The chat will start when you send the first message.
1Hili ndilo neno lililomjia Yeremia likitoka kwake Bwana katika mwaka wa 10 wa Sedekia, mfalme wa Yuda, ndio mwaka wa 18 wa Nebukadinesari.
2Ilikuwa hapo, vikosi vya mfalme wa Babeli vilipousonga Yerusalemu; naye mfumbuaji Yeremia alikuwa amefungwa uani penye kifungo kilichokuwa kwenye nyumba ya mfalme wa Yuda.[#2 Fal. 25:1-2.]
3Aliyemfunga ni Sedekia, mfalme wa Yuda, kwa kwamba: Mbona unafumbua kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtaniona, nikiutia mji huu mkononi mwa mfalme wa Babeli, auteke.[#Yer. 21:7; 27:6.]
4Naye Sedekia, mfalme wa Yuda, hatapona mikononi mwa Wakasidi, kwani atatiwa mkononi mwa mfalme wa Babeli, watasemeana kinywa kwa kinywa wakionana macho kwa macho.
5Atampeleka Sedekia Babeli; ndiko, atakakokuwa, mpaka nitakapomkagua; ndivyo, asemavyo Bwana: Mtakapopigana na Wakasidi hamtafanikiwa.[#Yer. 52:11.]
6Yeremia akasema: Neno la Bwana limenijia kwamba:
7Utamwona Hanameli, mwana wa mjomba wako Salumu, akija kwako kukuambia: Jinunulie shamba langu lililoko Anatoti! Kwani wewe unapaswa na kulikomboa, liwe lako.[#3 Mose 25:25; Ruti 4:3-4.]
8Kisha Hanameli, mwana wa mjomba wangu, akaja kwangu uani penye kifungo, kama Bwana alivyoniambia, akaniambia: Jinunulie shamba langu lililoko Anatoti katika nchi ya Benyamini, kwani inakupasa wewe kuwa nalo kwa kulikomboa. Nikatambua; ya kuwa hili ni lile neno la Bwana.
9Nikalinunua lile shamba kwake Hanameli, mwana wa mjomba wangu, lililoko Anatoti, nikamlipa fedha, nazo zilikuwa fedha kumi na saba.
10Nikaliandika katika cheti, nikatia muhuri, kikashuhudiwa na mashahidi, kisha nikampa fedha zake na kuzipima katika mizani.
11Nikakichukua kile cheti cha ununuzi chenye muhuri kilichoandikwa maagano na maongozi, tena kingine kilicho wazi.
12Hicho cheti cha ununuzi nikampa Baruku, mwana wa Neria, mwana wa Masea, machoni pake Hanameli, mwana wa mjomba wangu, napo machoni pao mashahidi walioyaandika majina yao katika cheti cha ununuzi napo machoni pao Wayuda wote waliokaa uani penye kifungo.
13Nikamwagiza Baruku machoni pao hivyo:
14Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Vichukue vyeti hivi, cheti cha ununuzi chenye muhuri nacho cheti hiki kilicho wazi, uvitie katika chombo cha udongo, vipate kukaa siku nyingi.
15Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Nyumba na mashamba na mizabibu itanunuliwa tena katika nchi hii.
16Nilipokuwa nimekwisha kumpa Baruku, mwana wa Neria, cheti cha ununuzi nikamwomba Bwana kwamba:
17E Bwana Mungu, tazama, wewe ulizifanya mbingu na nchi kwa uwezo wako mkubwa na kwa mkono wako ukunjukao, hakuna kisichowezekana kwako.[#Yer. 27:5; Luk. 1:37.]
18Watu maelfu huwahurumia, nazo manza, baba walizozikora, huzilipiza kwa wana wao waliotokea nyuma yao. U Mungu mkuu mwenye nguvu; Bwana Mwenye vikosi ni Jina lako.[#2 Mose 20:5-6.]
19Mashauri yako ni makuu, matendo yako ni mengi, macho yako hufumbuka, yazione njia zote za wana wa watu, umpe kila mtu yazipasayo njia zake nayo yayapasayo mapato ya matendo yake.[#Rom. 2:6.]
20Ulifanya vielekezo na vioja katika nchi ya Misri mpaka siku hii ya leo kwa Waisiraeli hata kwa watu wengine, ukajipatia Jina, kama linavyojulikana leo.
21Walio ukoo wako wa Isiraeli ukawatoa katika nchi ya Misri kwa kufanya vielekezo na vioja kwa kiganja chenye nguvu cha mkono ukunjukao, ukatisha kwa matisho makuu.
22Ukawapa nchi hii, uliyowaapia baba zao kuwapa, ni nchi ichuruzikayo asali na maziwa.
23Wakaja, wakaitwaa, kisha hawakuisikia sauti yako, wala hawakuyafuata Maonyo yako, wala hawakuyafanya yote, uliyowaagiza, wayafanye; kwa hiyo umewaletea haya mabaya yote.
24Tunayaona haya maboma, yako karibu, ni ya kuutekea mji huu; kweli mji huu utatiwa mikononi mwa Wakasidi wanaoupigia vita, maana panga na njaa na magonjwa mabaya yataushinda, yatimie uliyoyasema, nawe utakuwa ukiyatazama tu.
25Wewe Bwana Mungu, umeniambia: Jinunulie shamba kwa fedha, mashahidi wakiwako kuvishuhudia. Lakini mji huu utatiwa mikononi mwa Wakasidi.
26Neno la Bwana likamjia Yeremia kwamba:
27Tazama! Mimi ni Bwana, Mungu wao wote walio wenye miili. Je? Liko lo lote lisilowezekana kwangu?[#Yer. 32:17; 4 Mose 16:22.]
28Kwa hiyo Bwana anasema hivi: Mtaniona kweli, nikiutia mji huu mikononi mwao Wakasidi namo mkononi mwake Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, auteke.[#Yer. 32:3.]
29Kweli Wakasidi wanaoupigia mji huu vita watauingia, watauchoma moto mji huu na kuziteketeza nyumba, walimomvukizia Baali darini juu, nazo zile, walimomwagia miungu mingine vinywaji vya tambiko, kusudi wanikasirishe.[#Yer. 19:13.]
30Kwani wana wa Isiraeli nao wana wa Yuda tangu ujana wao huyafanya yale tu yaliyokuwa mabaya machoni pangu, kweli wana wa Isiraeli wamenikasirisha kwa matendo ya mikono yao; ndivyo, asemavyo Bwana.
31Kwani mji huu umenichafua na kuuwakisha moto wa makali yangu kuanzia siku ile, walipoujenga mpaka siku hii ya leo; kwa hiyo ninauondoa usoni pangu
32kwa ajili ya mabaya yote, wana wa Isiraeli na wana wa Yuda waliyoyafanya, kusudi wanikasirishe, wao wenyewe na wafalme wao na wakuu wao na watambikaji wao na wafumbuaji wao, walio watu wa Yuda nao wakaao Yerusalemu.
33Wakanigeuzia kosi zao, sizo nyuso; nami naliwafundisha pasipo kuchoka kila kulipokucha, lakini hawakuwako waliosikia, waonyeke.
34Wakayaweka matapisho yao katika ile Nyumba iliyoitwa kwa Jina langu, waitie uchafu.[#Yer. 7:30; 2 Fal. 21:4-5.]
35Wakamjengea Baali pa kumtambikia vilimani juu katika Bonde la Mwana wa Hinomu, wawatumie wana wao wa kiume na wa kike kuwa ng'ombe za tambiko za Moloki, nami sikuwaagiza hivyo, wala havikunijia moyoni, ya kuwa watafanya tapisho kama hilo, kusudi wawakoseshe Wayuda.[#Yer. 7:31; 19:5.]
36Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema sasa kwa ajili ya mji huu, ambao mnasema, ya kuwa umetiwa mkononi mwa mfalme wa Babeli kwa nguvu za panga na za njaa na za magonjwa mabaya:
37Mtaniona, nikiwakusanya na kuwatoa katika nchi zote, nilikowaendesha na kuwakimbiza kwa makali yangu yaliyowaka moto na kwa machafuko makuu, nitawarudisha mahali hapa na kuwapa kukaa salama.
38Nao watakuwa ukoo wangu, nami nitakuwa Mungu wao.[#Yer. 24:7; 30:22; 31:1,33.]
39Nami nitawapa kuwa wenye moyo mmoja washikao njia moja tu, waniogope siku zao zote; hivyo watajipatia mema wenyewe hata wana wao watakaokuwa nyuma yao.[#Ez. 36:27.]
40Nitafanya nao agano la kale na kale, ya kuwa sitaacha kuwafuata na kuwafanyizia mema, namo mioyoni mwao nitatia woga wa kuniogopa, wasiondoke tena kwangu.
41Nami nitawafurahia, niwafanyizie mema, kweli nitawapanda katika nchi hii kwa moyo wangu wote na kwa roho yangu yote.
42Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kama nilivyowaletea wao wa ukoo huu haya mabaya yote yaliyo makuu, ndivyo, nitakavyowaletea mema yote, niliyowaambia mimi.
43Mashamba yatanunuliwa tena katika nchi hii, mnayoisema ninyi, ya kuwa ni nyika tu pasipo watu na nyama kwa kutiwa mikononi mwa Wakasidi.
44Mashamba yatanunuliwa kwa fedha, hata vyeti vya ununuzi vitaandikwa na kutiwa muhuri na kushuhudiwa na mashahidi katika nchi ya Benyamini na pande zote za Yerusalemu, namo katika miji ya Yuda, namo katika miji iliyoko milimani, namo katika miji iliyoko mbugani, namo katika miji iliyoko upande wa kusini; kwani nitayafungua mafungo yao; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yer. 29:14; 30:3.]