The chat will start when you send the first message.
1*Neno lililomjia Yeremia likitoka kwa Bwana ni hili:
2Simama langoni mwa Nyumba ya Bwana, ulitangaze neno hili huko ukisema: Lisikieni neno la Bwana, ninyi Wayuda wote mnaoingia humu malangoni kumwangukia Bwana!
3Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli: Ziangalieni njia zenu na matendo yenu, yawe mema! Ndipo, nitakapowakalisha katika nchi hii.[#Yer. 26:13; Yes. 1:16.]
4Msijiegemeze maneno ya uwongo kwamba: Nyumba ya Bwana, Nyumba ya Bwana, Nyumba ya Bwana ni hii!
5Ila jikazeni, njia zenu na matendo yenu yawe mema, mfanyiziane yanyokayo kila mtu na mwenziwe!
6Msiwakorofishe wageni wala wafiwao na wazazi wala wajane! Wala msimwage mahali hapa damu zao wasiokosa! Wala msifuate miungu mingine! Maana hivyo mnajipatia mabaya.[#2 Mose 22:21-22.]
7Ndipo, nitakapowakalisha mahali hapa katika nchi hii, niliyowapa baba zenu, iwe yao tangu kale hata kale.
8Tazameni! Ninyi mnaojiegemeza maneno ya uwongo yasiyofaa:
9Huiba, huua, huzini, huapa kwa uwongo, humvukizia Baali, hufuata miungu mingine, msiyoijua.
10Kisha mnakuja kusimama machoni pangu katika Nyumba hii iliyoitwa kwa Jina langu, mkasema: Tumepona! mpate kuyafanya matapisho hayo yote.[#Yer. 4:10.]
11Je? Nyumba hii iliyoitwa kwa Jina langu imegeuka kuwa pango la wanyang'anyi machoni penu? Mimi nami ninayaona kweli. Ndivyo, asemavyo Bwana.*[#Mat. 21:13.]
12Haya! Nendeni mahali pangu kule Silo, nilipolikalisha Jina langu kwanza, myaone yote, niliyopafanyizia kwa ajili ya ubaya wao Waisiraeli walio ukoo wangu![#Yos. 18:1; 1 Sam. 4:12; Sh. 78:60.]
13Sasa ndivyo, asemavyo Bwana: nanyi mmeyafanya hayo matendo yote, tena nalisema nanyi pasipo kuchoka kusema, lakini hamkusikia, nikawaita, lakini hamkuitikia.[#Fano. 1:24; Yes. 65:12.]
14Kwa hiyo nitaifanyizia Nyumba hii iliyoitwa kwa Jina langu, ninyi mnayoitumia ya kujiegemezea, hata mahali hapo, nilipowapa ninyi na baba zenu, nitapafanyizia, kama nilivyofanya huko Silo.[#Yer. 26:6.]
15Nitawatupa, mwondoke machoni pangu, kama nilivyowatupa ndugu zenu wote pia walio kizazi chake Efuraimu.[#2 Fal. 17:18,20,23.]
16Wewe nawe usiwaombee wao wa ukoo huu! Wala usipaze sauti kunilalamikia kwa ajili yao, wala usinihimize! Kwani hapo sikusikii.[#Yer. 11:14; 14:11.]
17Huyaoni, wanayoyafanya katika miji ya Yuda namo Yerusalemu katika barabara zake?
18Watoto huokota kuni, nao baba huziwasha moto, wanawake wakikanda unga wa kufanya vikate vya mfalme wa kike wa mbinguni, tena humwaga vinywaji vya kutambikia miungu mingine, kusudi waniumize moyoni.[#Yer. 44:17.]
19Ndivyo, asemavyo Bwana: Hao watakao kuniumiza mimi hawajiumizi wenyewe, nyuso zao zipate kutiwa soni?
20Kwa hiyo hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Wataona, jinsi makali yangu yenye moto yatakavyomwagwa mahali hapa, yachome watu na nyama na miti ya mashamba na mazao ya nchi, yawake moto usiozimika.
21Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Ng'ombe zenu za tambiko za kuteketezwa nzima ziongezeni kwa ng'ombe zenu za tambiko za kuchinjwa, mpate kula nyama.[#Sh. 50:8-15.]
22Kwani sikuwaambia baba zenu, wala sikuwaagiza, nilipowatoa katika nchi ya Misri, watoe ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za kuchinjwa.[#Mika 6:6-8; 1 Sam. 15:22.]
23Kweli niliwaagiza neno hili tu kwamba: Isikieni sauti yangu! Ndivyo, nitakavyokuwa Mungu wenu, nanyi mtakuwa ukoo wangu. Kisha zishikeni njia zote, nitakazowaagiza, mpate kuona mema![#2 Mose 19:5.]
24Lakini hawakusikia, wala hawakuyatega masikio yao, wakaendelea kwa mashauri na kwa ushupavu wa mioyo yao mibaya, wakanionyesha migongo, lakini sizo nyuso.[#Yer. 11:8; Yes. 65:2.]
25Vikawa hivyo tangu siku ile, baba zenu walipotoka katika nchi ya Misri mpaka siku hii ya leo; nami nalituma kwenu watumishi wangu wote walio wafumbuaji, sikuchoka hata siku moja.
26Lakini hawakunisikia, wala hawakuyatega masikio yao, wakazishupaza kosi zao, wakafanya mabaya kuwashinda baba zao.[#Yer. 16:12.]
27Nawe ukiwaambia maneno haya yote, hawatakusikia, ukiwaita, hawatakuitikia.
28Basi, uwaambie: Taifa hili ndilo lisiloisikia sauti ya Bwana Mungu wao, wala hawakutaka kuonyeka. Welekevu umepotea, umetoweka vinywani mwao.[#Yer. 5:1.]
29Binti Sioni, zinyoe nywele zako za urembo, uzitupe! Piga kilio vilimani juu kusikokuwa na vijiti! Kwani Bwana amekikataa kizazi kilichomkasirisha, akakitupa.
30Kwani ndivyo, asemavyo Bwana: Wana wa Yuda wamefanya yaliyo mabaya machoni pangu, wakaweka matapisho yao katika Nyumba hii inayoitwa kwa Jina langu, waichafue.[#Yer. 32:34.]
31Wakapajenga pa kumtambikia Tofeti katika bonde la Mwana wa Hinomu, wateketeze hapo motoni wana wao wa kiume na wa kike; nami sikuwaagiza hivyo, wala havikunijia moyoni.[#3 Mose 18:21; 2 Fal. 23:10.]
32Kwa hiyo ndivyo, asemavyo Bwana: Wataona kweli, siku zikija, pasipotajwa tena Tofeti wala bonde la Mwana wa Hinomu, ila pataitwa Bonde la Uuaji; ndipo, watakapozikia kwenye Tofeti kwa kukosa pengine.[#Yer. 19:6.]
33Nayo mizoga ya watu wa ukoo huu itakuwa chakula cha ndege wa angani na cha nyama wa porini, asiweko atakayewatisha.[#Yer. 9:22; 19:7.]
34Ndipo, nitakapokomesha katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu sauti za vicheko na sauti za furaha, hata sauti za wachumba wa kiume na wa kike, kwani nchi hii itakuwa mavunjiko tu.[#Yer. 16:9.]