The chat will start when you send the first message.
1Fedha zina mahali pao zinapoonekana, nazo dhahabu zina mahali pao, wanapozifulia mitoni.
2Vyuma vinachimbuliwa uvumbini, tena yako mawe yanayotokea shaba kwa kuyeyushwa.
3Nalo giza mtu analikatia mpaka, ayachunguze mawe yaliyoko kule kuliko na giza lenyewe kwenye mlango wa kuzimu.
4Huko anachimbua shimo refu sana, kisha nayo njia ya ndani ya nchi pasipokaa watu; wanawahauliwa kwa kuwa chini ya hapo, watu wanapokanyaga; ndiko, wanakojiangika na kuning'inia, watu wengine wakiwa mbali.
5Nchi itoayo chakula juu chini yake inafudikizwa kwa kuchimbuliwa na nguvu zilizo sawa nazo za moto.
6Mahali pamojamoja huonekana mawe yenye almasi, pengine nayo madongo yenye dhahabu.
7Naye tai haijui njia hiyo, wala macho ya kozi hayajaiona kwa kuchungulia.
8Nyama wakali wenye majivuno hawajaikanyaga, wala simba mwenyewe hajaishika.
9Nayo mawe magumu yenyewe mtu huyavunja kwa mkono wake, hata milima anaifudikiza kwa kuichimbua toka misingini.
10Miambani anachonga njia za kupitia ndani yao; ndivyo, macho yake yanavyoona yote yaliyo yenye kima.
11Vijito vya ndani anaviziba, visimchuruzikie maji, apate kuyatokeza mwangani yaliyofichika ndani ya nchi.[#Iy. 28:25.]
12Lakini werevu wa kweli unaonekana wapi? napo mahali penye utambuzi pako wapi?
13Hakuna mtu ajuaye, unapotengenezwa, hauonekani katika nchi yao wenye uzima.
14Vilindi husema: Kwetu sisi hauko, nayo bahari husema: mimi nami sinao.
15Hata kwa dhahabu safi haupatikani, wala haulipiki kwa fedha kuwa bei yake,[#Fano. 3:14-15; 8:10-11.]
16wala haupimiki kwa dhahabu tupu ile ya Ofiri, wala kwa almasi au kwa vito vya sardio vilivyo vyenye kima.[#1 Fal. 9:28.]
17Wala dhahabu wala vioo vizuri mno ndivyo vinavyolingana nao, wala haununuliki kwa vyombo vya dhahabu vyenye urembo.
18Marijani na ulanga uangazikao vizuri hayakumbukwi uliko, kuwa na werevu wa kweli ni mali kuliko lulu.
19Hauwezekani kulinganishwa navyo vito vya topasio vitokavyo Nubi, wala haupimiki kwa dhahabu itakatayo kabisa.[#2 Mose 28:17.]
20Je? Werevu wa kweli unatoka wapi? napo mahali penye utambuzi pako wapi?
21Umefichika machoni pao wote walio wenye uzima, nao ndege wa angani hawauoni, kwa kuwa uko umefunikwa.
22Kuzimu nacho kifo husema: Kwa masikio yetu tulisikia tu, ukitajwa.
23Mungu anaitambua njia ya kwenda kwake, yeye tu anapajua, hapo pake ulipo.[#Fano. 8:22-31.]
24Kwani yeye huchungulia hata mapeoni kwa nchi, huyaona yaliyoko chini ya mbingu.
25Alipoutengeneza ukali wa upepo, alipoupima wingi wa maji,[#Iy. 26:10.]
26alipoyatengeneza maongozi ya mvua nayo njia ya umeme ulio wenye ngurumo:
27hapo ndipo, alipouona, kisha akautangaza kwa watu, akaushikiza, akauchunguza.
28Kisha akawaambia watu: Tazameni! Kumcha Bwana ndio werevu wa kweli, kuyaepuka mabaya ndio utambuzi.[#Sh. 111:10; Fano. 1:7.]
Iyobu akaendelea kutoa mifano akisema: