Iyobu 29

Iyobu 29

1Laiti ningekuwa, kama nilivyokuwa katika miezi iliyopita,

2Mungu alipoziangalia siku zangu!

3Hapo taa yake ilimulika juu ya kichwa changu, kwa mwanga wake nikaenda hata gizani.[#Sh. 18:29.]

4Siku zile nilikuwa mwenye nguvu za kiume, Mungu naye akakaa hemani mwangu kuwa mwenzangu wa mashauri.[#Sh. 25:14.]

5Hapo Mwenyezi alikuwa pamoja na mimi, nao watoto wangu wakanizunguka.

6Hapo miguu yangu ilioshwa kwa maziwa, nao mwamba uliochuruzika vijito vya mafuta ulikuwa kwangu.

7Nilipotokea langoni kwenye mji, nikiweke kiti changu uwanjani,

8vijana waliponiona wakaondoka kwenda pengine, nao wazee wakainuka, wasimame;

9Wakuu wakayakomesha maneno yao na kuviweka viganja vinywani mwao.

10Sauti za mabwana wakubwa nazo zikanyamaza, ndimi zao zikagandamana na fizi zao.

11Sikio la mtu liliponisikia, akanishangilia, jicho la mtu liliponiona, akanishuhudia.

12Kwani nilimponya mnyonge, aliponililia, hata waliofiwa na wazazi, walipokosa msaidiaji.[#2 Mose 22:21-22; 3 Mose 19:18.]

13Mbaraka yake aliyeufikia mwangamizo ikanijia, nayo mioyo ya wajane nikaichangamsha.

14Nilivaa wongofu, uniwie nguo, nayo maamuzi yangu yakawa kama kanzu na kilemba.

15Kipofu nilikuwa macho yake, kiwete nilikuwa miguu yake.

16Maskini mimi nilikuwa baba yao, nalo shauri la mtu, nisiyemjua, nikalichunguza vema.[#Iy. 31:18.]

17Lakini mpotovu nilimvunja meno, namo mlemle katika meno yake nikayapokonya aliyoyanyang'anya.[#Sh. 58:7.]

18Kwa hiyo nilisema: Katika kiota changu ndimo, nitakamozimia, siku zangu zitakapokuwa nyingi kama za mtende.

19Mizizi yangu itatandama juu penye maji, nao umande utayanyea matawi yangu usiku kucha.

20Utukufu, nilio nao, utakuwa mpya kila siku, nao upindi wangu utajipatia nguvu mpya mkononi mwangu.

21Mimi watu walinisikiliza na kungoja, nimalize; nilipowapa shauri langu, wakaninyamazia.

22Hakuwako mwingine aliyesema, nilipokwisha kusema, maneno yangu yakawa kama matone yaliyowadondokea.

23Kama wanavyongoja mvua, ndivyo, walivyoningoja, vinywa vyao vikaasama kama vyao wanaotwetea mvua ya vuli.

24Walipotaka kukata tamaa, nikawachekea, hawakuweza kuuinamisha chini uso wangu, ulipoangaza.

25Nilipojielekeza kwenda kwao nilikaa nao kama kichwa chao, au kama mfalme katika vikosi vyake kwa kuwa kama mtu anayewatuliza mioyo waliosikitika.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania