The chat will start when you send the first message.
1Ikawa katika mwaka wa 4 wa Yoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, ndipo, neno hili lilipomjia Yeremia likitoka kwa Bwana kwamba:[#Yer. 25:1.]
2Jichukulie kitabu cha kuzingwa, uandike humo maneno yote niliyokuambia kwa ajili ya Isiraeli na ya Yuda na ya mataifa yote, anzia siku ile, niliposema na wewe, tangu siku za Yosia mpaka siku hii ya leo.
3Labda watasikia walio wa mlango wa Yuda wakiambiwa mabaya yote, mimi ninayoyawaza kuwafanyizia, kusudi warudi kila mtu katika njia yake mbaya, nikiwaondolea manza zao na makosa yao.[#Yer. 26:3.]
4Yeremia akamwita Baruku, mwana wa Neria; kisha Baruku akayaandika katika kitabu cha kuzingwa maneno yote ya Bwana, aliyomwambia, kama Yeremia alivyoyasema kwa kinywa chake.[#Yer. 32:12.]
5Yeremia akamwagiza Baruku kwamba: Mimi nimefungwa, siwezi kwenda Nyumbani mwa Bwana.
6Kwa hiyo nenda, ukisome hiki kitabu, ulichokiandika maneno ya Bwana, kama nilivyoyasema kwa kinywa changu, watu wayasikie Nyumbani mwa Bwana siku ya kufunga mfungo, hata Wayuda wote waliokuja wakitoka mijini mwao sharti wayasikie, yakisomwa.
7Labda malalamiko yao yatamwangukia Bwana usoni pake, wakirudi kila mtu katika njia zake mbaya, kwani makali yenye moto ni makuu, Bwana aliyoyasema kuwafanyizia watu wa ukoo huu.[#Yer. 36:3.]
8Baruku, mwana wa Neria, akayafanya yote, kama mfumbuaji Yeremia alivyomwagiza, akayasoma mle kitabuni maneno ya Bwana Nyumbani mwake Bwana.
9Ikawa katika mwaka wa 5 wa Yoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa tisa, ndipo, walipotangaza, watu wote wa Yerusalemu nao watu wote waliotoka katika miji ya Yuda kuja Yerusalemu wamfungie Bwana.
10Baruku akayasoma mle kitabuni maneno ya Yeremia Nyumbani mwa Bwana katika ukumbi wa Gemaria, mwana wa Safani, aliyekuwa mwandishi penye ua wa juu kwenye lango jipya la Nyumba ya Bwana, watu wote wa ukoo huu wakayasikia.
11Naye Mikaya, mwana wa Gemaria, mwana wa Safani, akayasikia maneno yote ya Bwana, yaliposomwa mle kitabuni.
12Akashuka kwenda nyumbani mwa mfalme katika ukumbi wa mwandishi, akawakuta humo wakuu wote, wakikaa, akina mwandishi Elisama na Delaya, mwana wa Semaya, na Elnatani, mwana wa Akibori, na Gemaria, mwana wa Safani, na Sedekia, mwana wa Hanania, nao wakuu wote.
13Basi, Mikaya akawasimulia hayo maneno yote, aliyoyasikia, Baruku aliyoyasoma mle kitabuni masikioni pao wa ukoo huu.
14Ndipo, wakuu wote walipomtuma Yudi, mwana wa Netania, mwana wa Selemia, mwana wa Kusi, kwenda kwake Baruku kumwambia: Kitabu cha kuzingwa, ulichokisoma masikioni pao wa ukoo huu, kichukue mkononi mwako, uje huku! Baruku, mwana wa Neria, akakichukua kile kitabu cha kuzingwa mkononi mwake, akaja kwao.
15Wakamwambia: Kaa, ukisome napo masikioni petu! Baruku akakisoma masikioni pao.
16Walipoyasikia haya maneno yote, ndipo, walipostukiana kila mtu na mwenziwe, wakamwambia Baruku: Sharti tumjulishe mfalme maneno haya yote!
17Wakamwambia Baruku kwamba: Tusimulie, jinsi ulivyoyaandika maneno haya yote, kinywa chake kilipoyasema!
18Baruku akawaambia: Kwa kinywa chake akanisomea maneno haya yote, nami nikayaandika humu kitabuni kwa wino.
19Kisha wakuu wakamwambia Baruku: Nenda kujificha wewe na Yeremia, mtu asijue, mliko ninyi!
20Nao wakaja kwa mfalme uani kwake, lakini kile kitabu cha kuzingwa walikuwa wamekiweka vizuri katika ukumbi wa mwandishi Elisama, wakayasimulia hayo maneno yote masikioni pa mfalme.
21Mfalme akamtuma Yudi kukichukua kile kitabu cha kuzingwa, akakichukua hicho kitabu katika ukumbi wa mwandishi Elisama, Yudi akakisoma masikioni pake mfalme napo masikioni pao wakuu wote waliosimama na kumzunguka mfalme.
22Naye mfalme akakaa katika nyumba ya kipupwe kwa kuwa mwezi wa tisa, nacho chano chenye makaa kikawaka moto mbele yake.
23Ikawa, Yudi alipokwisha kusoma vipindi vitatu au vinne, mfalme akavikata kwa kisu cha mwandishi, akavitupa motoni penye chano, mpaka alipokwisha kukitupa kitabu kile cha kuzingwa chote motoni penye chano.
24Hawakustuka wala hawakuzirarua nguo zao, wala mfalme wala watumishi wake wote walioyasikia maneno hayo yote.[#2 Fal. 22:11.]
25Napo hapo, Elnatani na Delaya na Gemaria walipomwomba mfalme sanasana, asikiteketeze hicho kitabu cha kuzingwa, hakuwasikia.
26Mfalme akamwagiza Yerameli, mwana wa mfalme, na Seraya, mwana wa Azirieli, na Selemia, mwana wa Abudeli, kumchukua mwandishi Baruku na mfumbuaji Yeremia, lakini Bwana aliwaficha.
27Neno la Bwana likamjia Yeremia, mfalme alipokwisha kukiteketeza kile kitabu cha kuzingwa na maneno yote, Baruku aliyoyaandika humo kwa kuambiwa na kinywa chake, likamwambia:[#Yer. 36:4.]
28Jichukulie tena kitabu cha kuzingwa, ukiandike maneno hayo yote ya kwanza yaliyokuwamo katika kitabu kile cha kuzingwa cha kwanza, Yoyakimu, mfalme wa Yuda, alichokiteketeza.
29Lakini kwa ajili ya Yoyakimu, mfalme wa Yuda, utasema: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Wewe umekiteketeza kitabu hicho cha kuzingwa kwamba: Mbona umeandika humo kwamba: Mfalme wa Babeli atakuja kweli kuiharibu nchi hii na kukomesha huku watu na nyama?[#Yer. 7:20; 9:10; 25:9-11.]
30Kwa hiyo Bwana anasema hivi kwa ajili ya Yoyakimu, mfalme wa Yuda: Hatampata atakayekaa katika kiti cha kifalme cha Dawidi, nao mzoga wake utakuwa umetupiwa jua kali la mchana nayo baridi ya usiku.[#Yer. 22:19.]
31Nitampatilizia yeye na kizazi chake na watumishi wake manza zao, walizozikora, nikiwaletea wao nao wakaao Yerusalemu nao watu wa Yuda mabaya yote, niliyoyasema, ya kuwa nitawafanyizia, lakini hawakusikia.
32Ndipo, Yeremia alipochukua kitabu kingine cha kuzingwa, akampa mwandishi Baruku, mwana wa Neria, akayaandika humo, Yeremia aliyoyasema kwa kinywa chake, ni maneno yote ya kile kitabu, Yoyakimu, mfalme wa Yuda, alichokiteketeza kwa moto, pakaongezwa tena maneno mengi kama hayo.