The chat will start when you send the first message.
1Sekedia alikuwa mwenye miaka 21 alipopata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 11; jina la mama yake ni Hamutali, binti Yeremia, wa Libuna.
2Akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana kama yote, Yoyakimu aliyoyafanya.
3Kwa kuwa Bwana aliwakasirikia Wayerusalemu na Wayuda, akawatupa, waondoke usoni pake, ikawa hivyo: Sedekia akakataa kumtii mfalme wa Babeli.
4Ikawa katika mwaka wa 9 wa ufalme wake mwezi wa kumi siku ya kumi ya mwezi, ndipo, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, alipoujia Yerusalemu yeye na vikosi vyake vyote, wakapiga makambi huko, wakaujengea boma la kuuzungusha.
5Mji ukaja kusongwa hivyo na kuzingwa mpaka mwaka wa 11 wa mfalme Sedekia.
6Katika mwezi wa nne siku ya tisa njaa ikazidi mle mjini, watu wa nchi hii hawakuwa na vyakula.
7Ndipo, mji ulipobomolewa, nao wapiga vita wote wakatoroka na kutoka mjini na usiku kwa njia ya lango lililokuwa kati ya kuta mbili penye bustani ya mfalme; Wakasidi walipokuwa wamelala usingizi na kuuzunguka mji, wale wakashika njia ya nyikani.
8Kisha vikosi vya Wakasidi vikamfuata mfalme na kupiga mbio, vikampata Sedekia katika nyika ya Yeriko, navyo vikosi vyake vyote vilikuwa vimetawanyika na kumwacha.
9Wakamkamata mfalme, wakampeleka kwa mfalme wa Babeli huko Ribula katika nchi ya Hamati, akasema naye na kumhukumu.
10Mfalme wa Babeli akawaua wana wa Sedekia machoni pake, nao wakuu wote wa Wayuda akawaua huko Ribula.
11Kisha akayapofua macho yake Sedekia, akamfunga kwa minyororo; kisha mfalme wa Babeli akampeleka Babeli, akamtia kifungoni mpaka siku ya kufa kwake.[#Yer. 32:5.]
12Katika mwezi wa tano siku ya kumi ya mwezi, - ulikuwa mwaka wa 19 wa mfalme Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, - ndipo, Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, aliyesimama usoni pa mfalme wa Babeli, alipoingia Yerusalemu.
13Akaiteketeza Nyumba ya Bwana na nyumba ya mfalme, nazo nyumba zote za Yerusalemu, nazo nyumba kubwa zote akaziteketeza kwa moto.
14Kisha vikosi vyote vya Wakasidi waliokuwa na mkuu wao waliomlinda mfalme vikazibomoa kuta za boma lililouzunguka Yerusalemu.
15Kisha Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, akawateka na kuwahamisha wanyonge wa ukoo huo nayo masao ya watu waliosalia mjini nao waliokuwa wamemwangukia mfalme wa Babeli na kurudi upande wake nao mafundi waliosalia.
16Lakini kwa wanyonge wa nchi Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, wengine akawasaza, waiangalie mizabibu, wengine walime tu.
17Lakini zile nguzo mbili za shaba zilizokuwa penye Nyumba ya Bwana na vile vilingo vya kuwekea mitungi ya maji na bahari ya shaba iliyokuwa penye Nyumba ya Bwana Wakasidi wakazivunja, nazo zile shaba zao zote wakazipeleka Babeli.[#Yer. 27:19-22.]
18Hata masufuria na majembe na makato ya kusafishia mishumaa na vyano na kata navyo vyombo vyote pia vya shaba vilivyotumiwa Nyumbani mwa Bwana wakavichukua.
19Nazo sahani na mikungu na mabakuli na vyano na taa na vijiko na vivukizio vilivyokuwa vya dhahabu tupu navyo vilivyokuwa vya fedha tupu mkuu wao waliomlinda mfalme akavichukua.
20Zile nguzo mbili na ile bahari moja na zile ng'ombe kumi na mbili zilizokuwa chini yake na vile vilingo vya kuwekea mitungi ya maji, ambavyo mfalme Salomo alivitengenezea Nyumba ya Bwana, shaba zao hivyo vyombo vyote hazikuwezekana kupimwa kwa mizani.[#1 Fal. 7:15-47.]
21Zile nguzo urefu wake nguzo moja ulikuwa mikono kumi na nane, nayo kamba ya mikono kumi na miwili ikaizunguka, unene wa shaba ulikuwa nyanda nne, ndani palikuwa penye uvurungu.
22Juu yake palikuwa na kilemba cha shaba, urefu wa kwenda juu wa hiki kilemba kimoja ulikuwa mikono mitano; hiki kilemba kilikuwa kimezungukwa na misuko kama ya mkeka iliyokuwa yenye komamanga, yote pia ni ya shaba; nayo nguzo ya pili ilikuwa vivyo hivyo, nayo ilikuwa yenye komamanga.
23Komamanga zilikuwa tisini na sita zilizoning'inia; komamanga zote penye msuko wa nguzo moja zilikuwa mia.
24Mkuu wao waliomlinda mfalme akamchukua mtambikaji mkuu Seraya na mtambikaji wa pili Sefania nao walinda kizingiti watatu.[#1 Mambo 6:14.]
25Namo mjini akachukua mtumishi mmoja wa nyumbani mwa mfalme aliyewekwa kuwa mkuu wa kuwasimamia wapiga vita na watu saba waliokuwa na kazi machoni pa mfalme waliopatikana mjini na mwandishi wa mkuu wa vikosi aliyewaandika watu wa nchi waliotakiwa uaskari na watu sitini wa shambani waliopatikana mle mjini.
26Hao akawachukua Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, akawapeleka Ribula kwa mfalme wa Babeli.
27Naye mfalme wa Babeli akawapiga na kuwaua huko Ribula katika nchi ya Hamati. Kisha akawahamisha Wayuda, waitoke nchi yao.
28Watu wa ukoo huu, Nebukadinesari aliowahamisha katika mwaka wa saba, ndio hawa: Wayuda 3023.[#2 Fal. 24:11-16.]
29Katika mwaka wa kumi na nane wa ufalme wa Nebukadinesari waliohamishwa Yerusalemu ni 832.
30Katika mwaka wa ishirini na tatu wa ufalme wa Nebukadinesari, Nebuzaradani, mkuu wao waliomlinda mfalme, akahamisha Wayuda 745; wote pamoja walikuwa 4600.
31Ikawa katika mwaka wa 37 wa kuhamishwa kwake Yoyakini, mfalme wa Wayuda, katika mwezi wa kumi na mbili siku ya ishirini na tano, ndipo, Ewili-Merodaki, mfalme wa Babeli, alipomwonea uchungu Yoyakini, mfalme wa Wayuda; ikawa katika mwaka huohuo, alipoupata ufalme, akamtoa kifungoni,
32akasema naye maneno mema, akampa kiti chake cha kifalme juu ya viti vya kifalme vya wafalme wengine waliokuwa naye huko Babeli.
33Ndipo, alipoyavua mavazi yake ya kifungoni, akala chakula usoni pa mfalme pasipo kukoma siku zote, alizokuwapo.
34Nazo mali za kujitunza kila siku akapewa na mfalme wa Babeli siku zote, alizokuwapo, akapata siku kwa siku yaliyompasa mpaka siku ya kufa kwake.