Yona 2

Yona 2

Yona anamwomba Bwana, amwokoe.

1Bwana akaagiza samaki mkubwa, aje ammeze Yona, Yona akawamo tumboni mwa samaki huyo siku tatu mchana na usiku.[#Mat. 12:40; 16:4.]

2Mle tumboni mwa huyo samaki Yona akamwomba Bwana Mungu wake

3kwamba:

Nimemlilia Bwana niliposongeka, akaniitikia;

kuzimuni ndani nimemlalamikia, aniokoe,

ndipo, alipoisikia sauti yangu.

4Umenitupa vilindini baharini ndani,

mafuriko ya maji yanizunguke,

mawimbi yako yote na maumuko yako yote yakapita juu yangu.

5Nami nikawaza kwamba: Nimetupwa, nisitokee tena machoni pako,

nitawezaje kuliona tena Jumba lako takatifu?

6Maji yamenizunguka ya kuitosa nayo roho yangu,

vilindi vimenizunguka,

majani ya baharini yamekizinga kichwa changu.

7Nimezama kuifikia misingi ya milima,

makomeo ya nchi yamenifungia kale na kale,

lakini wewe Bwana Mungu wangu umenitoa kuzimuni, niwe mzima.

8Roho yangu ilipokuwa katika kuzimia ndani yangu,

ndipo, nilipomkumbuka Bwana,

maombo yangu yakakufikia katika Jumba lako takatifu.

9Washikao mizimu iliyo ya uwongo tu humwacha awahurumiaye,[#Sh. 31:7.]

10lakini mimi nitapaza sauti za kukushukuru,

ziwe ng'ombe zangu za tambiko, nitakazokutolea,

nayo, niliyokuapia na niyalipe! Wokovu uko kwake Bwana.

11Ndipo, Bwana alipomwagiza yule samaki, naye akaja

kumtapika Yona pwani.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania