The chat will start when you send the first message.
1Sikieni na kulisikiliza neno langu!
2Hili litakuwa la kuituliza mioyo yenu.
3Niacheni, nipate kusema mimi nami! Nitakapokwisha kuyasema yangu, na msimange tena.
4Je? Yuko mtu, ninayemsuta? Mbona sishindwi na kuvumilia?
5Nigeukieni mimi, mpate kustuka na kuiweka mikono vinywani mwenu!
6Kweli nami nikiyakumbuka nashikwa na woga, mwili wangu nao unakufa ganzi.
7Mbona wasiomcha Mungu huwapo? Mbona huwa wazee, nguvu zao zikiendelea kuongezeka?[#Sh. 37:4-12; Yer. 12:1.]
8Vizazi vyao huviona kwao kwa macho yao kuwa vyenye nguvu, nao wajukuu wao wako machoni pao.
9Nyumba zao hukaa salama pasipo kustushwa, nayo fimbo ya Mungu haiwapigi.
10Ng'ombe wao waume huzaza vema pasipo kukosa, ng'ombe wao wake huzaa vizuri pasipo kuharibu mimba.
11Huwatembeza watoto wao walio wengi kama kundi la kondoo, nao vijana wao huchezacheza na kupaza sauti
12wakiimbia patu na mazeze na kuifurahia milio ya mazomari.
13Siku zao huzitumia za kula mema, kisha hushuka kuzimuni kwa mara moja.
14Nao humwambia Mungu: Ondoka kwetu! hatupendezwi kuzijua njia zako.[#Iy. 22:17.]
15Mwenyezi ni nani, tumtumikie? Inatufaliaje kumtokea na kumwomba?
16Lakini tazameni: mema yao hawayashiki mikononi mwao, kwa hiyo mashauri yao wasiomcha Mungu na yanikalie mbali![#Iy. 22:18.]
17Taa zao wasiomcha Mungu zikizima, ni mara ngapi? Si kila mara, unapowajia mwangamizo wao? Ni mara ngapi, Mungu akiwapatia matanzi kwa kuwakasirikia,[#Iy. 18:5,12.]
18wawe kama bua kavu penye upepo au kama makapi, yakipokonywa na upepo wa chamchela?[#Sh. 1:4.]
19Mwasema: Mungu huwawekea watoto wao maovu yao; lakini angewalipisha wenyewe, wapate kumjua,[#Iy. 20:10; 2 Mose 20:5.]
20macho yao wenyewe yangeuona mwangamizo wao, wakinyweshwa makali yake Mwenyezi yaliyo yenye moto.
21Kwani mlango wao unawezaje kuwapendeza huko nyuma yao, miezi yao ikiisha kukatwa kwa kuitimiza hesabu yao?
22Je? Wanataka kumfundisha Mungu, apate kuwajua? Naye ndiye awahukumuye nao walioko huko juu.[#Mbiu. 5:8.]
23Huwa hivi: mmoja anakufa mwenye nguvu zake zote, naye alikuwa anatengemana na kutulia kabisa,
24vyombo vyake vya kukamulia vikijaa maziwa, kiini cha mifupa yake nacho kikiwa chenye mafuta.
25Mwingine anakufa mwenye uchungu rohoni mwake, kwa kuwa hakuna chema cho chote, alichokila.
26Kisha hulala pamoja humo uvumbini, vidudu vikiwafunika wote wawili.[#Iy. 3:13-19.]
27Tazameni! Ninayajua mawazo yenu nayo mashauri yenu ya kunikorofisha.
28Mwasema: Nyumba ya mkuu aliyetesa watu iko wapi? Mahema, wasiomcha Mungu waliomokaa, yako wapi nayo?
29Je? Wapitao njiani hamkuwauliza hayo? Hamzitambui habari zao za mambo, waliyoyaona wao?
30Kwamba: Siku ya msiba mbaya hupona, siku, makali yanapotokea, huepuka.
31Yuko nani anayeziumbua njia zake usoni pake? Tena yuko nani anayemlipisha aliyoyafanya yeye?
32Naye husindikizwa mpaka mazikoni, tena kaburini kwake wanangoja zamu.
33Udongo wa bondeni anauona kuwa mtamu, watu wote wanamfuata nyuma yake, nao waliomtangulia hawahesabiki.
34Nanyi mnaniambiaje matulizo ya moyo yaliyo ya bure? Kwani yanayosalia ya majibu yenu, ni ukatavu tu.
Elifazi wa Temani akajibu akisema: