Yeremia 44

Yeremia 44

Wayuda wanaonywa kwa ajili ya kutumikia miungu mingine.

1Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kuwaambia Wayuda wote waliokaa katika nchi ya Misri, ndio waliokaa Migidoli na Tahapanesi na Nofu na katika nchi ya Patirosi, la kwamba:[#Yer. 43:7.]

2Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Ninyi mmeyaona hayo mabaya yote, niliyouletea Yerusalemu nayo miji yote ya Yuda, mkaiona, ya kuwa leo ni mavunjiko tu, hamna akaaye humo

3kwa ajili ya mabaya yao, waliyoyafanya ya kunikasirisha, walipokwenda kuvukizia na kutumikia miungu mingine, wasiyoijua wenyewe, wala ninyi wala baba zenu.

4Nami nilituma kwenu watumishi wangu wote waliokuwa wafumbuaji pasipo kuchoka kila kulipokucha kuwaambia: Msilifanye neno hilo la kutapisha, ninalochukizwa nalo!

5Lakini hawakusikia, wala hawakuyatega masikio yao, warudi na kuyaacha mabaya yao, wasivukizie miungu mingine.

6Ndipo, makali yangu yenye moto yalipomwagika, moto ukawaka katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu, hiyo miji ikawa mavunjiko na mahame, kama inavyojulikana leo.

7Sasa hivi ndivyo, Bwana Mungu Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Mbona mnazifanyizia roho zenu mabaya makuu, mwang'oe kwenu waume na wake, vijana na wachanga, watoweke katikati ya Wayuda, kwenu lisisalie hata sao?

8Mbona mnanikasirisha kwa matendo ya mikono yenu, mkivukizia miungu mingine huku katika nchi ya Misri, mlikokuja kukaa ugenini tu? Mbona mnataka kujing'oa wenyewe, kusudi mwe wa kuapizwa na wa kutukanwa na mataifa yote ya huku nchini?

9Je? Mmeyasahau mabaya ya baba zenu na mabaya ya wafalme wa Yuda na mabaya ya wake zao na mabaya yenu na mabaya ya wake zenu, waliyoyafanya katika nchi ya Yuda namo barabarani mwa Yerusalemu?

10Mpaka siku hii ya leo hawajanyenyekea, wala hawakuogopa, kwani hawaendelei kwa Maonyo wala kwa maongozi yangu, niliyowapa ninyi na baba zenu, yawe machoni penu.

11Kweli hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Mtaniona, nikiwaelekezea uso wangu, niwafanyizie mabaya na kuwang'oa Wayuda wote pia.

12Nitawachukua masao ya Wayuda waliozielekeza nyuso zao kuja katika nchi ya Misri kukaa ugenini huku. Watamalizika wote katika nchi ya Misri, wakiuawa kwa panga na kwa njaa; kwa hiyo watamalizika wadogo kwa wakubwa wakifa kwa panga na kwa njaa; nao wataapizwa kwa kustukiwa, watazomelewa na kutukanwa,[#Yer. 29:17-18.]

13nikiwapatiliza wakaao katika nchi ya Misri, kama nilivyowapatiliza Wayerusalemu kwa panga na kwa njaa na kwa magonjwa mabaya.

14Hawatapata pa kuponea wala pa kukimbilia wale walio masao ya Wayuda waliokuja katika nchi ya Misri kukaa ugenini huku, wapate kurudi halafu katika nchi ya Yuda, roho zao zinayoitunukia, warudi huko na kukaa; kwani hawatarudi, isipokuwa watoro tu.

15Wakamjibu Yeremia waume wote waliojua, ya kuwa wake zao huvukizia miungu mingine, nao wake wote waliosimama hapo mkutano mkubwa, nao wote wa ukoo huu waliokaa Patirosi katika nchi ya Misri, wakasema:[#Yes. 11:11.]

16Neno hili, ulilotuambia katika Jina la Bwana, kwetu sisi hakuna atakayekusikia.

17Kwani tutayafanya kabisa maneno yote yaliyotoka vinywani mwetu, tumvukizie mfalme wa kike wa mbinguni na kummwagia vinywaji vya tambiko, kama tulivyofanya sisi na baba zetu na wafalme wetu na wakuu wetu katika miji ya Yuda namo barabarani mwa Yerusalemu, tukashiba vyakula, tukafanikiwa, lakini mabaya hatukuyaona.[#Yer. 7:17-18; Hos. 2:5.]

18Toka hapo, tulipoacha kumvukizia mfalme wa kike wa mbinguni na kummwagia vinywaji vya tambiko, ndipo, tulipokosa yote, tukamalizika kwa panga na kwa njaa.

19Tena tukimvukizia mfalme wa kike wa mbinguni na kummwagia vinywaji vya tambiko, je? Waume wetu hawako, tukimtengenezea mikate yenye mifano yake na kummwagia vinywaji vya tambiko?

20Yeremia akawaambia watu wote wa ukoo huu, waume kwa wake na watu wote pia waliomjibu neno hilo, akasema:

21Kweli mmevukiza mavukizo katika miji ya Yuda namo barabarani mwa Yerusalemu ninyi na baba zenu, wafalme wenu na wakuu wenu nao watu wote waliokuwako katika nchi. Lakini hayo ndiyo, Bwana aliyoyakumbuka, akayaweka moyoni mwake.

22Kwa hiyo Bwana hakuweza kuvumilia tena kwa ajili ya ubaya wa matendo yenu na kwa ajili ya matapisho, mliyoyafanya; ndipo, nchi ilipogeuka kuwa mavunjiko na mapori tu, ikaapizwa, pasiwepo aikaaye, kama ilivyo siku hizi.

23Kwa kuwa mmevukiza na kumkosea Bwana, mkakataa kuisikia sauti yake na kuendelea kwa Maonyo yake na kwa maongozi yake na kwa mashuhuda yake, kwa sababu hii yamewafikia haya mabaya, mnayoyaona siku hizi.

24Yeremia akawaambia waume wote wa ukoo huu nao wake wote: Lisikieni neno la Bwana, ninyi Wayuda wote mlioko katika nchi ya Misri!

25Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema kwamba: Ninyi na wake zenu mliyoyasema kwa vinywa vyenu, myamalize kwa mikono yenu, yale ya kwamba: Tutayafanya kabisa maagano yetu, tuliyoyaapiana ya kumvukizia mfalme wa kike wa mbinguni na kummwagia vinywaji vya tambiko, basi, vitimizeni viapo vyenu! Vifanyizeni kabisa hivyo viapo vyenu![#Yer. 44:17.]

26Lakini lisikieni neno la Bwana, ninyi Wayuda wote mkaao katika nchi ya Misri! Bwana anasema: Tazameni, nimeapa katika Jina langu kubwa kwamba: Jina langu lisitajwe tena katika nchi yote ya Misri vinywani mwa watu wa Kiyuda wo wote wakisema: Hivyo, Bwana Mungu alivyo Mwenye uzima!

27Mtaniona, nikiwa macho kuyaangalia mabaya, nitakayowafanyizia, siyo mema! Ndipo, watakapomalizika watu wote wa Kiyuda walioko katika nchi ya Misri kwa panga na kwa njaa, mpaka watakapokuwa wamekwisha.

28Nao watakaopona panga watatoka katika nchi ya Misri, warudi katika nchi ya Yuda, lakini watakuwa wachache sana, mkiwahesabu. Ndipo, masao yote ya Yuda waliokuja Misri kukaa ugenini huku watakapojua, kama ni neno lipi litakalosimama, langu au lao.[#Yes. 11:11.]

29Ndivyo, asemavyo Bwana: Hiki kitakuwa kielekezo chenu cha kwamba: Mimi nitawapatiliza mahali hapa, kusudi mjue, ya kuwa maneno yangu hutimilika kweli na kuwapatia mabaya.

30Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtaniona, nikimtia Farao Hofura, mfalme wa Misri, mikononi mwa adui zake namo mikononi mwao wanaoitafuta roho yake, kama nilivyomtia Sedekia, mfalme wa Yuda, mkononi mwa adui yake Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, aliyeitafuta roho yake.[#2 Mambo 36:13-20.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania