The chat will start when you send the first message.
1Hili ndilo neno, Bwana alilolisema kwa kinywa chake Yeremia kuwaambia Wababeli walioko katika nchi ya Wakasidi.[#Yes. 13:14.]
2Yatangazeni kwa mataifa, wayasikie! Twekeni bendera! Yasimulieni, msiyafiche! Semeni: Babeli umetekwa, Beli amepatwa na soni, Merodaki amestuka, vinyago vyao vimeumbuliwa, mifano yao imevunjika![#Yes. 46:1.]
3Kwani taifa lililotoka upande wa kaskazini limewapandia, hilo limeiharibu nchi yao iwe peke yake, isikae tena wala mtu wala nyama, wamekimbia kwenda zao.
4Ndivyo, asemavyo Bwana: Siku zile za wakati huo ndipo, wana wa Isiraeli pamoja na wana wa Yuda watakapokuja wakienda na kulia machozi; hivyo watakwenda kumtafuta Bwana Mungu wao.[#Yer. 31:9.]
5Watauliza njia ya kwenda Sioni; ndiko, nyuso zao zinakoelekea kwamba: Njoni kuandamana na Bwana, tukifanya agano la kale na kale lisilosahauliwa tena!
6Walio ukoo wangu walikuwa kondoo waliopotea, wachungaji wao waliwapoteza, wakatangatanga milimani, walipotoka mlimani wakaendea kilima kingine, wakakisahau kituo chao.
7Wote waliowaona wakawala, nao waliowasonga wakasema: Hatukosi. Hayo yakawapata, kwa kuwa walimkosea Bwana aliyekuwa lisho lao la kweli, ni yeye Bwana, baba zao waliyomngojea.
8Kimbieni, mwutoke mji wa Babeli, mliomo! Itokeni nayo nchi ya Wakasidi, mwe kama madume ya kondoo wanaoyatangulia makundi![#Yer. 51:6,45.]
9Kwani mtaniona mimi, nikiinua mkutano wa mataifa makubwa yatokayo upande wa kaskazinni, niyapandishe kwenda Babeli; watakapojipanga, hapohapo ndipo, utakapotekwa. Mishale yao ni kama ya mpiga vita mwerevu asiyerudi mikono mitupu.
10Nchi ya Wakasidi itatekwa, nao watakaoiteka watashiba wote; ndivyo, asemavyo Bwana.
11Kwa kuwa mwalifurahi, mkapiga vigelegele hapo, mlipolipokonya fungu langu, mkachezacheza kama ndama wakipura, mkalia kama farasi wenye nguvu:[#5 Mose 32:27; Yes. 10:5,7,15.]
12mama yenu atapatwa na soni kabisa, yeye aliyewazaa ataiva uso; hapo mtaona, hilo taifa lililokuwa la mwisho linavyogeuka kuwa nyika kavu na jangwa.
13Kwa kukasirika kwake Bwana hautakaa mtu, wote pia utakuwa peke yake tu, kila atakayepapita palipokuwa na Babeli, atapastuka na kuuzomea kwa ajili ya mapigo yake yote.[#Yer. 49:17; 51:37.]
14Jipangeni na kuuzunguka Babeli, ninyi nyote mpindao pindi! Upigeni mishale, msiitendee choyo! Kwani wamemkosea Mungu.
15Pigeni vigelegele po pote! Umejitia mikononi mwenu! Maboma yake yamebomolewa, kuta zake zimeangushwa, kwani hili ndilo lipizi la Bwana, kwa hiyo ulipisheni! Kama ulivyofanya, ufanyizieni![#Ufu. 18:6.]
16Huko Babeli wang'oeni wapanzi nao wavunaji washikao miundu siku za mavuno! Kwa kuzikimbia panga za wenye nguvu kila mtu atawageukia walio wa ukoo wake, kwa hiyo kila mtu ataikimbilia nchi ya kwao.
17Waisiraeli ni kama kondoo waliotawanyika kwa kufukuzwa na simba: kwanza mfalme wa Asuri aliwala, mwisho Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, aliwavunja mifupa.
18Kweli hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Mtaniona, nikimpatiliza mfalme wa Babeli na nchi yake, kama nilivyompatiliza mfalme wa Asuri.
19Nitawarudisha Waisiraeli kwao, walikokaa, wajilishe mazao ya Karmeli na ya Basani, roho zao zishibe milimani kwa Efuraimu nako huko Gileadi.
20Ndivyo, asemavyo Bwana: Siku zile zitakapotimia, manza, Waisiraeli walizozikora, zitatafutwa, lakini zitakuwa haziko, nayo makosa ya Wayuda, lakini hayataonekana, kwani nitayaondoa kwao, nitakaowasaza.[#Yer. 51:20.]
21Ipandie nchi yenye makatavu mawili, uingie namo, wakaamo wenye kupatilizwa! Waue na kuwamaliza walio nyuma yao! Yafanye yote, kama nitakavyokuagiza!
22Sauti za vita zinasikilika katika nchi hii, nayo mavunjiko ni makubwa.
23Kumbe nyundo iliyozipiga nchi zote imepondeka kwa kuvunjikavunjika! Kumbe Babeli umegeuka kuwa wa kustukiwa na mataifa yote![#Yer. 31:34; 33:8.]
24Nimekutegea, wewe Babeli, ukanaswa, nawe ulikuwa huvijui; umeonwa, ukakamatwa, kwani umemtaka Bwana, mpigane.
25Bwana amelifungua limbiko lake, akayatoa mata ya makali yake, kwani yeye Bwana Mungu Mwenye vikosi yuko na kazi katika nchi ya Wakasidi.
26Njoni huku na kutoka kwenye mapeo ya nchi! Vifungueni vyanja vyake vya ngano, mzikusanye kuwa chungu, kisha zimalizeni kwa kuziteketeza, masao yasipatikane kamwe!
27Wachomeni ng'ombe wao wote kwa mikuki, waanguke kwa kuchinjwa hivyo, Watapatwa na mambo, kwani siku yao inakuja, watakapopatilizwa.
28Sauti zao walioitoka nchi ya Babeli kwa kukimbia mbio sana zinasikilika Sioni, wakiyatangaza malipizi ya Bwana Mungu wetu, jinsi alivyolilipizia Jumba lake takatifu!
29Waiteni wapiga mishale wote wanaopinda pindi, waje Babeli, wapige kambi zao kuuzunguka, usipate pa kukimbilia. Ulipisheni matendo yake! Yote, uliyoyafanya, ufanyizieni yaleyale! Kwani umejivuna kuwa mkuu kuliko Bwana, kuliko yeye aliye Mtakatifu wa Isiraeli.[#Yer. 50:15.]
30Kwa hiyo vijana wako wataangushwa barabarani mwako, nao waume wote wa kupiga vita watanyamazishwa siku hiyo; ndivyo, asemavyo Bwana.
31Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu Mwenye vikosi: Utaniona, nikikujia, wewe mkorofi; kwani itakuja siku yako, nitakapokupatiliza.
32Ndipo, mkorofi atakapojikwaa, aanguke, lakini hatakuwako atakayemwinua; mijini mwake nitawasha moto, uiteketeze yote pande zake zote.
33Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Wameteseka wana wa Isiraeli pamoja na wana wa Yuda; wote waliowateka na kuwahamisha wanawashika, wakakataa kuwapa ruhusa kwenda.
34Lakini mkombozi wao ni mwenye nguvu, Bwana Mwenye vikosi ni Jina lake. Yeye atawagombea hayo magomvi yao, kusudi aitulize nchi, lakini wakaao Babeli atawahangaisha.
35Ndivyo, asemavyo Bwana: Panga na ziwajie Wakasidi nao wakaao Babeli nao wakuu wao nao werevu wao wa kweli!
36Panga na ziwajie wapuzi, wapumbae! Panga na ziwajie wapiga vita wao, wazimie kwa kustuka!
37Panga na ziwajie farasi wao na magari yao nao warugaruga walio katikati yao, wawe kama wanawake! Panga na zivijie navyo vilimbiko vyao, vipokonywe![#Yer. 51:30.]
38Jua kali na liyapige maji yao, yakauke! Kwani nchi hii ni ya vinyago, nao wenyeji wameingiwa na wazimu kwa ajili ya mifano yao.
39Kwa hiyo watakaa humo nyama wa porini na mbwa wa mwitu, nao mbuni watakaa mwake, lakini watu hawatakaa humo kale na kale, ila utakaa pasipo mtu kwa vizazi na vizazi.
40Ndivyo, asemavyo Bwana: Kama Mungu alivyoangamiza Sodomu na Gomora pamoja na vijiji vyao, hivyo napo hapa hapatakaa mtu, wala hapatalala mgeni wa kimtu.[#1 Mose 19:24-25.]
41Utaona, watu wakija toka kaskazini, tena taifa kubwa na wafalme wengi watainuka mapeoni kwa nchi.[#Yer. 50:9.]
42Wanashika pindi na mikuki, ni wakorofi, hawana huruma, sauti zao huvuma kama bahari, hupanda farasi, wako tayari kupiga kama mtu wa vitani; wanakujia wewe, binti Babeli.[#Yer. 6:23.]
43Mfalme wa Babeli amezisikia habari zao; ndipo, mikono yake ilipolegea, masongano yakamshika na uchungu, kama mwanamke anayetaka kuzaa.
44Kama simba anavyopanda akitoka machakani kwenye Yordani, ajie maboma yenye nguvu, ndivyo, nitakavyowakimbiza kwao kwa mara moja, naye aliyechaguliwa nitamweka kuwa mkuu wao, kwani yuko nani afananaye na mimi? Au yuko nani atakayeniwekea siku? Yuko mchungaji gani atakayesimama usoni pangu?[#Yer. 49:19-21.]
45Kwa hiyo lisikieni shauri la Bwana, aliloukatia Babeli, nayo mawazo yake, aliyoiwazia nchi ya Wakasidi kwamba: kweli watakaowakokotakokota ndio wadogo wa makundi, kweli nchi yao yenyewe itawastukia.
46Kwa mtutumo wa kutekwa kwa Babeli nchi itatetemeka, navyo vilio vitasikilika kwa mataifa.