The chat will start when you send the first message.
1Ikawa, Yabini, mfalme wa Hasori, alipoyasikia, akatuma kwa Yobabu, mfalme wa Madoni, na kwa mfalme wa Simuroni na kwa mfalme wa Akisafu,
2na kwa wafalme waliokuwako kaskazini milimani na nyikani upande wa kusini wa Kineroti (Genezareti) na katika nchi ya tambarare na vilimani kwa Dori huko baharini,
3hata kwa Wakanaani waliokaa upande wa maawioni kwa jua na upande wa baharini na kwa Waamori na kwa Wahiti na kwa Waperizi na kwa Wayebusi milimani na kwa Wahiwi waliokaa chini kwa Hermoni katika nchi ya Misipa.
4Wakatoka wao pamoja na majeshi yao, wakawa watu wengi, kama mchanga ulioko ufukoni kwenye bahari ulivyo mwingi; walikuwa hata na farasi na magari mengi sana.
5Hawa wafalme wote walipokwisha kupatana mashauri, wakaenda, wakapiga makambi pamoja kwenye ziwa la Meromu, wapate kupigana nao Waisiraeli.
6Lakini Bwana akamwambia Yosua: Usiwaogope! Kwani kesho saa zizi hizi mimi nitawatoa wao wote, kuwa wamekwisha kuuawa na Waisiraeli, nao farasi wao na uwakate mishipa, nayo magari yao na uyachome moto.
7Ndipo, Yosua na wapiga vita wote waliokuwa naye walipowaendea huko kwenye ziwa la Meromu, mara wakawashambulia,
8naye Bwana akawatia mikononi mwa Waisiraeli, wakawapiga, wakawakimbiza mpaka Sidoni ulio mkuu na mpaka Misirefoti-Maimu (Maji Kupwa) na mpaka bondeni kwa Misipe upande wa maawioni kwa jua, wakawapiga, wasisaze hata mmoja aliyekimbia.[#Yos. 13:6.]
9Yosua akawafanyizia, kama Bwana alivyomwagiza, farasi wao akawakata mishipa, nayo magari yao akayachoma moto.
10Wakati huo Yosua akarudi, akauteka Hasori, naye mfalme wake akamwua kwa upanga, kwani kale Hasori ulikuwa mji mkuu wa hizi nchi za kifalme zote.
11Wakawapiga wote pia waliokuwamo kwa ukali wa panga wakiwatia wote waliovuta pumzi mwiko wa kuwapo, hakusalia hata mmoja; nao mji wa Hasori akauteketeza kwa moto.[#4 Mose 21:2.]
12Nayo miji yote ya hao wafalme Yosua akaiteka pamoja na wafalme wao, akawapiga kwa ukali wa panga akiwatia mwiko wa kuwapo, wasiachwe kabisa, kama Mose, mtumishi wa Bwana, alivyowaagiza.
13Lakini miji yote iliyokuwa juu ya vilima vyao Waisiraeli hawakuiteketeza, Hasori peke yake tu Yosua aliuteketeza.
14Nazo nyara zote za humo mijini pamoja na nyama wa kufuga wana wa Isiraeli wakawachukua, lakini watu waliwaua wote kwa ukali wa panga, mpaka wawaangamize kabisa, hawakusaza ye yote aliyevuta pumzi.
15Kama Bwana alivyomwagiza mtumishi wake Mose, ndivyo, Mose naye alivyomwagiza Yosua, navyo ndivyo, Yosua alivyovifaanya: yale maneno yote, Bwana aliyomwagiza Mose, hakutengua hata moja, asilifanye.
16Ndivyo, Yosua alivyoiteka hiyo nchi nzima, ile ya milimani nayo ya upande wa kusini nayo nchi yote ya Goseni nayo nchi ya tambarare nayo ya nyika nayo milima ya Isiraeli pamoja na nchi yao ya tambarare,[#Yos. 10:41.]
17toka ile milima mitupu inayoendelea hata Seiri, mpaka Baali-Gadi katika bonde la Libanoni chini ya mlima wa Hermoni; nao wafalme wao wote Yosua akawateka, akawapiga na kuwaua.
18Siku nyingi Yosua alipiga vita nao hao wafalme wote.
19Haukuwako mji uliofanya mapatano na wana wa Isiraeli, wasipokuwa wale Wahiwi waliokaa Gibeoni; yote mingine waliichukua kwa kupiga vita.[#Yos. 9:15.]
20Kwani hili nalo lilitoka kwa Bwana, akiishupaza mioyo yao, waende kupiga vita na Waisiraeli, ule mwiko wa kuwapo waliotiwa umalizike, wasijipatie upendeleo, ila mwangamizo wao tu, kama Bwana alivyomwagiza Mose.[#5 Mose 7:2.]
21Wakati huo Yosua akaenda kuwang'oa Waanaki milimani kwa Heburoni na kwa Debiri na kwa Anabu na milimani ko ote kwa Wayuda na milimani ko kote kwa Waisiraeli, Yosua akawatia mwiko wa kuwapo wao wenyewe na miji yao, wasiachwe kabisa.[#4 Mose 13:22; 5 Mose 1:28.]
22Hawakusalia Waanaki katika nchi ya wana wa Isiraeli, ni kule Gaza tu na Gadi na Asdodi; ndiko, walikosalia.[#1 Sam. 17:4.]
23Yosua akaichukua hiyo nchi yote nzima, kama Bwana alivyomwambia Mose, kisha Yosua akaigawia Waisiraeli, iwe fungu lao, kama walivyogawanyika kwa mashina yao. Kisha nchi ikapata kutulia, kwani vita vilikuwa vimekoma[#Yos. 14:15.]