Yeremia 9

Yeremia 9

1Nataka sana, kichwa changu kingegeuka kuwa maji, nayo macho yangu yangegeuka kuwa kisima cha machozi, nipate kuwalilia mchana na usiku wazaliwa wa ukoo wangu waliouawa![#Yer. 13:17; Omb. 1:16.]

Kuulilia ubaya wa Wayuda.

2Nataka sana, ningepata nyikani fikio la wasafiri, ningewaacha wao walio ukoo wangu na kutoka kwao, kwani wao wote ndio wagoni, ni chama cha wadanganyi.

3Huzikaza ndimi zao kuwa pindi za kupiga maneno ya uwongo; wamepata nguvu katika nchi, lakini si kwa welekevu, kwani wakitoka pabaya huingia pabaya pengine, lakini mimi hawanijui; ndivyo, asemavyo Bwana.

4Jilindeni kila mtu kwa ajili ya mwenziwe! Hata ndugu na ndugu msiegemeane! Kwani kila ndugu humponza ndugu yake, hata kila rafiki hufuata masingizio.[#Mika 7:5-6.]

5Kila mmoja humwongopea mwenziwe, lakini neno la kweli hawalisemi, wakazifunza ndimi zao kusema uwongo, hupotoa, mpaka wachoke.

6Unakaa kwenye madanganyifu katikati, nami kwa udanganyifu wamekataa kunijua; ndivyo, asemavyo Bwana.

7Kwa hiyo Bwana Mwenye vikosi anasema hivi: Kweli wataniona, nikiwayeyusha na kuwajaribu. Kwani nifanye mengine gani nikiwatazama wazaliwa wa ukoo wangu?

8Ndimi zao ni mishale ya kuchoma na kuua, husema madanganyifu: kwa vinywa vyao husema matengemano na wenzao, lakini mioyoni huviziana.

9Mambo kama hayo nisiyapatilize kwao? watu walio hivyo Roho yangu isiwalipize? ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yer. 5:9.]

10Milima nitaililia na kuiombolezea, nazo mbuga za nyikani nitazitungia wimbo wa kilio, kwani ziko peke yao, hakuna mtu apitaye hapo, hapasikiliki tena sauti za ng'ombe, hata ndege wa angani pamoja na nyama wa porini wamekimbia kwenda zao.[#Yer. 4:25; 12:4.]

11Hata Yerusalemu nitaugeuza kuwa machungu ya mawe tu, panapokaa mbwa wa mwitu, nayo miji ya Yuda nitaigeuza kuwa peke yao, isikae watu.[#Yer. 26:18.]

12Yuko nani aliye mwerevu wa kweli, ayatambue haya? Yuko nani, ambaye kinywa cha Bwana kilisema naye, ayatangaze, kama ni kwa sababu gani, nchi hii ikiangamia, iwe peke yake, pasipite mtu?[#5 Mose 32:29.]

13Bwana akasema: Kwa sababu wameyaacha Maonyo yangu, niliyowapa, wayaangalie, wakakataa kuisikia sauti yangu, hawakuifuata.

14Ila wameufuata ushupavu wa mioyo yao, wakayafuata Mabaali, kama baba zao walivyowafundisha.[#Yer. 7:24.]

15Kwa hiyo Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anasema hivi: Wataniona kweli, nikiwalisha majani machungu na kuwanywesha maji yenye sumu.[#Yer. 23:15.]

16Nitawatawanya kwenye wamizimu, wasiowajua hawa wala baba zao, tena nitatuma panga nyuma yao, mpaka niwamalize.[#3 Mose 26:33.]

17Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Yatambueni! Waiteni wanawake waombolezaji, waje! Tumeni nako kwao wanawake walio werevu wa kweli, waje!

18Waje upesi kutuombolezea, macho yetu yachuruzike machozi, nazo kope zetu zitiririke maji!

19Sauti za maombolezo zinasikilika upande wa Sioni kwamba: Tumetekwa namna gani na kutwezwa kabisa? Hatuna budi kuiacha nchi yetu, kwani makao yetu wameyabwaga chini.

20Sasa ninyi wanawake, lisikieni neno la Bwana, masikio yenu yalipokee neno la kinywa chake! Wafundisheni wana wenu wa kike kuomboleza, kila mwanamke mmoja amfundishe mwenziwe kulilia kufa kwamba:

21Kifo kimepanda madirishani mwetu, kimeingia majumbani mwetu, kiwapokonye watoto barabarani mwa mji, nao wavulana viwanjani!

22Sema: Ndivyo, asemavyo Bwana: Mizoga ya watu itaanguka shambani kuwa kama vinyesi au kama miganda inavyoanguka chini nyuma ya mvunaji, lakini hakuna mwenye kuiokota.[#Yer. 7:33.]

23*Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mwerevu wa kweli asijivunie werevu wake! Wala mwenye nguvu asijivunie nguvu zake! Wala mwenye mali asijivunie mali zake!

24Ila mwenye kujivuna na ajivunie kuwa mtambuzi wa kunijua mimi, ya kuwa mimi Bwana ndiye afanyaye upole na maamuzi yaongokayo katika nchi hii! Kwani hayo ndiyo yanipendezayo; ndivyo, asemavyo Bwana.*[#1 Kor. 1:31; 2 Kor. 10:17.]

25Ndivyo, asemavyo Bwana: Tazameni! Siku zinakuja, nitakapowapatiliza wote waliotahiriwa kwa kuwa tena kama watu wasiotahiriwa,

26akina Wamisri na Wayuda na Waedomu nao wana wa Amoni na Wamoabu nao wote wakatao nywele za panjani wakaao nyikani; kwani wamizimu wote ni watu wasiotahiriwa miilini, lakini wote walio wa mlango wa Isiraeli ni wenye mioyo isiyotahiriwa.[#3 Mose 19:27; 5 Mose 30:6; Yer. 4:4.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania