Yeremia 46

Yeremia 46

Mapatilizo ya nchi ya Misri.

1Hili ndilo neno la Bwana lililomjia mfumbuaji Yeremia kwa ajili ya wamizimu.

2Yatakayowapata Wamisri. Kwa ajili ya vikosi vya Farao Neko, mfalme wa Misri, vilivyokuwa Karkemisi penye mto wa Furati, vilipopigwa na Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, katika mwaka wa nne wa Yoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, anasema:[#2 Mambo 35:20; Yes. 19; Ez. 29—30.]

3Tengenezeni ngao ndogo na kubwa, mwende vitani!

4Watandikeni farasi, wapandeni, ninyi wapanda farasi! Jipangeni, wenye kofia za chuma vichwani! Inoeni mikuki, kisha zivaeni shati za chuma!

5Mbona ninawaona hawa, wakirudi nyuma kwa kustuka? Mbona wanguvu wao wamepondeka, wakakimbia sana pasipo kugeuka? Matisho po pote! ndivyo, asemavyo Bwana.

6Lakini naye mwenye miguu miepesi hatakimbia, wala mwenye nguvu hatapona. Upande wa kaskazini kando ya mto wa Furati wamejikwaa, wakaanguka.

7Alikuwa nani aliyepanda kama mto wa Nili, maji yake yakajirusha kama ya mito mikubwa?

8Mmisri alipanda kama mto wa Nili, maji yakajirusha kama ya mito mikubwa, akasema: Nitapanda kuifunikiza nchi, niangamize mji nao wakaao humo!

9Pandeni, ninyi farasi! Pigeni mbio kama wenye wazimu, ninyi magari! Wapiga vita na watokee, wale Wanubi na Waputi washikao ngao na Waludi washikao pindi, wajuao kuzivuta!

10Siku hii ni yake Bwana Mungu Mwenye vikosi, ni siku ya lipizi ya kuwalipiza wapingani wake, panga zitakula, zishibe, mpaka zilewe kwa damu zao, kwani wao ndio kama ng'ombe za kumtambikia Bwana Mungu Mwenye vikosi katika nchi ya upande wa kaskazini kwenye mto wa Furati.[#5 Mose 32:42; Yes. 34:5.]

11Pandeni Gileadi kuchukua mafuta ya kwaju, ninyi wanawali mliozaliwa Misri! Ni bure, ukitumia dawa nyingi, hakuna itakayokuponya.[#Yer. 8:22.]

12Mataifa yameyasikia yakutiayo soni, vilio vyako vimeijaza nchi. Kwani mpiga vita amejikwaa kwa mpiga vita mwenziwe, wakaanguka wote wawili pamoja.

13Hili ndilo neno, Bwana alilomwambia mfumbuaji Yeremia, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, alipokuja kuipiga nchi ya Misri:

14Pigeni mbiu huko Misri na kuitangaza Migidoli! Tena itangazeni Nofu na Tahapanesi kwamba: Jipangeni na kujitengeneza! Kwani panga zimewala waliokuzunguka.

15Mbona watukufu wako wamelazwa chini? Hawakusimama, kwani Bwana aliwakumba;

16akakwaza wengi, wakaangukiana mtu na mwenziwe wakiambiana: Inuka, turudi kwetu kwa wenzetu wa ukoo katika nchi, tulikozaliwa, tuzikimbie panga za wanguvu!

17Ndiko, walikomwita Farao, mfalme wa Misri: Angamio, ameikosa siku yake ya kupona!

18Ndivyo, asemavyo Mfalme, Jina lake Bwana Mwenye vikosi: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, atakuja afananaye na Tabori ulio mkuu wa kuipita milima mingine au na Karmeli huko pwani.

19Jifanyizieni vyombo vya kwenda navyo mkitekwa, ninyi wanawali mkaao Misri! Kwani Nofu utakuwa mahame tu kwa kuteketea, msikae mtu.

20Misri ni mori mzuri mno, lakini mbung'o anakuja upesi toka kaskazini.

21Nao warugaruga wao waliokuwa kwao kama ndama wenye manono, hao nao wamegeuka, wakakimbia wote pamoja, hawakusimama, kwani siku ya kuangamia kwao iliwafikia, ndio wakati wa kupatilizwa kwao.

22Mashindo yao yakawa kama ya nyoka akikimbia, kwani wale wanakuja na vikosi vyao, wanawajia wakishika mashoka kama wakata kuni.

23Ndivyo, asemavyo Bwana: Wataikata misitu yao isiyochunguzika, kwani ni wengi kuliko nzige, hawahesabiki.

24Wanawali wa Misri, wamepatwa na soni kwa kutiwa mikononi mwa watu waliotoka kaskazini.

25Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anasema: Mtaniona, ninavyompatiliza Amoni wa No naye Farao na nchi yake ya Misri hata miungu yake na wafalme wake; nitampatiliza Farao kweli nao wote wamwegemeao.[#Yer. 43:12.]

26Nitawatia mikononi mwao wanaozitafuta roho zao, namo mikononi mwa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, namo mikononi mwa watumishi wake. Lakini hayo yatakapokwisha, nchi itakaa watu kama siku za kale; ndivyo, asemavyo Bwana.

Waisiraeli wanatulizwa mioyo.

27Wewe mtumishi wangu Yakobo, usiogope! Nawe Isiraeli, usistuke! Kwani utaniona, nikikuokoa na kukutoa huko mbali, nao walio kizazi chako nitawatoa katika ile nchi, walikopelekwa kwa kutekwa. Yakobo atarudi, akae na kutulia pasipo kuhangaika, kwani hakuna atakayemstusha.[#Yer. 30:10; Yes. 44:2.]

28Ndivyo, asemavyo Bwana: Wewe ntumishi wangu Yakobo, usiogope! Kwani mimi niko pamoja na wewe, kwani nitayamaliza mataifa yote, ambayo nimekutupa kwao, lakini wewe sitakumaliza, nitakuchapa tu, kama yakupasavyo, nisikuache pasipo patilizo lo lote.[#Yer. 30:11.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania