The chat will start when you send the first message.
1Ndivyo, asemavyo Bwana: Siku zile nitaiwia milango yote ya Isiraeli Mungu wao, nao wataniwia ukoo wangu.[#Yer. 24:7; 31:33.]
2Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: ukoo wao waliosazwa na panga wameona upole nyikani, kwa kuwa watakwenda kwenye pumzikio la Bwana.
3Bwana amenionekea toka mbali akiniambia: Nimekupenda kwa upendo wa kale na kale, kwa hiyo nimekuvuta kwa kukuhurumia, uje kwangu.
4Nitakujenga; ndipo, utakapokuwa umejengwa, wewe mwanamwali wa Isiraeli! Utajipamba tena na kupiga patu, utatoka nao wachezao ngoma wakicheka.
5Utapanda tena mizabibu katika milima ya Samaria, nao wapanzi walioipanda wataichuma.
6Kwani iko siku, walinzi watakapoita mlimani kwa Efuraimu kwamba: Inukeni, tupande kwenda Sioni kwa Bwana Mungu wetu!
7Kwani, hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mpigieni Yakobo vigelegele vya furaha! Mwimbieni sana aliye kichwa chao mataifa! Pazeni sauti na kumshangilia! Semeni: Bwana, waokoe, walio ukoo wako, walio masao ya Waisiraeli!
8Mtaniona, nikiwaleta na kuwatoa katika nchi ya upande wa kaskazini, nikiwakusanya na kuwatoa mapeoni kwa nchi, nao vipofu na viwete, hata wenye mimba pamoja nao wazaao, watakuwa kundi kubwa, watakaporudi huku.[#Yes. 35:8-10.]
9Watakuja na kulia, nami nitawaongoza, wakinilalamikia; nitawapeleka kwenye vijito vya maji na kushika njia inyokayo, wasijikwae hapo, kwani nitakuwa baba yao Waisiraeli, nao Waefuraimu watakuwa kama mwanangu wa kwanza.[#2 Kor. 6:18.]
10Lisikieni Neno la Bwana, ninyi mataifa! Litangazeni kwenye visiwa vilivyoko mbali! Semeni: Aliyewatawanya Waisiraeli anawakusanya na kuwalinda, kama mchungaji anavyolilinda kundi lake.
11Kwani Bwana amewaokoa walio wa Yakobo, akawaokoa mikononi mwake aliyewashinda nguvu.
12Watakuja, wapige vigelegele mlimani kwa Sioni na kuyakimbilia mema ya Bwana, ngano na mvinyo na mafuta na wana wa kondoo na ndama; ndipo, roho zao zitakapokuwa kama shamba lenye maji, hawatazimia tena kwa njaa.[#Yes. 58:11.]
13Ndipo, wanawali watakapofurahia tena kucheza ngoma pamoja na vijana wa kiume na wazee pia, kwani ndipo, nitakapoyageuza masikitiko yao, yawe machangamko, nikiwatuliza mioyo na kuwafurahisha, wayaache majonzi yao.
14Hata roho zao watambikaji nitazipendeza na kuwapa manono, nao walio ukoo wangu watashiba mema; ndivyo, asemavyo Bwana.
15Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Sauti imesikiwa Rama, ni kilio na maombolezo yenye uchungu. Raheli anawalilia watoto wake, hakutaka kubembelezwa kwa ajili ya watoto wake, kwani hawako.[#Mat. 2:18.]
16Lakini hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Ukataze umio wako, usilie! Nayo macho yako yakataze, yasitoe machozi! Kwani mshahara wa matendo yako uko, hao watarudi wakitoka katika nchi ya adui; ndivyo, asemavyo Bwana.
17Tena kiko kingojeo kitakachotimia siku zilizoko mbele yako, kwani wanao watarudi kwenye mipaka yao; ndivyo, asemavyo Bwana.
18Nimemsikia Efuraimu, akipiga kilio kwamba: Umeniponda, nikapondeka kama ndama asiyefundishwa bado; nigeuze! ndipo, nitakapokuwa nimegeuka. Kwani wewe ndiwe Bwana Mungu wangu.
19Kwani nilipokuwa nimegeuka, nilijuta; nilipokuwa nimeonyeka, nilijipiga kiuno, nikaona soni na kuiva uso, kwani nilikuwa nimetwishwa matusi ya ujana wangu.
20Je? Efuraimu siye mwanangu mwenye kiasi kikuu? Siye mtoto wa kupendezwa naye? Ijapo nimemtisha, ninamkumbuka tena, nao moyo wangu unajihangaisha kwa ajili yake, mpaka nimhurumie; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yes. 49:15; Hos. 11:8.]
21Jisimamishie yaonyeshayo njia, kajiwekee vielekezo, nazo njia, ulizozipita ulipokwenda, zitie moyoni mwako! Rudini, mlio wanawali wa Isiraeli! Rudini katika hii miji yenu!
22Mnataka kutangatanga mpaka lini, ninyi wasichana wakatavu! Kwani Bwana ataumba jambo lililo jipya katika nchi: mwanamke atamkingia mumewe!
23Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Nitakapoyafungua mafungo yao, watu watalitumia tena neno hilo katika nchi ya Yuda namo mijini mwao la kwamba: Bwana na akubariki, uliye mbuga yenye wongofu, uliye mlima wenye utakatifu!
24Nao Wayuda watakaa huku katika miji yao yote iliyoko, walio wakulima nao watembeao na makundi.
25Kwani roho zilizozimia kwa kiu nitazirudisha na kuzinywesha, nazo roho zilizozimia kwa njaa nitazishibisha.[#Mat. 11:28.]
26Kisha nikaamka, nikaona, ya kuwa hivyo, nilivyolala usingizi, vimenipendeza sana.
27Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaona, siku zikija, nitakapoumwagia mlango wa Isiraeli na mlango wa Yuda mbegu za watu na mbegu za nyama.
28Itakuwa, kama nilivyokuwa macho na kuangalia, wang'olewe, wapondwe, wavunjwe, waangamizwe, wafanyiziwe mabaya, ndivyo, nitakavyokuwa macho na kuangalia, wajengwe, wapandwe; ndivyo, asemavyo Bwana.
29Siku zile hawatasema tena: Baba walipokula zabibu bichi, ndipo, wana walipokufa ganzi la meno.[#Omb. 5:7; Ez. 18:2.]
30Ila kila mtu atauawa na manza, alizozikora yeye; hata kila mtu atakayekula zabibu bichi atakufa mwenyewe ganzi la meno.
31*Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaona, siku zikija, nitakapofanya nao wa mlango wa Isiraeli nao wa mlango wa Yuda Agano Jipya.[#Ebr. 8:8-12.]
32Halitakuwa, kama Agano lile lilivyokuwa, nililolifanya na baba zao siku ile, nilipowashika mikono, niwatoe katika nchi ya Misri; lile Agano langu walilivunja, kama mimi si Bwana wao; ndivyo, asemavyo Bwana.
33Agano, nitakalolifanya nao wa mlango wa Isiraeli, siku hizi zitakapokuwa zimepita, ni hili: Nitawapa Maonyo yangu, yakae katika mawazo yao, tena nitayaandika mioyoni mwao, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yer. 31:1; Yes. 54:13; Rom. 11:27; Ebr. 10:16-17.]
34Hawatafundishana tena mtu na mwenziwe, wala mtu na ndugu yake kwamba: Mjueni Bwana! Kwani wote watanijua, hivyo walivyo wadogo, mpaka wakiwa wakubwa, kwani nitawaondolea manza zao, walizozikora, nisiyakumbuke tena makosa yao; ndivyo, asemavyo Bwana.*
35Hivi ndivyo, anavyosema Bwana aliyeliweka jua kuwa mwanga wa mchana hata miandamo ya mwezi pamoja na nyota kuwa mwanga wa usiku; ni yeye anayeichafua bahari, mawimbi yake yavume. Bwana Mwenye vikosi ni Jina lake;
36basi, ndivyo, asemavyo Bwana: Hapo, matengenezo hayo yatakapotoweka machoni pangu, ndipo, walio wa kizazi cha Isiraeli watakapokoma, wasiwe taifa la siku zote machoni pangu.[#Yer. 33:25; Rom. 11:1.]
37Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Hapo, mbingu zilizoko juu zitakapopimika, hapo, misingi ya nchi itakapochunguzika, ndipo, nitakapowatupa wote walio wa kizazi cha Isiraeli kwa ajili ya matendo yao yote; ndivyo, asemavyo Bwana.
38Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaona, siku zikija, mji huu utakapojengwa kuwa wa Bwana kuanzia kwenye mnara wa Hananeli kulifikisha lango la pembeni;[#Zak. 14:10.]
39toka hapo kamba ya kupimia itakwenda tena moja kwa moja mpaka kwenye kilima cha Garebu, hapo itazunguka kwenda Goa.
40Nalo bonde lote la mizoga na la majivu na mashamba yote mpaka kwenye mto wa Kidoroni na mpaka pembeni kwa Lango la Farasi lililoko upande wa maawioni kwa jua yatakuwa Patakatifu pa Bwana, hapatang'olewa tena, wala hapatavunjwa tena kale na kale.[#2 Mambo 29:16.]