Yeremia 34

Yeremia 34

Yatakayomjia Sedekia.

1Hili ndilo neno lililomjia Yeremia likitoka kwa Bwana, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, na vikosi vyake vyote na watu wa nchi zote za kifalme, mkono wake ulizozitawala, hayo makabila yote walipopiga vita, wauteke Yerusalemu na miji yake yote, likawa la kwamba:

2Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Nenda kumwambia Sedekia, mfalme wa Yuda, ukimwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Utaniona, nikiutia mji huu mkononi mwa mfalme wa Babeli, auteketeze kwa moto!

3Nawe hutaopoka mkononi mwake, kwani utakamatwa, utiwe mkononi mwake, nawe utaonana na mfalme wa Babeli macho kwa macho, atasema na wewe kinywa kwa kinywa, nawe utakwenda Babeli.[#Yer. 32:4.]

4Lisikie tu neno lake Bwana, wewe Sedekia, mfalme wa Yuda! Haya ndiyo, Bwana anayokuambia:[#Yer. 52:11.]

5Utakufa na kutulia; kama baba zako waliokuwa wafalme wa kwanza, waliokuwa mbele yako, walivyowashiwa mioto, ndivyo, watakavyokuwashia nawe mioto wakikuombolezea kwamba: E Bwana! Kwani hili ndilo neno, nililolisema mimi; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yer. 22:18; 2 Mambo 16:14.]

6Mfumbuaji Yeremia akamwambia Sedekia, mfalme wa Yuda, maneno haya yote mle Yerusalemu,

7vikosi vya mfalme wa Babeli walipoupigia Yerusalemu vita, wauteke pamoja na miji yote ya Yuda iliyosalia, ndiyo Lakisi na Azeka; kwani hiyo ndiyo iliyosalia katika miji ya Yuda iliyokuwa yenye maboma.[#2 Fal. 25:1.]

Mapatilizo yatakayowapata Wayuda.

8Hili ndilo neno lililomjia Yeremia likitoka kwa Bwana hapo, mfalme Sedekia alipokwisha kuagana na watu wote waliokuwamo Yerusalemu kuwatangazia watumwa ukombozi,[#Yer. 34:14.]

9kila mtu amwachilie mtumwa wake na kijakazi wake walio wa Kiebureo, akiwapa ruhusa, wajiendee tu, tena mtu asimtumikishe tena mwenziwe kazi za kutumwa katika nchi ya Yuda.

10Wakayasikia wakuu wote nao watu wote walioingia katika agano hilo la kwamba: Kila mtu ampe mtumwa wake na kijakazi wake ruhusa, wajiendee tu, asiwatumikishe tena kazi za kitumwa; nao walipoyasikia, wakawapa ruhusa, wajiendee tu.

11Lakini walipokwisha kufanya hivyo wakawarudia, wakawarudisha watumwa na vijakazi, waliowapa ruhusa, wajiendee tu, wakawashurutisha tena kuwa watumwa na vijakazi.

12Kwa hiyo neno la Bwana likamjia Yeremia likitoka kwa Bwana kwamba:

13Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Mimi nilifanya Agano na baba zenu siku ile, nilipowatoa katika nchi ya Misri nyumbani, mlimokuwa watumwa, kwamba:

14Mwisho wa miaka saba, kila mtu akiwa na ndugu yake wa Kiebureo aliyenunuliwa nawe, sharti umpe ruhusa, atoke kwako, ajiendee tu. Akutumikie miaka sita, kisha sharti umpe ruhusa, atoke kwako, ajiendee tu! Lakini baba zenu hawakunisikia, wala hawakuyatega masikio yao.[#2 Mose 21:2; 5 Mose 15:12.]

15Nanyi mmefanya leo tena yanyokayo machoni pangu, kila mtu akimtangazia mwenziwe ukombozi, mkaagana hivyo usoni pangu katika Nyumba hii inayoitwa kwa Jina langu.

16Lakini mkawarudia, mkalitia Jina langu uchafu mkiwarudisha kila mtu mtumwa wake na kijakazi wake, mliowapa ruhusa, wajiendee roho zao zilikotaka, mkawashurutisha kuwa tena watumwa na vijakazi wenu.

17Kweli hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Hamkunisikia mkimtangazia kila mtu ndugu yake na mwenzake ukombozi. Kwa hiyo ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaniona nikiwatangazia ukombozi na kuwaitia panga na magonjwa mabaya na njaa, nitawatoa ninyi, mtupwe huko na huko katika nchi zote zenye wafalme huku nchini.

18Nao waume waliolivunja agano wasipoyatimiza maneno ya hilo agano, walilolifanya usoni pangu, nitawatoa kuwa kama ndama ya tambiko, waliyoikata vipande viwili, kisha huipitia katikati.[#1 Mose 15:10,17.]

19Wakuu wa nchi ya Yuda nao wakuu wa Yerusalemu nao wakuu wa nyumba za mfalme nao watambikaji nao watu wote wa nchi hii waliovipitia vipande vya ndama ya tambiko katikati,

20hao wote nitawatia mikononi mwa adui zao namo mikononi mwao wanaozitafuta roho zao, nayo mizoga yao itakuwa chakula cha ndege wa angani na cha nyama wa porini.[#Yer. 7:33.]

21Naye Sedekia, mfalme wa Yuda, nao wakuu wake nitawatia mikononi mwao adui zao namo mikononi mwao wanaozitafuta roho zao namo mikononi mwa vikosi vya mfalme wa Babeli, vilivyotoka kwenu kwenda zao.

22Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaniona nikiwaagiza na kuwarudisha penye mji huu, waupigie vita, wauteke, wauteketeze kwa moto; nayo miji ya Yuda nitaitoa kuwa mapori tu, pasikae mtu.[#Yer. 37:8.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania