The chat will start when you send the first message.
1Jihimizeni kukimbia, ninyi wana wa Benyamini, mtoke Yerusalemu! Namo Tekoa pigeni baragumu! Nako kwenye Beti-Keremu twekeni bendera, kwani toka kaskazini yanakuja mabaya yanayotisha na mavunjiko yaliyo makuu.[#Yer. 4:6.]
2Binti Sioni aliye mzuri aliyejizoeza mororo nitamwangamiza.
3Watakuja kwake wachungaji na makundi yao, watapiga mahema kwake na kumzinga, walishe kila mmoja fungu lake wakisema: Jitakaseni, mpigane nao![#Yer. 4:17.]
4Inukeni, tupapandie, jua lingaliko juu! A, tumechelewa sisi! Jua linataka kuchwa, vivuli vya jioni vinajivuta.
5Inukeni! Tupande na usiku, tuyaharibu majumba yake![#Yer. 5:1.]
6Kwani ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Kateni miti, kisha mwifukie kuwa boma la kuuzinga Yerusalemu! Maana ndio mji utakaopatilizwa kwa ajili ya ukorofi uliomo mwake.
7Kama kisima kinavyoyatoa maji yake, ndivyo, unavyoyatoa mabaya yake. Makorofi na mapotovu husikilika mwake, macho yangu huona siku zote maumivu na mapigo.
8Onyeka, Yerusalemu, roho yangu isije kujitenga nawe, nisikugeuze kuwa nchi yenye mapori matupu yasiyokaa watu!
9Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Masao yako, Isiraeli, yataokotezwa kama yake mzabibu; ukunjue tena mkono wako kama mchuma zabibu, akiyatazama matawi!
10Nimwambie nani na kumshuhudia, wapate kusikia? Tazama! Hawakutahiriwa penye masikio, hawawezi kusikia. Neno lake Bwana likawa kicheko kwao, hawapendezwi nalo.
11Nami nimejaa makali ya Bwana yenye moto, nimechoka kuyazuia. Basi, na yapige watoto wanaocheza njiani nao vijana, wakikusanyika pamoja, kwani wote, waume na wake, wazee na wakongwe, watashikwa nayo.
12Nyumba zao zitaachiliwa wengine, hata mashamba na wanawake vilevile, kwani nitawakunjulia mkono wangu wao wakaao katika nchi hii; ndivyo, asemavyo Bwana.
13Kwani wao wote, walivyo wadogo mpaka wakiwa wakubwa, hutamani mali tu; hata wafumbuaji na watambikaji wote pia hufanya yenye uwongo.[#Yer. 8:10-12.]
14Madonda yao walio wazaliwa wa ukoo wangu huyaponya juujuu wakisema: Tengemaneni! Tengemaneni! lakini hakuna utengemano.[#Yer. 8:11; Ez. 13:10,16; 1 Tes. 5:3.]
15Watapatwa na soni, kwani hufanya yatapishayo; lakini hawaoni soni, wala hawajui kuiva nyuso. Kwa hiyo wataanguka pamoja na wenzao watakaoanguka siku hiyo, nitakapowapatiliza; ndipo, watakapojikwaa. Ndivyo, Bwana anavyosema.
16Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Simameni njiani, mwone! Ulizeni mapito ya kale, kama njia njema ni ipi? Hiyo ishikeni, mzipatie roho zenu kituo! Wakasema: Hatutaishika.[#Yer. 44:16; Mat. 11:29.]
17Nitawawekea walinzi, mwiangalie sauti ya baragumu! Wakasema: Hatutaiangalia.[#Yes. 52:8; Ez. 3:17.]
18Kwa hiyo sikieni, ninyi wamizimu! Ninyi mliokutanika, yatambueni yatakayokuwa kwao!
19Nayo nchi, sikia! Na mnione, nikiwaletea mabaya watu wa ukoo huu, ndiyo yaliyozaliwa na mawazo yao, kwani maneno yangu hawakuyasikiliza, nayo Maonyo yangu wameyakataa.[#5 Mose 32:1; Yes. 1:2.]
20Uvumba utokao Saba unanifaliaje? Nayo manukato yatokayo nchi ya mbali ni ya nini? Ng'ombe zenu za tambiko hazinipendezi, wala vipaji vyenu vya tambiko havinifurahishi.[#Yes. 1:11.]
21Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Nitazameni, jinsi ninavyoweka mawe ya kukwazia njiani kwao walio ukoo huu, nao watajikwaa wote pia, baba na watoto, wenyeji na wenzao wataangamia.[#Yes. 8:14.]
22Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Tazameni! Watu watakuja toka nchi ya kaskazini, taifa kubwa litainuka kwenye mapeo ya nchi.[#Yer. 5:15; 5 Mose 28:49.]
23Hushika pindi na mikuki, ni wakorofi pasipo huruma, makelele yao ni kama kuvuma kwa bahari, nao hupanda farasi; wamejivika kama watu waendao vitani, wapigane na wewe, binti Sioni.[#Yer. 50:42.]
24Tulipokisikia kivumo chao, mikono yetu ikalegea, tukasongeka, uchungu ukatushika kama wa mzazi.
25Msitoke kwenda shambani, wala njiani msiende! Kwani panga za adui ziko, zinawastusha po pote.
26Mlio wazaliwa wa ukoo wangu, jivikeni magunia, mpate kugaagaa mavumbini! Ombolezeni kama waliofiwa na mwana wa pekee! Vilio na viwe vyenye uchungu sana! Kwani mara mwangamizi atatujia.[#Amo. 8:10.]
27Nimekuweka kwao walio ukoo wangu, uwajaribu, kwani ni wagumu, uwatambue ukizijaribu njia zao.
28Wao wote ndio wabishi wenyewe waendao wakisingizia, ni wagumu kama shaba na vyuma, wao wote ndio wapotezaji wabaya.[#Ez. 22:18.]
29Mifuo ikifukutwa, mle motoni hutoka shaba tu. Imekuwa kazi bure kuyeyusha mara kwa mara, kwani mabaya yaliyomo hayakutengeka.
30Sharti waitwe fedha zitupwazo, kwani Bwana amewatupa.[#Yes. 1:22.]