The chat will start when you send the first message.
1Ikawa, Yeremia alipokwisha kuwaambia watu wote wa ukoo huu maneno yote ya Bwana Mungu wao, ndiyo maneno yale yote, yeye Bwana Mungu wao aliyomtuma kuwaambia,
2ndipo, Azaria, mwana wa Hosaya, na Yohana, mwana wa Karea, na watu wote waliojivuna walipomwambia Yeremia: Wewe umesema uwongo, Bwana Mungu wetu hakukutuma kutuambia: Msiende Misri kukaa ugenini huko!
3Kwani Baruku, mwana wa Neria, anakushurutisha, utupingie, apate kututia mikononi mwa Wakasidi, watuue, wengine watuteke na kutupeleka Babeli.
4Basi, Yohana, mwana wa Karea, nao wakuu wote wa vikosi nao watu wote wa ukoo huu hawakuisikia sauti ya Bwana, wakae katika nchi ya Yuda.
5Yohana, mwana wa Karea, na wakuu wote wa vikosi wakayachukua masao yote ya Wayuda waliorudi kukaa katika nchi ya Yuda wakitoka kwa mataifa yote, walikotupiwa.
6Wakawachukua waume na wake na watoto na wana wa kike wa mfalme nao wote pia, Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, aliowaacha na Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Safani, hata mfumbuaji Yeremia na Baruku, mwana wa Neria.
7Wakaja katika nchi ya Misri, kwani hawakuisikia sauti ya Bwana, wakakaa Tahapanesi.[#2 Fal. 25:26.]
8Neno la Bwana likamjia Yeremia huko Tahapanesi kwamba:
9Chukua kwa mkono wako mawe makubwa, uyafukie katika udongo penye tanuru lililoko pa kuiingilia nyumba ya Farao huku Tahapanesi, watu wa Yuda wakitazama!
10Kisha uwaambie: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Mtaniona, ninavyomtuma na kumchukua mtumishi wangu Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, nikiweka kiti chake cha kifalme juu ya mawe haya, niliyoyafukia, naye ataliwamba hema lake lenye utukufu juu yao.[#Yer. 25:9.]
11Atakuja kuipiga nchi hii ya Misri, nao walio wa kufa watakufa, nao walio wa kutekwa watatekwa, nao walio wa upanga watapigwa na upanga.[#Yer. 15:2.]
12Namo katika nyumba za miungu ya Misri nitatia moto, naye ataziteketeza, nayo miungu ataiteka; atajivika nchi ya Misri, kama mchungaj anavyojivika nguo yake, kisha atatoka huku na kutengemana.[#Yer. 46:25.]
13Lakini nguzo za nyumba ya kulitambikia jua iliyoko katika nchi ya Misri atazivunja, nazo nyumba za miungu ya Misri ataziteketeza kwa moto.