Iyobu 1

Iyobu 1

Mali za Iyobu amchaye Mungu.

1Kulikuwa na mtu katika nchi ya usi, jina lake Iyobu. Mtu huyu alikuwa mnyofu wa kweli mwenye kumcha Mungu, nayo mabaya alikuwa ameyaepuka.[#1 Mose 10:23; 22:21; 36:28; Yer. 25:20; Omb. 4:21; Ez. 14:14,20.]

2Kwake walizaliwa wana saba wa kiume na watatu wa kike.

3Makundi yake yalikuwa mbuzi na kondoo pamoja 7000 na ngamia 3000 na majozi ya ng'ombe 500 na punda majike 500, hata watumwa wake wakawa wengi sana. Kwa hiyo yule mtu alikuwa mkuu kuliko watu wote waliokaa upande wa maawioni kwa jua.

4Wanawe wa kiume walifanya nyumbani mwake kila mmoja sikukuu yake; ndipo, walipowaalika maumbu zao watatu kula na kunywa pamoja nao.

5Ikawa, kila walipozila hizo sikukuu zao, Iyobu hutuma kwao, akawatakasa kesho yake asubuhi akiwatolea ng'ombe za tambiko, wao wote kila mtu yake, kwani Iyobu alisema: Labda wanangu wamekosa wakiacha kumcha Mungu mioyoni mwao. Hivyo ndivyo, Iyobu alivyovifanya siku zote.

Uvumilivu wa Iyobu katika majaribu makuu.

6Ikawa siku moja, wana wa Mungu walipokuja kumtokea Bwana, Satani naye akaja katikati yao.[#Iy. 2:11; 1 Fal. 22:19-22; 1 Mambo 21:1; Zak. 3:1.]

7Bwana akamwuliza Satani: Umetoka wapi? Satani akamjibu Bwana akisema: Natoka katika kutembea katika nchi na kujiendea huko na huko.

8Bwana akamwuliza Satani: Umemwangalia mtumishi wangu Iyobu? Kwani katika nchi hakuna mtu kama yeye, ni mnyofu wa kweli mwenye kumcha Mungu, nayo mabaya ameyaepuka.[#Iy. 1:1.]

9Satani akamjibu Bwana akisema: Je? Iyobu anamcha Mungu bure?[#Sh. 73:13.]

10Wewe humwangalii mwenyewe na nyumba yake nayo yote yaliyo yake po pote? Ukazibariki kazi za mikono yake, nayo makundi yake yameieneza nchi.

11Haya! Ukunjue mkono wako, uyapige yote yaliyo yake! Ndipo, atakapokutukana usoni pako.

12Bwana akamwambia Satani: Tazama, yote yaliyo yake nakupa! Ila yeye mwenyewe tu usimguse kwa mkono wako! Ndipo, Satani alipotoka usoni pake Bwana.

13Ikawa siku moja, wanawe wa kiume na wa kike walipokula sikukuu na kunywa nvinyo nyumbani mwa ndugu yao aliyezaliwa wa kwanza,

14mjumbe akaja kwake Iyobu, akamwambia: Ng'ombe walipokuwa wanalima, nao punda walipolisha kando yao,

15mara watu wa Saba wakatushambulia, wakawachukua, nao vijana wakawapiga kwa ukali wa panga zao, mimi nikapona peke yangu tu, nikupashe habari.[#1 Mose 10:7,28; 25:3.]

16Huyu angali akisema, akaja mwingine, akasema: Moto wa Mungu umeanguka toka mbinguni, ukawaka kwenye mbuzi na kondoo, ukawala pamoja na vijana, mimi nikapona peke yangu tu, nikupashe habari.

17Huyu angali akisema, akaja mwingine, akasema: Wakasidi wamekuja vikosi vitatu, wakatushambulia, wakawakamata ngamia, wakawachukua, nao vijana wakawapiga kwa ukali wa panga zao, mimi nikapona peke yangu tu, nikupashe habari.[#1 Mose 11:28.]

18Huyu angali akisema, akaja mwingine, akasema: Wanao wa kiume na wa kike walipokula sikukuu na kunywa nvinyo nyumbani mwa ndugu yao aliyezaliwa wa kwanza,

19mara upepo mkubwa uliotoka upande wa nyika ukazipiga pembe zote nne za ile nyumba, ikawaangukia wale vijana, wakafa; mimi nikapona peke yangu tu, nikupashe habari.

20Ndipo, Iyobu alipoinuka, akazirarua nguo zake, akajinyoa kichwa chake, akajitupa chini kumwangukia Mungu,[#1 Mose 37:34.]

21akasema: Nilipotoka tumboni mwa mama nilikuwa mwenye uchi, tena nitakapotoka huku nitakuwa mwenye uchi vilevile. Bwana ndiye aliyenipa, Bwana ndiye aliyeyachukua tena, Jina la Bwana na litukuzwe![#Mbiu. 5:15; 1 Tim. 6:7.]

22Katika mambo hayo yote Iyobu hakukosa, wala hakumwazia Mungu kuwa mwenye mambo yasiyopasa.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania