The chat will start when you send the first message.
1Ikawa katika mwezi wa saba, ndipo, Isimaeli, mwana wa Netania, mwana wa Elisama wa kizazi cha kifalme, aliyekuwa mkuu wa mfalme, alipokuja Misipa pamoja na watu kumi kwa Gedalia, mwana wa Ahikamu, wakala chakula pamoja naye huko Misipa.[#Yer. 40:8; 2 Fal. 25:25.]
2Ndipo, Isimaeli, mwana wa Netania, alipoinuka na wale watu kumi waliokuwa naye, wakampiga Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Safani, kwa panga, mpaka wakamwua; naye ndiye, mfalme wa Babeli aliyemweka kuisimamia nchi hiyo.[#Yer. 40:5.]
3Nao Wayuda wote waliokuwa Misipa pamoja na Gedalia, nao Wakasidi waliopatikana kule, nao wapiga vita Isimaeli akawaua.
4Ikawa, hata siku ya pili ya kumwua Gedalia mtu hakuvijua.
5Wakaja watu waliotoka Sikemu na Silo na Samaria, nao walikuwa watu 80 waliojinyoa ndevu na kuvaa nguo zilizoraruliwa, tena walikuwa wamejikatakata chale, namo mikononi mwao walichukua vipaji vya tambiko na uvumba kuvipeleka Nyumbani mwa Bwana.[#3 Mose 19:28.]
6Isimaeli, mwana wa Netania akatoka Misipa, akawaendea, akienda akilia machozi; alipowafikia akawaambia: Njoni kwa Gedalia, mwana wa Ahikamu!
7Ikawa, walipofika mjini kati, ndipo, Isimaeli, mwana wa Netania, alipowaua, akawatumbukiza kisimani, yeye na watu waliokuwa naye.
8Kwao wale kukaonekana watu kumi, wakamwambia Isimaeli: Usituue! Kwani tuko na vilimbiko, tulivyovificha porini, vya ngano na vya mawele na vya mafuta na vya asali; ndipo, alipowaacha, asiwaue pamoja na ndugu zao.
9Hicho kisima, Isimaeli alimoitumbukizia mizoga yao yote, aliowaua, walipokuja kwa Gedalia, ni kile, mfalme Asa alichokifanya kwa ajili ya kupigana na Basa, mfalme wa Isiraeli; hicho ndicho, Isimaeli, mwana wa Netania, alichokijaza mizoga yao, aliowaua.[#1 Fal. 15:16,22.]
10Kisha Isimaeli akawateka watu wote wa ukoo huu waliosalia Misipa: wana wa kike wa mfalme nao wote pia walioachwa Misipa, Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, aliompa Gedalia, mwana wa Ahikamu, awaangalie. Basi, Isimaeli, mwana wa Netania, akawateka, akashika njia kwenda kujitia kwa wana wa Amoni.
11Yohana, mwana wa Karea, nao wakuu wote wa vikosi waliokuwa naye walipoyasikia hayo mabaya yote Isimaeli, mwana wa Netania, aliyoyafanya,[#Yer. 40:8,13-16.]
12wakawachukua watu wote, wakaenda kupigana na Isimaeli, mwana wa Netania, wakamwona penye maji mengi karibu ya Gibeoni.[#2 Sam. 2:13.]
13Ikawa, watu wote wa ukoo huu waliokuwa na Isimaeli walipomwona Yohana, mwana wa Karea, nao wakuu wote wa vikosi waliokuwa naye, wakafurahi.
14Ndipo, watu wote wa ukoo huu, Isimaeli aliowateka Misipa, wakageuka nyuma, wakarudi kwenda kwa Yohana, mwana wa Karea.
15Isimaeli, mwana wa Netania, akamkimbia Yohana pamoja na watu wanane, akaenda kwa wana wa Amoni.
16Yohana, mwana wa Karea, na wakuu wote wa vikosi waliokuwa naye wakawachukua watu wote wa ukoo huu waliosalia, wakawarudisha na kuwatoa kwa Isimaeli, mwana wa Netania, aliowateka Misipa, alipokwisha kumwua Gedalia, mwana wa Ahikamu, nao walikuwa waume wapigao vita na wanawake na watoto na watumishi wa mfalme wa nyumbani, basi, wakawarudisha toka Gibeoni.
17Wakaondoka, wakakaa penye fikio la Kimuhamu lililoko kando ya Beti-Lehemu, wakataka kwenda Misri,[#Yer. 43:7; 2 Sam. 19:37.]
18kwa kuwakimbia Wakasidi, kwani waliwaogopa, kwa kuwa Isimaeli, mwana wa Netania, alimwua Gedalia, mwana wa Ahikamu, mfalme wa Babeli aliyemweka kuisimamia nchi hiyo.