Yeremia 30

Yeremia 30

Wokovu wa Isiraeli na wa Yuda.

1Hili ndilo neno lililomjia Yeremia likitoka kwa Bwana kwamba:

2Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema kwamba: Yaandike hayo maneno yote, niliyokuambia katika kitabu!

3Kwani ndivyo, asemavyo Bwana: Tazama! Siku zitakuja, nitakapoyafungua mafungo yao walio ukoo wangu wa Isiraeli na wa Yuda, niwarudishe katika ile nchi, niliyowapa baba zao, nayo itakuwa yao tena; ndivyo, Bwana anavyosema.[#Yer. 29:14.]

4Haya ndiyo maneno, Bwana aliyoyasema kwa ajili ya Isiraeli na ya Yuda,

5kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Tumesikia sauti ya kustusha na kushangaza, hakuna penye utengemano.

6Ulizeni, mwone, kama yuko mwanamume atakayezaa! Mbona nimewaona waume wote wakitia mikono yao viunoni pao kama mwanamke anayetaka kuzaa? Mbona nyuso zote zimegeuka, zikachujuka?[#Yes. 13:8.]

7Kumbe siku hiyo ni kubwa, hakuna ifananayo nayo; ndipo, Yakobo anaposongeka, lakini napo atapatoka, aokoke.[#Yoe. 2:11; Sef. 1:15.]

8Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi: Itakuwa siku ile, nitakapoyavunja makongwa shingoni pako na kuyararua mafungo yako, wageni wasiwatumikishe tena.[#Yer. 27:12.]

9Ila watamtumikia Bwana Mungu wao na Dawidi, mfalme wao, nitakayemwinua kwao.[#Yer. 23:5; Ez. 34:23.]

10Ndivyo, asemavyo Bwana: Nawe, mtumishi wangu Yakobo, usiogope, wala usistuke, Isiraeli! Kwani utaniona, nikikuokoa na kukutoa katika nchi za mbali, nacho kizazi chako nitakitoa katika nchi, walikofungiwa. Yakobo atarudi, atatulia pasipo kusumbuliwa, kwani hakuna atakayemhangaisha.[#Yer. 46:27; Yes. 44:2.]

11Kwani mimi niko pamoja na wewe nikuokoe; ndivyo, asemavyo Bwana. Kwani nitayamaliza mataifa yote, ambayo nimekutawanya kwao, wewe peke yako sitakumaliza, nitakuchapa tu, kama yakupasavyo, nisikuache pasipo patilizo lo lote.[#Yer. 10:24.]

12Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kidonda chako hakiwezekani, pigo lako haliponi.[#Yer. 15:18.]

13Hakuna akupigiaye shauri, alitoe jipu lako usaha; hakuna dawa ya kubandika, ikuponye.

14Wote waliokupenda wamekusahau, hawakuulizi tena, kwani nimekupiga, kama ninavyopiga mchukivu, nimekuchapa pasipo huruma, kwa kuwa ulifanya maovu mengi, kweli makosa yako ni makali.

15Mbona unakililia kidonda chako, ya kuwa maumivu yako hayawezekani? Nimekufanyizia hayo, kwa kuwa ulifanya maovu mengi, nayo makosa yako ni makali.

16Kweli wote waliokula wewe wataliwa, nao wote waliokusonga watakwenda kufungwa; waliokunyang'anya nao watanyang'anywa, nao wote waliopokonya mali zako nitawatoa, wapokonywe nao mali zao.[#Yes. 33:1.]

17Kwani ndivyo, asemavyo Bwana: Nitakupatia uzima tena, hata vidonda vyako nitaviponya, kwa kuwa wewe Sioni wamekuita Mfukuzwa kwa kwamba: Hakuna anayemwuliza.[#Yes. 33:6.]

18Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtaniona, nikiyafungua mafungo ya mahema yake Yakobo, nikiyahurumia makao yake; nao mji utajengwa tena juu ya chungu zake, hata jumba kuu litakaa, kama yalipasavyo.[#Yer. 30:3.]

19Namo mwao zitatoka nyimbo za kushukuru na sauti zao wachekao; nami nitawapa kuwa wengi, wasiwe wachache, nitawapa utukufu, wasibezwe.

20Nao watoto wao watakuwa kama kale; nalo kundi lao la watu litapata nguvu usoni pangu, nao wote waliowakorofisha nitawapatiliza.

21Mkuu wao atakuwa mtu wa kwao; atakayewatawala atatoka katikati yao; nami nitamfikisha, anijie karibu, kwani yuko nani ajipaye moyo wa kunijia mwenyewe? ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yer. 30:9.]

22Nanyi mtakuwa ukoo wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.[#Yer. 24:7.]

23Mtakiona kimbunga cha Bwana, hata makaa yenye moto yakitoka kwake, nao upepo wa chamchela wenye nguvu utawaangukia vichwani wao wasiomcha Mungu.[#Yer. 23:19.]

24Ukali wake Bwana wenye moto hautatulia, mpaka uyafanye na kuyatimiza mawazo ya moyo wake; siku za mwisho mtayatambua haya.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania