Yeremia 48

Yeremia 48

Mapatilizo ya Wamoabu.

(Taz. Yes. 15; 16; Ez. 25:8-11; Amo. 2:1-3; Sef. 2:8-11.)

1Yatakayowapata Wamoabu. Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Nebo yameupata, kwani umebomolewa! Kiriatemu umepatwa na soni kwa kutekwa, kweli boma lake lililokuwa mlimani limepatwa na soni kwa kustuka.

2Hakuna tena utukufu wa Moabu; mle Hesiboni wanawawazia mabaya kwamba: Twende, tuwang'oe, wasiwe kabila! Nawe Madimeni, utanyamazishwa, panga zitakufuata nyuma.

3Toka Horonemu kunasikilika makelele, maangamizo na mavunjiko ni makubwa.

4Wamoabu wamevunjika, vilio vinasikilika hata Soari.

5Kwani njia ya kupandia Luhiti wanaipanda na kulia, hata katika njia ya kutelemkia toka Horonemu kunasikilika yowe zao wasongekao kwa ajili ya mavunjiko kwamba:

6Kimbieni! Ziponyeni roho zenu! Mwe kama mti wa nyikani usio na majani![#Yer. 17:6.]

7Kwa kuwa unayaegemea matendo yako na vilimbiko vyako, wewe nawe utatekwa, naye Kemosi hana budi kwenda kuhamishwa pamoja na watambikaji wake na wakuu wake.[#1 Fal. 11:7.]

8Mwangamizaji ataujia kila mji, hakuna mji utakaopona, penye bonde pataangamia, napo penye mbuga pataharibika, kama Bwana alivyosema.

9Wapeni Wamoabu mabawa, watoke na kuruka! Kwani miji yao itakuwa mapori, msikae mtu.

10Ameapizwa afanyaye kazi ya Bwana na kulegea! Ameapizwa auzuiaye upanga, usiue![#1 Sam. 15:3,9,11.]

11Wamoabu walikaa pasipo kuhangaishwa tangu ujana wao, wakatulia penye mvinyo zao zenye shimbi, hawazitoi chomboni na kumimina katika kingine, wala hawajakwenda kuhamishwa; kwa hiyo yapendezayo vinywa vyao kuyala ni yaleyale, nayo yapendezayo pua zao kuyanusa hayakugeuka.

12Ndivyo, asemavyo Bwana: Kwa hiyo wataona, siku zikija, nitakapotuma kwao mafundi wa mvinyo, watavipindua vyombo vyao na kuzimwaga mvinyo zilizomo, kisha wataivunja hiyo mitungi yao.

13Ndipo, Wamoabu watakapoona soni kwa ajili ya Kemosi, kama walio wa mlango wa Isiraeli walivyoona soni kwa ajili ya Beteli mlimokuwa na egemeo lao.

14Mwasemaje: Sisi tu wenye nguvu, tu mafundi wa kupiga vita?

15Wamoabu wataangamia, miji yao itapandiwa, nao vijana wao waliochaguliwa watakuwa hawana budi kutelemka, wauawe; ndivyo, asemavyo Mfalme, Jina lake ni Bwana Mwenye vikosi.

16Angamio lao Wamoabu liko karibu, mabaya yao yanakuja upesi sana.

17Nyote mkaao na kuwazunguka waombolezeeni pamoja nao wote walijuao jina lao! Semeni: Kumbe fimbo yenye nguvu imevunjika! Nayo ilikuwa bakora yenye utukufu!

18Ondokeni penye utukufu, mkae mchangani penye ugumu, ninyi wanawali mkaao Diboni! Kwani mwenye kuwaangamiza Wamoabu anapanda kufika kwako, ayabomoe maboma yako!

19Ninyi mkaao Aroeri, simameni njiani na kupeleleza mkiwauliza watoro walioepuka, mkisema: Kumetendeka nini?

20Wamoabu wamepatwa na soni kwa kuvunjika; lieni na kupaza sauti: Yatangazeni kwenye Arnoni, ya kuwa Wamoabu wameangamia!

21Mapatilizo yameijia nchi yenye mbuga huko Holoni na Yasa na Mefati,

22na Diboni na Nebo na Beti-Dibulatemu,

23na Kiriatemu na Beti-Gamuli na Beti-Meoni,

24na Kirioti na Bosira na miji yote ya nchi ya Moabu iliyoko mbali, nayo iliyoko karibu.

25Pembe ya Moabu imekatwa, nao mkono wake umevunjwa; ndivyo, asemavyo Bwana.

26Walevyeni! Kwani wamejikuza kuliko Bwana; na waanguke kifudifudi katika matapiko yao, wachekwe nao hao![#Yer. 25:15.]

27Au Waisiraeli hawakuchekwa kwenu? Je? Walionwa kwenye wezi, mkiwatingishia vichwa kila mlipowataja?

28Ninyi mkaao Moabu, tokeni mijini, mkae magengeni, mwe kama hua wanaojenga matundu yao juu penye miamba iliyokatika.

29Tumesikia, ya kuwa Wamoabu walijivuna sanasana, wakajikuza kwa kujivuna kwao, kwa kiburi chao wakawaza makuu mioyoni mwao.

30Ndivyo, asemavyo Bwana: Mimi nimeyajua makorofi yao, ya kuwa hayana maana, nayo maneno yao makuu, ya kuwa hawakuyafanya.

31Kwa hiyo ninawalilia Wamoabu, ninawapigia Wamoabu wote makelele; wengine wanawapigia kite watu wa Kiri-Heresi.

32Kuliko Yazeri ninawalilia ninyi mizabibu ya Sibuma, matawi yenu yaliendelea kufika baharini, yalifika kweli kwenye bahari ya Yazeri; siku za kiangazi walipochuma zabibu zenu, mara mwangamizaji akaja.

33Ndipo, shangwe za furaha zilipotoweka Karmeli na katika nchi ya Moabu. Nayo mvinyo iliyokuwa kamulioni nikaikomesha, hawakamui tena kwa kupiga shangwe; shangwe zao sizo shangwe tena.

34Toka Hesiboni wanapiga makelele, hata Elale na Yasa wanapaza sauti zao, tena toka Soari hata Horonemu na Eglati-Selisia hulia, ya kuwa nayo maji ya Nimurimu yatakuwa yamekauka.

35Ndivyo, asemavyo Bwana: Nitawakomesha Wamoabu, wasipande vilimani kuivukizia miungu yao.

36Kwa hiyo moyo wangu unawapigia Wamoabu kite na kuvuma kama zomari, nao watu wa Kiri-Heresi moyo wangu unawapigia kite na kuvuma kama zomari, kwa kuwa mapato waliyojipatia yamepotea.[#Yer. 4:19; Yes. 15:7; 16:11.]

37Kwani vichwa vyote vitakuwa vyenye vipara, nazo ndevu zote zitakuwa zimenyolewa, nayo mikono yote itakuwa yenye chale, navyo viuno vyote vitakuwa na magunia.[#Yer. 47:5.]

38Po pote vipaani katika nchi ya Moabu napo barabarani po pote patakuwa na maombolezo, kwani nitawavunja Wamoabu, kama ni chombo kisichopendeza; ndivyo, asemavyo Bwana.

39Kumbe wamevunjika! Pigeni vilio! Kumbe Wamoabu wamezigeuza kosi zao kwa soni! Tangu hapo Wamoabu watakuwa kicheko na kitisho kwao wote wakaao na kuwazunguka.

40Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Tazameni, anawarukia Wamoabu kama kozi na kuwakunjulia mabawa yake.[#Yer. 49:22.]

41Kirioti umetekwa, nayo miji yenye maboma imechukuliwa; kwa hiyo mioyo ya wapiga vita wa Moabu itakuwa siku ile kama moyo wa mwanamke anayetaka kuzaa.

42Wamoabu wataangamizwa, wasiwe taifa tena, kwa kuwa wamejikuza kuliko Mungu.

43Mastuko na miina na matanzi yatawapata ninyi mkaao Moabu; ndivyo, asemavyo Bwana.

44Ayakimbiaye mastuko ataanguka mwinani; atokaye mwinani atakamatwa na tanzi; haya yatakuwa hapo, nitakapowatimilizia hao Wamoabu mwaka wa mapatilizo yao; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yes. 24:17-18.]

45Watoro wakisimama kivulini kwenye Hesiboni kwa kuishiwa nguvu, moto utatoka Hesiboni namo Sihoni kati, moto uwakao sana utatoka, utavila vipanja vya Wamoabu nazo tosi zao wapigao vita.[#4 Mose 21:28-29.]

46Yatawapata, ninyi Wamoabu! Ukoo wake Kemosi utaangamia! Kwani wanao wa kiume watachukuliwa kwenda utumwani, nao wanao wa kike watakwenda kuwa vijakazi.

47Kisha nitayafungua mafungo ya Moabu, siku zitakapotimia; ndivyo, asemavyo Bwana.

Mpaka hapa ni hukumu za Moabu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania