The chat will start when you send the first message.
1Ndivyo, asemavyo Bwana: Siku zile wataifukua makaburini mwao mifupa ya wafalme wa Yuda na mifupa ya wakuu wao na mifupa ya watambikaji na mifupa ya wafumbuaji na mifupa yao waliokaa Yerusalemu.
2Kisha wataitandaza penye jua na penye mwezi napo penye kikosi chote cha mbinguni, maana wamepapenda, wakapatunukia, wakapafuata, wakapatafuta, wakapaangukia; haitaokotwa, wala haitazikwa tena, itakuwa mbolea tu juu ya nchi.[#5 Mose 4:19; Yer. 14:16.]
3Nayo masazo yote yatakayosazwa ya mlango huu mbaya yatapendezwa zaidi na kufa kuliko kuwapo mahali po pote, nilipowatupia hayo masazo; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi.
4*Uwaambie: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Je? Wako waangukao wasioinuka tena? Au yuko ageukaye asiyerudi tena?
5Mbona ukoo huu wa Yerusalemu umegeuka pasipo kurudi kale na kale? Wameyashika madanganyifu, wakakataa kurudi.
6Nikaangalia na kusikiliza, hawasemi yaliyo sawa, wala hakuna mtu aujutiaye ubaya wake kwamba: Je? Nimefanya nini? Kila mmoja hugeuka kwa kujikimbilia kwao kama farasi akimbiaye vitani.
7Naye korongo wa angani huzijua siku zake, hata hua na kinega na mbayuwayu huzishika siku zao za kuja, lakini walio ukoo wangu hawayajui yampasayo Bwana.[#Yes. 1:3.]
8Mnasemaje: Sisi tu werevu wa kweli, nayo Maonyo yake Bwana tunayo? Ndio, lakini tazameni! Kalamu zao waandishi zenye uwongo zimeyageuza kuwa uwongo!
9Walio werevu wa kweli wamepatwa na soni, wanazizimuka kwa kuumbuliwa; Neno lake Bwana wamelitupa, sasa wako na werevu gani tena ulio wa kweli?*
10Kwa hiyo nitawapa wengine wake zao, nayo mashamba yao nitawapa wale watakaowatwaa, kwani wao wote, walivyo wadogo mpaka wakiwa wakubwa, hutamani mali tu, hata wafumbuaji na watambikaji wote pia hufanya yenye uwongo.[#Yer. 6:12-15; Yes. 56:11.]
11Madonda yao walio wazaliwa wa ukoo wangu huyaponya juujuu wakisema: Tengemaneni! Tengemaneni! Lakini hakuna utengemano.[#Yer. 6:14.]
12Watapatwa na soni, kwani hufanya yatapishayo; lakini hawaoni soni, wala hawajui kuiva nyuso. Kwa hiyo wataanguka pamoja na wenzao watakaoanguka siku hiyo, nitakapowapatiliza; ndipo, watakapojikwaa; ndivyo, Bwana anavyosema.
13Ndivyo, asemavyo Bwana: Ninapotaka kuchuma kwao, mizabibu, haina zabibu, wala mikuyu haina kuyu, nayo majani yao inakuwa inanyauka; kwa hiyo nitatoa watu, wawaondoe.
14Mbona sisi tunajikalia? Na tukusanyike, tuingie katika miji yenye maboma, tukaangamie humo! Kwani Bwana Mungu wetu atatuangamiza na kutunywesha maji yenye sumu, kwa kuwa tumemkosea Bwana.[#Yer. 9:15.]
15Mbona tunangojea utengemano? Lakini hakuna chema! Mbona tunangojea siku za kupona? Lakini tunayoyaona ni mastuko.[#Yer. 14:19.]
16Upande wa Dani kunasikilika, farasi wao wanavyofoka, kwa uvumi wa makelele yao walio wenye nguvu nchi hii yote inatetemeka; watakuja, wataila nchi nayo yote yaliyomo, miji pamoja nao wakaaamo.
17Angalieni! Nitatuma kwenu nyoka za pili wasiowezekana kwa uganga wo wote, wawaume ninyi; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Mbiu. 10:11.]
18Napata wapi utulivu wa roho katika masikitiko? Moyo wangu umeugua humu ndani.[#Yer. 4:19.]
19Nikiangalia ninasikia sauti za vilio vyao walio wazaliwa wa ukoo wangu, zikitoka katika nchi ya mbali kwamba: Je? Bwana hayumo naye? Sioni wala mfalme wake hayumo naye? Kwa sababu gani wamenisikitisha na vinyago vyao na mambo mageni yasiyo maana?
20Mavuno yamepita, kiangazi kimekwisha, lakini sisi hatukuokolewa.
21Kwa mavunjiko yao walio wazaliwa wa ukoo wangu nami nimevunjika, nikaomboleza, ushangao ukanishika kwa nguvu.
22Je? Haiko miti yenye dawa huko Gileadi? Wala hakuna mponya huko? Mbona wazaliwa wa ukoo wangu hawakupata kuponywa?[#Yer. 46:11.]