The chat will start when you send the first message.
1Alipokuwa akitambea akaona amtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa.[#Luk. 13:2.]
2Wanafunzi wakamwuliza wakisema: Mfunzi mkuu, aliyekosa ni nani? Huyu au wazazi wake, akizaliwa kipofu?
3Yesu akajibu: Hawakukosa wala huyu wala wazazi wake, ila alizaliwa hivyo, kazi ya Mungu ionekane kwake.[#Yoh. 11:4.]
4Sisi sharti tuzifanye kazi zake aliyenituma, mchana ukingali upo. Usiku unakuja, pasipowezekana kufanya kazi.[#Yoh. 5:17.]
5Nikingali ulimwenguni, mimi ndio mwanga wa ulimwengu.[#Yoh. 8:12.]
6Alipokwisha kuyasema haya akatena mate chini, akayavuruga hayo mate kuwa kitope, nacho kitope akampaka machoni,[#Mar. 8:23.]
7akamwambia: Nenda, unawe katika ziwa la Siloa, ni kwamba: Aliyetumwa. Basi, akaenda, akanawa, akarudi mwenye kuona.[#Yes. 8:6.]
8Majirani zake nao waliomwona siku zote, alivyokaa na kuombaomba, wakasema: Huyu siye aliyekuwa amekaa na kuombaomba?
9Wengine wakasema: Ndiye; wengine wakasema: Siye, wamefanana tu; yeye akasema: Mimi ndiye.
10Basi, wakamwuliza: Macho yako yamefumbukaje?
11Akajibu: Yule mtu anayeitwa Yesu alivuruga kitope, akanipaka machoni, akaniambia: Uende penye ziwa la Siloa, unawe! Nikaenda, nikanawa, nikapata kuona.
12Walipomwuliza: Yuko wapi huyo? akasema: Sijui.
13Wakampeleka kwa Mafariseo yule aliyekuwa ni kipofu.
14Lakini siku, Yesu alipokivuruga kitope na kumfumbua macho yake, ilikuwa ya mapumziko.[#Yoh. 5:9.]
15Mafariseo walipomwuliza tena, alivyopata kuona, akawaambia: Alinipaka kitope machoni, nikanawa, ndio naona.
16Kwao Mafariseo walikuwako waliosema: Mtu huyo hakutoka kwa Mungu, kwani haishiki miiko ya siku ya mapumziko. Wengine waliposema: Mtu mkosaji awezaje kuvifanya vielekezo kama hivyo? wakakosana wao kwa wao.[#Yoh. 7:43; 9:31,33.]
17Kwa hiyo wakamwambia kipofu tena: Wewe unamwona kuwa nani, kwa sababu alikufumbua macho? Naye akasema: Ni mfumbuaji.
18Basi, Wayuda hawakulisadiki neno lake, ya kuwa alikuwa ni kipofu, akapata kuona, mpaka walipowaita wazazi wake yeye aliyepata kuona;
19wakawauliza: Huyu ndiye mwana wenu, mnayemsema: Alizaliwa kipofu? Sasa amepataje kuona?
20Wazazi wake wakajibu, wakasema: Twajua, huyu ni mwana wetu, naye alizaliwa kipofu;
21lakini hatujui, jinsi alivyopata kuona sasa, wala hatumjui sisi aliyemfumbua macho. Mwulizeni mwenyewe! Ni mtu mzima; atajisemea mwenyewe.
22Wazazi wake walisema hivyo kwa kuwaogopa Wayuda, kwani Wayuda walikuwa wamekula njama ya kwamba: Mtu atakayemwungama, kuwa ni Kristo, akatazwe kuiingia nyumba ya kuombea.[#Yoh. 7:13; 12:42.]
23Kwa hiyo wazazi wake walisema: Ni mtu mzima, mwulizeni mwenyewe!
24*Kisha wakamwita mara ya pili yule mtu aliyekuwa ni kipofu, wakamwambia: Mtukuze Mungu! Sisi twajua: Mtu huyo ni mkosaji.[#Yos. 7:19.]
25Yule akajibu: Kama ni mkosaji, sijui; ninalolijua, ni hili moja: Mimi niliyekuwa kipofu naona sasa.
26Walipomwuliza: Amekufanyia nini? Amekufumbua macho jinsi gani?
27akawajibu: Nimekwisha kuwaambia; nanyi hamkusikia. Mnatakaje kuvisikia tena? Au nanyi mnataka kuwa wanafunzi wake?
28Wakamtukana, wakasema: Wewe ndiwe mwanafunzi wake yule, lakini sisi tu wanafunzi wake Mose.
29Sisi tunajua, ya kuwa Mungu alisema na Mose, lakini huyo hatumjui, alikotoka.
30Yule mtu akajibu, akawaambia: Neno hili ni la kustaajabu, ya kuwa ninyi hamjui, alikotoka, naye amenifumbua macho!
31Twajua, ya kuwa Mungu hasikii wakosaji; ila mtu akimwogopa Mungu na kuyafanya, ayatakayo, basi, huyo humsikia.[#Fano. 15:29; Yes. 1:15.]
32Tangu hapo kale haijasikiwa, ya kuwa mtu aliyafumbua macho ya mtu aliyezaliwa kipofu.
33Huyo kama angekuwa hakutoka kwa Mungu, asingeweza kufanya kitu.[#Yoh. 9:16.]
34Wakajibu, wakamwambia: Wewe uliyezaliwa wote mzima mwenye makosa, unatufundisha sisi? Wakamfukuza, atoke.[#Yoh. 9:2.]
35Kisha Yesu akasikia, ya kuwa wamemfukuza, atoke; alipomwona akasema: Unamtegemea Mwana wa mtu?
36Yule akajibu, akasema: Ni yupi, Bwana, nipate kumtegemea?
37Yesu akamwambia: Umekwisha kumwona, naye anayesema na wewe ndiye.[#Yoh. 4:26.]
38Ndipo, aliposema: Nakutegemea, Bwana! Akamwangukia.
39Kisha Yesu akasema: Nimekuja katika ulimwengu huu, niuhukumu, wasioona wapate kuona nao waonao wapate kupofuka.[#Mat. 13:11-15.]
40Wengine wao Mafariseo waliokuwa pamoja naye walipoyasikia haya wakamwambia: Je? Nasi tu vipofu?[#Mat. 15:14; 23:26.]
41Yesu akawaambia: Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa wenye makosa. Lakini sasa mkisema: Twaona, basi, makosa yenu yanawakalia.*[#Fano. 26:12.]