Yohana 3

Yohana 3

Nikodemo.

1*Kulikuwa na mtu wa Mafariseo, jina lake Nikodemo, aliyekuwa mkuu wa Wayuda.[#Yoh. 7:50; 19:39.]

2Huyo akamjia na usiku, akamwambia: Mfunzi mkuu, tunajua, ya kuwa wewe u mfunzi aliyetoka kwa Mungu, kwani hakuna mtu anayeweza kuvifanya vielekezo hivyo, unavyovifanya wewe, Mungu asipokuwa naye.

3Yesu akajibu, akamwambia: Kweli kweli nakuambia: Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.[#1 Petr. 1:23.]

4Nikodemo akamwambia: Mtu atawezaje kuzaliwa akiisha kuwa mzee? Ataweza kuingia tena tumboni mwa mama yake, apate kuzaliwa?

5Yesu akajibu: Kweli kweli nakuambia: Mtu asipozaliwa majini na Rohoni, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu;[#Ez. 36:25-27; Mat. 3:11; Ef. 5:26; Tit. 3:5.]

6kilichozaliwa na mwili ni mwili, nacho kilichozaliwa na Roho ni roho.[#Yoh. 1:13; 1 Mose 5:3; Sh. 51:7; Rom. 8:5-9.]

7Usistaajabu, nikikuambia: Sharti mzaliwe mara ya pili!

8Upepo huvuma, upendako, nawe huusikia uvumi wake, lakini hujui, uanziako wala ukomeako. Hivyo ndivyo, kila aliyezaliwa Rohoni alivyo.

9Nikodemo alipojibu na kumwuliza: Haya yawezekanaje kuwapo?

10Yesu akajibu, akamwambia: Je? Wewe u mfunzi wa Isiraeli, tena haya huyatambui?

11Kweli kweli nakuambia: Sisi huyasema, tuyajuayo; huyashuhudia, tuliyoyaona, lakini hamwupokei ushuhuda wetu![#Yoh. 7:16; 8:26,28.]

12Msiponitegemea, nikiwaambia mambo ya ulimwenguni, mtanitegemeaje, nikiwaambia mambo ya mbinguni?

13Tena hakuna aliyepaa mbinguni, asipokuwa Mwana wa mtu aliyeshuka toka mbinguni.[#Ef. 4:9.]

14Kama Mose alivyokweza nyoka jangwani, vivyo hivyo hata Mwana wa mtu sharti akwezwe,[#4 Mose 21:8-9.]

15kila amtegemeaye apate uzima wa kale na kale.*

16*Kwani kwa hivyo, Mungu alivyoupenda ulimwengu, alimtoa Mwana wake wa pekee, kila amtegemeaye asiangamie, ila apate uzima wa kale na kale.[#Rom. 5:8; 8:32; 1 Yoh. 4:9.]

17Kwani Mungu hakumtuma Mwana wake ulimwenguni, auhukumu ulimwengu, ila ulimwengu upate kuokolewa naye.[#Yoh. 12:47.]

18Amtegemeaye hahukumiwi; asiyemtegemea amekwisha kuhukumiwa, kwani hakulitegemea Jina la Mwana wa Pekee wa Mungu[#Yoh. 3:36; 5:24.]

19Nayo hukumu ndiyo hii: mwanga ulikuja ulimwenguni, lakini watu waliipenda giza kuliko mwanga, kwa sababu matendo yao yalikuwa mabaya,[#Yoh. 1:5,9-11.]

20kwani kila mwenye kutenda maovu huuchukia mwanga, haji mwangani, matendo yake yasipatilizwe;[#Ef. 5:13.]

21lakini mwenye kuyafanya yaliyo ya kweli huja mwangani, matendo yake yaonekane, ya kuwa yametendeka katika Mungu.*

Yesu na Yohana.

22Kisha Yesu na wanafunzi wake wakaenda katika nchi ya Yudea, akashinda kule pamoja nao akibatiza.[#Yoh. 4:1-2.]

23Lakini Yohana alikuwa akibatizia Enoni karibu ya Salemu, kwani kule kulikuwa na maji mengi, tena ndiko, watu walikomwendea, wakabatizwa naye,

24maana Yohana alikuwa hajatiwa bado kifungoni.[#Mat. 14:3.]

25Ikawa, wanafunzi wa Yohana walipobishana na Myuda kwa sababu ya maosho,

26wakaja kwa Yohana, wakamwambia: Mfunzi mkuu, aliyekuwa pamoja na wewe kule ng'ambo ya Yordani, yule uliyemshuhudia wewe, tazama, huyo anabatiza, watu wote wakimwendea.[#Yoh. 1:26-34; 4:1-2.]

27Yohana akajibu, akasema: Hakuna, mtu awezacho kukitwaa, asichopewa toka mbinguni.[#Ebr. 5:4.]

28Ninyi wenyewe mwanishuhudia, ya kuwa nalisema: Mimi siye Kristo ila nimetumwa, nimtangulie yeye.[#Yoh. 1:20,23,27.]

29Aliye mwenye mchumba ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi anayesimama na kumsikiliza hufurahi sana kwa kuisikia sauti yake bwana arusi; basi, hiyo furaha yangu imetimia.[#Mat. 9:15; 22:2.]

30Yeye sharti akue, nami sharti nipunguke.

31Anayekuja toka juu ni mkuu kuliko wote; aliyetoka chini ni wa nchini, husema yaliyo ya nchini; anayekuja toka mbinguni ni mkuu kuliko wote.[#Yoh. 8:23.]

32Aliyoyaona nayo aliyoyasikia, ndiyo, anayoyashuhudia, lakini hakuna anayeupokea ushuhuda wake.[#Yoh. 3:11.]

33Aupokeaye ushuhuda wake huyu anamtambulisha Mungu waziwazi, kuwa ni wa kweli;[#1 Yoh. 5:10.]

34kwani aliyetumwa na Mungu huyasema maneno yake Mungu, naye Mungu haigawii Roho kwa kuipima.[#Yoh. 1:33-34.]

35Baba humpenda Mwana, akampa yote mkononi mwake.[#Yoh. 5:20; Mat. 11:27.]

36Amtegemeaye Mwana anao uzima wa kale na kale, lakini asiyemtii Mwana hataona uzima, ila makali ya Mungu humkalia.[#Yoh. 3:18.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania