Iyobu 32

Iyobu 32

Elihu anaanza kusema na kuzieleza sababu za kunyamaza kwake.

1Hao watu watatu walipoacha kumjibu Iyobu, kwa kuwa alikuwa mwongofu machoni pake,

2ndipo, makali ya Elihu wa Buzi, mwana wa Barakeli wa mlango wa Ramu, yalipowaka moto, naye Iyobu ndiye, makali yake yaliyemwakia, kwa kuwa alijiwazia rohoni mwake kuwa hakumkosea Mungu.[#1 Mose 22:21; Iy. 9:20; 13:18; 19:6-7; 23:7; 27:2,6; 31:35.]

3Nao wale wenzake watatu makali yake yakawawakia, kwa kuwa hawakuona tena la kumjibu Iyobu la kumwumbua kuwa amekosa.[#Iy. 15:5; 18:21; 20:29; 22:5.]

4Lakini Elihu alikawia kusema na Iyobu, kwani wale walikuwa wakubwa kumpita yeye kwa siku zao.

5Elihu alipoona, ya kuwa hakuna jibu tena litokalo vinywani mwao wale watatu, makali yake yakawaka kama moto.

6Ndipo, Elihu wa Buzi, mwana wa Barakeli, alipojibu, akasema:

Mimi ni mdogo kwa miaka, ninyi m wazee, kwa hiyo nimejizuia, nikaogopa kuwaelezea ninyi, ninayoyajua mimi.

7Nilisema: Wenye uzee na waseme, walio na miaka mingi na waujulishe werevu wa kweli.[#Iy. 12:12.]

8Lakini kinachowapa watu utambuzi ni roho iliyomo mwao pamoja na pumzi yake yeye Mwenyezi.

9Lakini wazee wenye miaka mingi sio wanaoerevuka kweli, wao wazee sio wanaoyajua mashauri yaliyo sawa.

10Kwa hiyo nasema: Nisikilizeni, mimi nami niyaeleze, ninayoyajua!

11Tazameni! Nimeyangojea maneno yenu, nikausikiliza utambuzi wenu, mlipouchunguza, mvumbue, hayo mambo yalivyo.

12Ninyi nimewaangalia sana, hii ni kweli; lakini nilipotazama sikumwona aliyemshinda Iyobu, wala mmoja wenu hakuweza kumjibu aliyoyasema.

13Msiseme: Kwa kuwa ni mwenye werevu wa kweli, tumeona, atakayemshinda ni Mungu, si mtu.

14Hajajiweka tayari kusema na mimi, lakini kama ninyi mlivyosemeana naye, sitamjibu hivyo.

15Ndipo, walipostuka, hawakujibu tena, wakawa wamepotelewa na maneno ya kusema.

16Walipokuwa hawasemi neno, nikangoja, lakini wakasimama tu pasipo kujibu tena.

17Basi, nami na nijibu fungu langu, nami na niyaeleze, ninayoyajua.

18Kwani nimejaa maneno ya kusema, roho yangu humu ndani yangu imesongeka, mpaka niyatoe.

19Tazameni: Tumbo langu linafanana na mvinyo isiyofunguliwa njia, ni kama viriba vipya vinavyotaka kupasuka.

20Na niseme, humu ndani mpanuke kidogo tu, na niifumbue midomo yangu, nijibu nami.

21Sitaki kupendelea uso wa mtu, wala maneno yaliyo mafuta ya midomo tu sitamwambia mtu,

22kwani yaliyo mafuta ya midomo tu sijui kuyasema, muumbaji wangu angeniondoa upesi sana.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania