Yeremia 4

Yeremia 4

Watakapojuta, Bwana atawapokea.

1Ndivyo, asemavyo Bwana: Kama utarudi, Isiraeli, rudi kwangu! Kama utayaondoa matapisho yako machoni pangu, hutafukuzwa.

2Ndipo, utakapoapa na kumtaja Bwana kwa kweli na kwa unyofu na kwa wongofu. Nao wamizimu watajiombea mema kwake pamoja na kumshangilia.[#Yer. 12:16; Yes. 65:16.]

3Kwani hivyo Bwana aliwaambia waume wa Yuda nao wakaao Yerusalemu: Jilimieni shamba jipya, msipande miibani![#Hos. 10:12.]

4Jitahirini, mwe wake Bwana, mkiyaondoa magovi ya mioyo yenu, ninyi waume wa Yuda nanyi mkaao Yerusalemu, kwamba: Makali yangu yasitokee yakiteketeza kama moto, watu wakishindwa kuzima, kwa ajili ya mabaya ya matendo yenu![#Yer. 9:26; 5 Mose 10:16.]

Vita vitaiangamiza nchi ya Yuda.

5Tangazeni katika nchi ya Yuda! Namo Yerusalemu watu na wasikie, mkisema! Pigeni baragumu katika nchi! Pazeni sauti kwa nguvu kabisa mkitangaza kwamba: Kusanyikeni, tuingie katika miji yenye maboma!

6Twekeni bendera, ielekee Sioni! Jihimizeni kukimbia, msisimame! Kwani mimi ninaleta mabaya kutoka upande wa kaskazini, hata mavunjiko mengi.[#Yer. 1:14.]

7Simba ametoka mwituni kwake kupanda kwetu, mwenye kuangamiza mataifa ameondoka, akatoka mahali pake, aigeuze nchi yako kuwa mapori, miji yako iwe mabomoko tu.

8Kwa hiyo jifungeni magunia! Ombolezeni na kulia! Kwani moto wa makali yake Bwana hautaondoka kwetu.

9Ndivyo, asemavyo Bwana: Itakuwa, siku ile moyo wa mfalme utapotea pamoja na mioyo ya wakuu wake, nao watambikaji watastuka, hata wafumbuaji watapigwa na bumbuazi.

10Nikasema: E Bwana Mungu! Kweli umewapoteza watu wa ukoo huu nao Wayerusalemu ulipowaambia: Mtakaa na kutengemana! Kumbe sasa upanga umewafikia rohoni![#Yer. 6:14.]

11Siku zile watu wa ukoo huu nao Wayerusalemu wataambiwa: Upepo uchomao moto umetoka vilimani nyikani, ukaja kuwavumia wazaliwa wa ukoo wangu, sio wa kupunga wala wa kupepeta.

12Ni upepo mkali zaidi, hauiwezi kazi hiyo, ukanijia; sasa mimi nitasema nao yawapasayo, yawapate.

13Tazameni, anapanda kama mawingu, magari yake ni kama kimbunga, farasi wake wanakwenda mbiombio kuliko tai. A, tumekwisha kupatwa, tunaangamia.

14Ifueni mioyo yenu, Wayerusalemu, ubaya uitoke, mpate kuokolewa! Mawazo yako maovu yatakaa mpaka lini ndani yako?[#Yes. 1:16.]

15Kwani inasikilika sauti ya mtangazaji atokaye nchi ya Dani, tena mwingine anapiga mbiu ya maovu atokaye milimani kwa Efuraimu kwamba:

16Yakumbusheni mataifa, yaipige mbiu hii kuifikisha Yerusalemu kwamba: Wenye kuvizia wanakuja, wanatoka nchi ya mbali, waipigie miji ya Yuda makelele yao ya vita.

17Wanajisimamisha kama walinzi wa shamba wakiuzunguka mji, kwani umenibishia; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yer. 1:15; 6:3.]

18Mwenendo wako na matendo yako yamekupatia haya; ubaya wako ndio unaokuletea huu uchungu, unakuchoma rohoni mwako.

Masikitiko ya mfumbuaji.

19Tumboni mwangu, tumboni mwangu ndimo, ninamoona machungu, hata mwenye maganda ya moyo wangu, maana moyo wangu umenichafuka sana, siwezi kunyamaza, kwani nimesikia sauti ya baragumu rohoni mwangu na makelele ya mapigano.[#Yes. 16:9.]

20Inatangazwa, jinsi mavunjiko yanavyofuata mavunjiko mengine, nchi yote nzima imeharibika, mara navyo vituo vyangu vimeharibiwa pamoja na mahema yangu kwa kitambo kimoja tu.

21Mpaka lini nitaiona bendera? Mpaka lini nitaisikia sauti ya baragumu?

22Kwani walio ukoo wangu ni wapumbavu; mimi hawakunijua kwa kuwa watoto wenye ujinga wasiotambua kitu; kweli ndio wajuzi wa kufanya mabaya, lakini kufanya mema hawajui kabisa.

23Nilipoitazama nchi, nikaiona kuwa peke yake tu pasipo kitu cho chote; nikazitazama mbingu nazo, lakini nako hakuna mwanga.

24Nikaitazama milima nayo, nikaiona, inavyotukutika, hata vilima vyote vikatikisika.

25Nikatazama, nikaona ya kuwa hakuna mtu, hata ndege wote wa angani walikuwa wamekimbia.

26Nikatazama, nikaona, ya kuwa mashamba yenye matunda ni nyika, nayo miji yao yote ilikuwa imebomolewa, Bwana asiione tena kwa kuwa na makali yenye moto.

27Kwani Bwana alisema hivyo: Nchi yote nzima itakuwa jangwa, lakini sitaimaliza kabisa.[#Yer. 5:10,18.]

28Kwa sababu hii nchi inaomboleza, nazo mbingu huko juu zinajivika weusi; kwa sababu nimeyasema niliyoyawaza moyoni, sitajuta, wala sitarudi na kuyaacha.

29Kwa makelele yao wapanda farasi na wenye kuvuta pindi watu wote waliomo mijini wamekimbia, wakaingia machakani, wakapanda magengeni, miji yote ikaachwa, hakuna mtu anayekaa humo.

30Nawe ukiharibiwa hivyo utafanyaje? Ijapo uvae nguo nyekundu za kifalme, ujipambe mapambo ya dhahabu, hata utie wanja machoni pako, huo uzuri wako utakuwa wa bure, wapenzi wako watakubeza, tamaa zao ni kukuua tu.

31Nimesikia sauti kama ya mwanamke mwenye kuzaa aonaye uchungu zaidi kwa kuzaa mara ya kwanza, ni sauti ya binti Sioni, akipiga kite na kuikunjua mikono yake kwamba: A, yamenipata! Roho yangu inazimia mbele yao wauao.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania