5 Mose 24:1-4.]
2Yaelekeze macho yako vilimani, utazame! Pako mahali, usipofanyiziwa ugoni? Ulikaa njiani na kuwangoja kama Mwarabu nyikani, ukaichafua nchi kwa ugoni wako uliokuwa mbaya.
3Kwa hiyo ulinyimwa mvua za masika, hata za vuli hazikunya, lakini paji lako ni lilelile la mwanamke mgoni, ukakataa kuingiwa na soni.
4Tena unaniita sasa: Baba yangu! Wewe ulikuwa mwenzangu mpendwa wa siku za ujana!
5Je? Atakasirika siku zote, asiniondolee makosa kale na kale? ndivyo, unavyosema; kisha unayafanya mabaya, unayoyaweza.
6Bwana akaniambia siku za mfalme Yosia kwamba: Umeyaona, binti Isiraeli aliyoyafanya akiniacha? Alipanda kila kilima kirefu, akakaa chini ya kila mti wenye majani mengi kufanya ugoni palepale.[#Yer. 2:20.]
7Alipokwisha kuyafanya hayo yote, nimesema: Rudi kwangu! Lakini hakurudi, hata dada yake binti Yuda avunjaye maagano aliyaona.
8Nikauona huo ugoni wote, alioufanya binti Isiraeli akiniacha, nikampa ruhusa, ajiendee, nikampa nacho cheti cha kuachana. Lakini naye dada yake binti Yuda hakuogopa, akaenda, akafanya ugoni naye.[#2 Fal. 17:18-19; Ez. 23:2-11.]
9Ikawa, uvumi wa ugoni wake ukaichafua nchi, akazini akitumia mawe na miti.
10Alipoyafanya hayo yote, naye dada yake binti Yuda avunjaye maagano hakurudi kwangu kwa moyo wake wote, ila kwa uwongo tu; ndivyo, asemavyo Bwana.
11Bwana akaniambia: Binti Isiraeli akiniacha, roho yake ni njema kuliko yake binti Yuda avunjaye maagano.
12Nenda kuyatangaza maneno haya na kupaza sauti upande wa kaskazini, useme: Rudi, binti Isiraeli uliyeniacha! ndivyo, asemavyo Bwana: sitawatazama kwa macho makali, kwani ni mpole. Ndivyo, asemavyo Bwana; Sitakasirika kale na kale.[#Sh. 103:8-9.]
13Jua tu, ya kuwa umekora manza ulipomtengua Bwana Mungu wako ukienda huko na huko kufuata wageni chini ya kila mti wenye majani mengi, lakini sauti yangu hukuisikia; ndivyo, asemavyo Bwana.
14Rudini, ninyi wana mlioniacha! ndivyo, asemavyo Bwana. Kwani mimi ni bwana wenu; nitawachukua mmoja katika mji mmoja, tena wawili katika udugu mmoja, niwapeleke Sioni.[#Hos. 2:19; Yes. 6:13.]
15Nitawapa wachungaji waupendezao moyo wangu, wawachunge, mpate ujuzi wa kuerevuka.[#Yer. 23:4.]
16Ndivyo, asemavyo Bwana: Hapo, mtakapokuwa wengi kwa kuzaa wana katika nchi ile, siku zile hawatalitaja tena Sanduku la Agano la Bwana, halitaingia moyoni mwa mtu, hawatalikumbuka, hawatataka kuliona, wala hawatafanya jingine tena.
17Siku zile Yerusalemu watauita Kiti cha kifalme cha Bwana; kule Yerusalemu ndiko, wamizimu wote watakakokusanyikia kwa ajili ya Jina la Bwana, hawataendelea tena kuufuata ugumu wa mioyo yao mibaya.[#Yes. 2:2-4; 65:2.]
18Siku zile mlango wa Yuda utauendea mlango wa Isiraeli, nao watakuja pamoja wakitoka katika nchi ya upande wa kaskazini, waje kuikalia nchi, niliyowapa baba zenu, iwe fungu lao.[#Yes. 11:11-13.]
19Nami nalisema: A, nitakuweka kwenye wana, nitakupa nchi ya kupendezwa nayo kwa kuwa yenye utukufu kuyapita matukufu yote ya wamizimu! Nikasema: Utaniita: Baba! Usiondoke nyuma yangu![#Yer. 3:4.]
20Lakini kama mwanamke anavyomdanganya mwenziwe akimwacha, ndivyo, mlivyonidanganya na kuniacha, ninyi wa mlango wa Isiraeli; ndivyo, asemavyo Bwana.
21Sauti zinasikilika vilimani juu, ni kilio cha malalamiko ya wana wa Isiraeli, kwa kuwa wamezipotoa njia zao kwa kumsahau Bwana Mungu wao.
22Rudini, ninyi wana mlioniacha! Nitawaponya, ingawa mmeniacha. Tutazame! Tumekujia, kwani wewe ndiwe Bwana Mungu wetu.[#Hos. 6:1.]
23Kweli mambo ya vilimani juu ni ya uwongo tu, nayo michezo ya vileleni milimani; kweli kwake Bwana Mungu wetu ndiko, wokovu wa Isiraeli uliko.
24Jambo lenye soni limeyala mapato ya baba zetu tangu ujana wetu, kondoo na mbuzi wao na ng'ombe wao, hata wana wao wa kiume na wa kike.
25Sharti tulale kwa kupatwa na soni, nayo matusi yatufunike, kwani tumemkosea Bwana Mungu wetu, sisi na baba zetu tangu utoto wetu mpaka siku hii ya leo, hatukuisikia sauti ya Bwana Mungu wetu.