The chat will start when you send the first message.
1Je? Unaweza kumvua nondo wa baharini kwa ndoana au kuufunga ulimi wake kwa kamba katika taya la chini?[#Yes. 27:1.]
2Au utaweza kumtia ugwe puani mwake? Au utaweza kulitoboa shavu lake kwa kulabu?
3Je? Atazidi kukulalamikia? Au atakuambia maneno ya upole?
4Atafanya agano na wewe, umchukue, awe mtumishi wako kale na kale?
5Je? Utamchezesha kama ndege, ukimfunga wa kufurahisha vijana wa kike?
6Chama cha wavuvi kinamchuuzia na kuwagawanyia wachuuzi vipande vipande?
7Je? Utaweza kueneza mikuki ngozini pake au kichwani pake vyusa vya wavuvi?
8Haya! Mpelekee mkono wako, umkamate! Ndipo, utakapolikumbuka pigano hilo, usilirudie tena.
9Tazama! Hicho kingojeo cha kumkamata ni uwongo, ukimtazama tu utakufa ganzi.
10Hakuna ajipaye moyo wa kumwamsha; tena yuko nani atakayesimama usoni pangu, mimi Mungu?
11Yuko nani aliyeanza kunipa kitu, nimlipe? Yote pia yaliyoko chini ya mbingu ni yangu mimi.[#Rom. 11:35.]
12Sitanyamaza, nisiseme, jinsi viungo vyake vilivyo, nazo nguvu zake, jinsi zilivyo kubwa, nayo matengenezo yake, jinsi yalivyo mazuri.
13Yuko nani awezaye kulichuna vazi lake? Yuko nani atiaye mkono katika mataya yake yenye meno mawilimawili?
14Yuko nani awezaye kuifungua milango ya kinywa chake? Kwani pande zote zinayo meno yaogopeshayo.
15Magamba yake ni mazuri mno kwa hivyo, yanavyojipanga: kama ni kukazwa kwa nguvu ya chapa, hugandamana karibukaribu,
16hushikamana kabisa kila moja na mwenzake, upepo tu usiweze kupita katikati yao.
17Kweli kila moja linagandamana na mwenzake, yanashikana kwa nguvu, yasitengeke.
18Akienda chafya humulikisha mwanga, nayo macho yake yanafanana nayo makope ya mapambazuko.
19Mienge ya moto hutoka kinywani mwake, nayo hurukisha macheche ya moto.
20Katika mianzi ya pua yake hutoka moshi kama wa chungu kichemkacho au wa moto wa matete.
21Pumzi yake huunguza kama makaa yenye moto, hata miali ya moto hutoka kinywani mwake.
22Shingoni pake ndipo, nguvu zinapokaa, mbele yake yako matetemeko na mastusho.
23Manofu ya mwili wake yanashupaa, kwa kukazana hapo, yalipo, hayatikisiki.
24Moyo wake nao ni mgumu kama jiwe, ugumu wake ni kama wa jiwe la chini la kusagia.
25Akiinuka, nao wenye nguvu hushikwa na woga, kwa kustushwa hukosa njia ya kukimbilia.
26Ukimpiga kwa upanga haumwingii, wala mkuki wala mshale wala chuma cho chote.
27Chuma hukiwazia kuwa jani kavu, nayo shaba huiwazia kuwa mti uliobunguka.
28Mishale ya upindi haiwezi kumkimbiza, nayo mawe ya kombeo kwake hugeuka kuwa kama makapi.
29Marungu huwaziwa naye kuwa mabua makavu, tena huicheka shindo ya mkuki, ukitupwa.
30Upande wake wa chini una vigae vyenye pembe, alipogaagaa ni kama matopeni, palipopita gari la kupuria.
31Hukichafua nacho kilindi, kiwe kama chungu kinachochemka; huivuruga nayo bahari, iwe kama dawa, zikivurugwa chunguni.
32Nyuma yake hiyo njia, aliyoishika, huangazika, hilo povu la kilindi mtu angeliwazia kuwa mvi.
33Huku nchini hakuna afananaye naye; alichoumbiwa, ni hiki: asistuke kamwe!
34Wote walio wakuu huwatazama tu, kuliko wenye majivuno wote mfalme ndiye yeye.
Iyobu akamjibu Bwana akisema: