Iyobu 17

Iyobu 17

Kingojeo chake Iyobu ni kufa tu.

1Roho yangu imenyongeka, siku zangu zinataka kuzimika, ni penye makaburi tu panaponingoja.

2Lakini na sasa yako masimango, wanayonitolea, nami sina budi kutazama tu kwa macho yangu, wakinitia uchungu.

3Nakuomba, jitoe mwenyewe kuniwia kole, kwani yuko wapi mwingine atakayepeana mikono na mimi?[#Iy. 16:19.]

4Kwa kuwa umeuficha ubingwa, usije mioyoni mwao, kwa hiyo hutawaacha tu, wajikuze wenyewe.

5Mtu akiwaalika wenziwe kugawanyiana fungu lake mwingine, ndipo, yatakapozimia macho yao wanawe huyo mtu.

6Aliyemweka kuwa fumbo la watu, ni mimi, mtu wa kutemewa mate usoni nitakuwa mimi.[#Iy. 30:9.]

7Kwa hiyo macho yangu yameingiwa kiwi kwa majonzi, navyo viungo vyangu vyote pia viko kama kivuli.[#Sh. 6:8.]

8Wanyokao wanayastuka sana mambo hayo, nao watakatao wanachafuka sana kwa ajili yao wambezao Mungu.

9Lakini mwenye kuishika njia yake ni mwongofu, naye mwenye mikono iliyo safi huongezeka nguvu.

10Lakini ninyi nyote rudini, mje kwangu, ingawa nisione aliye mwerevu wa kweli miongoni mwenu.

11Siku zangu zimekwisha kupita, mawazo yangu nayo yamekwisha kukatika, tena ndiyo yaliyokuwa mapato ya moyo wangu.

12Ingawa waugeuze usiku kuwa mchana, na kuniambia: Mwanga uko karibu kwako kuliko giza,

13nakungojea kuzimu tu kuwa nyumba yangu, nukitandikie malalo yangu kwenye giza.

14Kaburi sina budi kuliita: baba yangu ni wewe, navyo vidudu: mama yangu na maumbu zangu.[#Iy. 4:19.]

15Kwa hiyo kingojeo changu kingine kiko wapi? kilicho kingojeo changu, yuko nani atakayekichungulia?

16Nacho kitashuka kufika penye makomeo ya kuzimu; ndiko, tutakakotulia pamoja uvumbini.

Bildadi anasema mara ya pili: wasiomcha Mungu huangamia.

Bildadi wa Sua akajibu akisema:

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania