The chat will start when you send the first message.
1Sasa wananicheka walio wenye siku chache kuliko mimi, ambao baba zao nilikataa kuwaweka mahali, mbwa wa makundi yangu ya kondoo walipokuwa nao.[#Iy. 29:8-11.]
2Nazo nguvu za mikono yao zingenifalia nini? Kwani uwezo wao wenye nguvu ulikuwa umeangamia.
3Kwa kuwa ukosefu na njaa zilikuwa ziliwagofua, huguguna nayo mazao ya nyika iliyo kama jangwa jeusi, iliyo tupu kabisa pasipo cho chote cha kulisha watu.
4Kwa hiyo huchuma vijanijani vyenye chumvi panapo na vichakachaka, nayo mizizi ya mifagio ni chakula chao.
5Hufukuzwa penye watu wengine, wakiwazomea kama wezi.
6Hawana budi kukaa katika makorongo yaogopeshayo, hata mashimoni ndani ya nchi, hata miambani.
7Hulia kwa njaa vichakani wakilala chini ya upupu.
8Ndio wenye upumbavu wenyewe wasiojua hata majina yao, nako kwao walifukuzwa na kupigwa.
9Sasa nimegeuka kuwa mtu wao hao wa kumzomea, nikapata kuwa kwao kama fumbo.[#Iy. 17:6; Sh. 69:13; Omb. 3:63.]
10Kwa kutapishwa na mimi huwa mbali, wasinifikie karibu, lakini hawajikatazi kunitemea mate usoni pangu.[#Mat. 26:67.]
11Vilivyowazuia wakavifungua, wanitese, usoni pangu wakavitupa mbali hivyo vifungo vyao.
12Hawa watu waovu hujisimamisha kuumeni kwangu, waisukume miguu yangu, iondoke kwao, nazo njia zao zilizowaangamiza hunitwika mimi.
13Njia yangu wakaichimbua, isipitike, wao wakosao msaidiaji husaidia kunitumbukiza mwangamizoni.
14Kama ni kutokea katika ufa mpana, hunijia mimi, makelele yao huzidi sana kwa kusukumana.
15Mastusho kama hayo yakanigeukia, kama ni kwa nguvu za upepo yakautangua ukuu wangu upesi, nayo yawezayo kuniokoa yakatoweka kama wingu.
16Kwa hiyo roho yangu imeyeyuka sasa ndani yangu, siku za kuteseka zikanipata.[#Sh. 42:5.]
17Usiku unaichoma mifupa yangu huko ndani, mpaka ioze, nayo maumivu yangu yanayoniguguna hayapumziki.
18Hizo nguvu nyingi zikaligeuza vazi langu, zikanikaza kama ukosi wa kanzu yangu.[#Iy. 7:5.]
19Zikanibwaga matopeni, nikafanana nayo mavumbini na majivu.
20Nikikulilia, wewe, hunijibu; hata nikisimama, unanitazama tu.[#Iy. 19:7; Sh. 22:3.]
21Umegeuka kuwa mpingani wangu asiyenihurumia, kwa huo uwezo wa mkono wako ukanifukuza.
22Ukaniinua na kuniweka juu ya upepo, unipeleke, ukaniyeyusha kwa hizo nguvu za chamchela.
23Nakujua, utakakonipeleka, ndiko kufani, uniingize nyumbani mwenye mkutano wao wote waliokuwa uzimani.
24Je? Mtu akitumbukia shimoni hanyoshi mkono? Au mtu akizama hapigi yowe kwa sababu hiyo?
25Aliyepatwa na siku ngumu sikulia naye? Roho yangu haikumsikitikia naye mkiwa?
26Nilipotazamia mema, mabaya yakaja; nilipongojea mwanga, giza ikaja.[#Yer. 14:19.]
27Matumbo yakachafuka, yakakataa kunyamaza, siku za mateso ziliponifikia mimi nami.
28Nikajiendea na msiba wangu pasipo kuona jua, nikaondoka penye mkutano, nipate kulia.
29Nimegeuka kuwa ndugu yao mbwa wa mwitu, na mwenzao mumbi wapigao kite.
30Ngozi yangu inachubuka kwa kuwa nyeusi, itoke mwilini mwangu, nayo mifupa yangu imeungua kwa joto la mwili.
31Hivyo zeze langu limegeuka kuwa la kuombolezea, nalo zomari langu hupiga sauti za vilio tu.[#Sh. 30:12.]