Yeremia 35

Yeremia 35

Kutii kwao Warekabu na kubisha kwao Wayuda.

1Hili ndilo neno lililomjia Yeremia likitoka kwa Bwana siku za Yoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, kwamba:[#1 Mambo 2:55.]

2Nenda nyumbani mwao Warekabu kusema nao, uwapeleke Nyumbani mwa Bwana katika ukumbi mmoja, uwape mvinyo, wanywe.

3Nikamchukua Yazania, mwana wa Yeremia, mwana wa Habasinia, pamoja na ndugu zake na wanawe wote nao wote walio wa mlango wa Warekabu.

4Nikawapeleka Nyumbani mwa Bwana katika ukumbi wa wana wa Hanani, mwana wa Igidalia, aliyekuwa mtu wa Mungu. Nao ukumbi huo ulikuwa kando ya ukumbi wa wakuu uliokuwa juu ya ukumbi wa Masea, mwana wa Salumu, aliyekuwa mlinda kizingiti.

5Kisha nikaweka mbele yao walio wa mlango wa Warekabu mitungi iliyojaa mvinyo na vikombe, nikawaambia: Nyweni mvinyo!

6Wakajibu: Hatunywi mvinyo, kwani Yonadabu, mwana wa baba yetu Rekabu, alituagiza kwamba: Msinywe mvinyo ninyi na wana wenu kale na kale![#2 Fal. 10:15,23.]

7Wala msijenge nyumba, wala msimwage mbegu, wala msipande mizabibu, wala msiwe nayo! Ila mkae mahemani siku zenu zote, mpate kuwapo siku nyingi huku nchini, mliko wageni ninyi.

8Tukaisikia sauti ya Yonadabu, mwana wa baba yetu Rekabu, katika mambo yote, aliyotuagiza, tusinywe mvinyo sisi wala wake zetu wala wana wetu wa kiume na wa kike:

9hatujengi nyumba za kukaa humo, wala mizabibu wala mashamba wala mbegu hatunazo.

10Tunakaa mahemani, kwani tumeyasikia, tukayafanya yote, kama baba yetu Yonadabu alivyotuagiza.

11Ikawa, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, alipopanda katika nchi hii, ndipo, tuliposema: Haya! Na tuje kwenda Yerusalemu na kuvikimbia vikosi vya Wakasidi na vya Washami! Basi, tukakaa Yerusalemu.

12Neno la Bwana likamjia Yeremia kwamba:

13Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Nenda kuwaambia watu wa Yuda nao wakaao Yerusalemu: Je? Hamtaki kuonyeka, myasikie maneno yangu? Ndivyo, asemavyo Bwana:

14Maneno yake Yonadabu, mwana wa Rekabu, aliyowaagiza wanawe, wasinywe mvinyo, yametimizwa nao: hawanywi mvinyo hata siku hii ya leo, kwani wamelisikia agizo la baba yao. Mimi nami nimesema nanyi pasipo kuchoka kila kulipokucha, lakini hamkunisikia.

15Nikatuma kwenu watumishi wangu wote walio wafumbuaji pasipo kuchoka kila kulipokucha kwamba: Rudini kila mtu katika njia yake mbaya na kufanya matendo mema! Msifuate miungu mingine kuitumikia! Ndipo, mtakaporudi katika nchi, niliyowapa baba zenu! Lakini hamkuyatega masikio yenu, wala hamkunisikia.[#Yer. 25:4-7.]

16Kweli, wana wa Yonadabu, mwana wa Rekabu, wamelitimiza agizo la baba yao, alilowaagiza; lakini wao wa ukoo huu hawanisikii.

17Kweli, hivi ndivyo, Bwana Mungu Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Mtaona, nikiwaletea Wayuda nao wakaao Yerusalemu yale mabaya yote, niliyoyasema ya kuwafanyizia, kwa kuwa niliposema nao, hawakunisikia, nilipowaita, hawakujibu.[#Yer. 7:13.]

18Nao walio wa mlango wa Rekabu Yeremia akawaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Kwa kuwa mmelisikia agizo la baba yenu Yonadabu, mkayashika maagizo yake yote, mkayafanya yote, kama alivyowaagiza,

19kwa hiyo ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Hatakoseka mtu wa Yonadabu, mwana wa Rekabu, atakayesimama usoni pangu siku zote.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania