The chat will start when you send the first message.
1Je? Mgombezaji atabishana naye Mwenyezi?[#Yes. 45:9.]
2Atakayebishana na Mungu na ajibu!
3Ndipo, Iyobu alipomjibu Bwana akisema:
4Mimi ni mdogo zaidi, nikujibu nini? Nimekifumba kinywa changu kwa kiganja changu.
5Nimesema mara moja, lakini sitajibu tena, sitaendelea kusema mara ya pili.
6Bwana akamjibu Iyobu akiwa mle upeponi mwenye nguvu za kuvuma, akasema:
7Haya! Jifunge viuno vyako kama mtu wa kiume! Kisha nitakuuliza, upate kunijulisha![#Iy. 38:3.]
8Je? Mashauri, niliyoyakata, utayatangua wewe? Je? Utaniumbua kuwa mwovu, ujitokeze kuwa mwongofu?
9Je? Uko na mkono kama wake Mungu? Kwa kupaza sauti utaweza kunguruma kama yeye?[#Iy. 37:5.]
10Haya! Jipambe utukufu na ukuu! Jivike urembo na enzi!
11Yamwage machafuko ya ukali wako, mbwage chini kila, utakayemwona, ya kuwa amejivuna!
12Kila utakayemwona, ya kuwa amejivuna, umnyenyekeze! Nao waovu waangushe papo hapo, wanaposimama!
13Wachimbie uvumbini wote pamoja, nazo nyuso zao zifungie gizani hapo, wanapochimbiwa!
14Ndipo, nitakapokutukuza mimi nami kwa kwamba: Mkono wako wa kiume unakuokoa.
15Mtazame kiboko, niliyemwumba, kama nilivyokuumba wewe; naye hula majani kama ng'ombe.
16Zitazame nguvu zake, alizo nazo kiunoni mwake, nao uwezo wake uliomo mishipani mwa tumbo lake.
17Hunyosha mkia wake, uwe kama mwangati, mishipa ya mapaja yake imefungamana.
18Mifupa yake ndio mabomba ya shaba, nazo mbavu zake ndio fimbo za chuma.
19Wa kwanza wa viumbe vya Mungu ndiye yeye, naye aliyemwumba alimgawia nao upanga wake.
20Mapori ya milimani humtolea chakula, nao nyama wote wa porini huchezacheza hapo.
21Hulala chini ya miti yenye kivuli hujificha penye matete mabwawani.
22Ile miti yenye kivuli humfunika kwa kivuli chao, nayo mifuu ya mtoni humzunguka.
23Tazama, ijapo maji ya mto yafurike sana, hastuki kamwe, hutulia, ijapo mto kama Yordani umshambulie kuingia kinywani.
24Yuko nani atakayemkamata, akiwa macho? Au yuko nani atakayeitoboa pua yake, amfunge kwa kamba?