Yeremia 39

Yeremia 39

Yeremia aliyoyaona, Yerusalemu ulipotekwa.

(1-10: Yer. 52:4-16; 2 Fal. 25:1-12.)

1Yerusalemu ukatekwa hivyo: katika mwaka wa 9 wa Sedekia, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa 9 Nebukadinesari, mfalme wa Babeli alikuja Yerusalemu na vikosi vyake vyote, wakaanza kuusonga.

2Katika mwaka wa 11 wa Sedekia katika mwezi wa nne siku ya tisa boma la mji likabomolewa.

3Wakaingia wakuu wote wa mfalme wa Babeli, wakakaa penye lango la kati, ni Nergali-Sareseri na Samugari-Nebu na Sarsikimu, mkuu wa watumishi wa nyumbani mwa mfalme, na Nergali-Sareseri, mkuu wa waaguaji, nao wengine wote waliokuwa wakuu wa mfalme wa Babeli.

4Sedekia, mfalme wa Yuda, alipowaona yeye na wapiga vita wote, ndipo, walipokimbia, wakatoka mjini na usiku kwa njia ya bustani ya mfalme wakipita lango lililokuwa katikati ya zile kuta mbili za boma, wakaishika njia ya kwenda nyikani.

5Vikosi vya Wakasidi vikawafuata na kupiga mbio, wakamfikia Sedekia katika nyika ya Yeriko, wakamkamata, wakampeleka kwa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, mjini mwa Ribula katika nchi ya Hamati, yeye akasema naye na kumhukumu.

6Mfalme wa Babeli akawaua wana wa Sedekia machoni pake yeye huko Ribula, nao wakuu wote wa Yuda mfalme wa Babeli akawaua.

7Kisha akayapofua macho ya Sedekia, akamfunga kwa minyororo, ampeleke Babeli.

8Nyumba ya mfalme na nyumba za watu Wakasidi wakaziteketeza kwa moto, nazo kuta za boma la Yerusalemu wakazibomoa.

9Lakini masao ya watu wa ukoo huu, waliosalia mjini, ndio waliokuwa wamerudi upande wao na kuwaangukia nayo masao mengine ya watu waliosalia wakatekwa, Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, akawapeleka Babeli.

10Lakini waliokuwa wanyonge wa ukoo huu, wasiokuwa na kitu, Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, akawaacha katika nchi ya Yuda, akawapa mashamba ya mizabibu na mashamba mengine siku ile.

11Nebukadinesari mfalme wa Babeli, akamtia Yeremia mkononi mwa Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, akimwagiza kwamba:

12Mchukue, mwangalie kwa macho yako, usimfanyizie kibaya cho chote, ila mwenyewe atakavyokuambia, basi, ndivyo umfanyizie!

13Ndipo, Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, na Nebusazibani, mkuu wa watumishi wa nyumbani mwa mfalme, na Nergali-Sareseri, mkuu wa waaguaji, nao wakuu wote wa mfalme wa Babeli walipotuma,

14wakamchukua Yeremia wakimtoa uani penye kifungo, wakamwagiza Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Safani, amtoe kifungoni na kumpa ruhusa kwenda nyumbani, akakaa katikati ya watu.[#Yer. 38:28; 40:5-6.]

15Neno la Bwana lilimjia Yeremia, alipokuwa amefungwa uani penye kifungo, kwamba:

16Nenda kumwambia Ebedimeleki, yule Mnubi, kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Utaniona, nikiuletea mji huu niliyoyasema, yauwie, nayo ni mabaya, siyo mema, yatatimia usoni pako siku ile.[#Yer. 38:7.]

17Lakini ndivyo, asemavyo Bwana: Wewe nitakuponya siku hiyo, hutatiwa mikononi mwao watu wale, unaowaogopa.

18Kwani nitakuponya, usiuawe kwa upanga, nayo roho yako itakuwa pato lako, kwani umenitegemea; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Iy. 5:20.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania