The chat will start when you send the first message.
1Neno la Bwana likamjia Yona, mwana wa Amitai, kwamba:[#2 Fal. 14:25.]
2Ondoka, uende katika mji ule mkubwa wa Niniwe, uutangazie, ya kuwa ubaya wao umenitokea hapa juu![#Sh. 139:7,9-10.]
3Lakini Yona akaondoka kumkimbia Bwana, aende Tarsisi, akatelemka kwenda Yafo; ndipo, alipoona merikebu inayokwenda Tarsisi, akawapa nauli yao, akajipakia mle kwenda nao Tarsisi, amkimbie Bwana.
4Ndipo, Bwana alipotuma upepo mkali huko baharini, ukawa kimbunga kikali kule baharini, ile merikebu ikawa karibu ya kuvunjika.
5Mabaharia wakaogopa, wakaililia miungu, kila mtu mungu wake, kisha vyombo vilivyokuwamo merikebuni wakavitupa baharini, merikebu ipate kuwa nyepesi. Lakini Yona alikuwa ameshuka na kuingia chumba cha ndani cha huko chini, akalala usingizi mwingi.
6Mkuu wa merikebu akamjia, akamwambia: Inakuwaje ukijilalia usingizi? Inuka, umlilie Mungu wako! Labda Mungu atatukumbuka, tusiangamie.
7Kisha wote wakaambiana, kila mtu na mwenziwe: Haya! Na tupige kura, tujue, kama ni kwa ajili ya nani, tukipatwa na mabaya haya! Walipopiga kura, ikamwangukia Yona.[#Fano. 16:33.]
8Wakamwambia: Tuelezee, kama ni kwa sababu gani, tukipatwa na mabaya haya! Unafanya kazi gani? Tena ni wapi, ulikotoka? Nchi yako ni ipi? U mtu wa kabila gani wewe?
9Akawaambia: Mimi ni Mwebureo, mimi ninamcha Bwana, Mungu wa mbingu, aliyezifanya bahari na nchi kavu.[#1 Mose 1:9-10.]
10Ndipo, wale waume waliposhikwa na woga mwingi, wakamwuliza: Umefanya nini? Kwani waume wale walikwisha jua, ya kuwa amemkimbia Bwana, kwani aliwasimulia.
11Wakamwuliza: Tukufanyie nini, bahari ipate kutulia mbele yetu? Kwani bahari ilikuwa ikiendelea kuchafuka zaidi.
12Akawaambia: Nichukueni mnitupe baharini! Ndipo, bahari itakapotulia mbele yenu, kwani ninajua, ya kuwa ni kwa ajili yangu mimi, hiki kimbunga kikubwa kikiwatokea ninyi.
13Kisha wale waume wakafanya bidii sana kuvuta makasia, wapeleke merikebu pwani, lakini hawakuweza, kwani bahari ilikuwa ikiendelea kuwachafukia zaidi.
14Ndipo, walipomlilia Bwana kwamba: E Bwana, usiache, tukiangamia kwa ajili ya roho ya mtu huyu! Wala usitutwike damu, tusiyoikosea! Kwani wewe Bwana umefanya, kama ulivyopendezwa.
15Kisha wakamchukua Yona, wakamtupa baharini; ndipo, bahari ilipotulia ikiacha kuchafuka.
16Kwa hiyo wale waume wakamwogopa Bwana, woga mwingi ukawashika, wakamtambikia Bwana na kumtolea ng'ombe ya tambiko pamoja na kumwapia viapo.