Yosua 17

Yosua 17

Fungu la nusu ya Manase.

1Kisha shina la Manase likapigiwa kura, kwani yeye alikuwa mwana wa kwanza wa Yosefu. Naye Manase mwanawe wa kwanza alikuwa Makiri, babake Gileadi; kwa kuwa huyu alikuwa mtu wa kupiga vita, alipewa Gileadi na Basani.[#4 Mose 26:29; Yos. 13:31.]

2Kisha wana wa Manase waliosalia wakapata mafungu yao ukoo kwa ukoo, wana wa Abiezeri na wana wa Heleki na wana wa Asirieli na wana wa Sekemu na wana wa Heferi na wana wa Semida; hawa ndio wana wa kiume wa Manase, mwana wa Yosefu, kwa koo zao.

3Lakini Selofuhadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi mwana wa Makiri, mwana wa Manase, hakuwa na wana wa kiume, ila wa kike tu, nayo haya ndiyo majina ya wanawe wa kike: Mala na Noa, Hogla, Milka na Tirsa.[#4 Mose 26:33; 27:1.]

4Hawa wakamtokea mtambikaji Elazari na Yosua, mwana wa Nuni, na wakuu kwamba: Bwana alimwagiza Mose kutupa sisi fungu katikati ya waumbu zetu, liwe letu! Kwa agizo hilo la Bwana akawapa fungu katikati ya ndugu za baba yao, liwe lao.

5Kwa hiyo Manase akagawiwa na kura mafungu kumi pasipo kuzihesabu nchi za Gileadi na za Basani zilizoko ng'ambo ya huko ya Yordani,

6kwani wana wa kike wa Manase waligawiwa mafungu, yawe yao katikati ya wanawe wa kiume, nayo nchi ya Gileadi ikawa yao wana wa Manase waliosalia.

7Nao mpaka wa Manase ulitoka kwa Aseri, ukaja Mikimetati unaoelekea Sikemu; huko uligeukia kuumeni kufika kwa wenyeji wa Eni-Tapua.

8Nchi ya Tapua ilikuwa yake Manase, lakini mji wa Tapua uliokuwa mpakani ulikuwa wao wana wa Efuraimu.

9Kisha mpaka ulitelemka kwenye kijito cha Kana upande wa kusini wa hicho kijito; huko iko miji ya Waefuraimu katikati ya miji ya Manase. Kisha mpaka wa Manase uliendelea upande wa kaskazini wa hicho kijito, hata utokee baharini.[#Yos. 16:9.]

10Upande wa kusini ulikuwa wa Efuraimu, nao upande wa kaskazini ulikuwa wa Manase; nayo bahari ilikuwa mpaka: upande wake wa kaskazini walipakana na Aseri, nao upande wa maawioni kwa jua walipakana na Isakari.

11Tena Manase alipata kwa Isakari na kwa Aseri miji hii: Beti-Seani pamoja na vijiji vyake na Ibilamu pamoja na vijiji vyake na wenyeji wa Dori pamoja na vijiji vyake na wenyeji wa Endori pamoja na vijiji vyake na wenyeji wa Taanaki pamoja na vijiji vyake na wenyeji wa Megido pamoja na vijiji vyake, ni ile nchi yenye vilima vitatu.[#Amu. 1:27; 1 Sam. 28:7.]

12Lakini wana wa Manase hawakuweza kuwafukuza wenyeji wa hiyo miji; ndivyo, Wakanaani walivyopata kukaa kwanza katika nchi hii.[#Yos. 15:63.]

13Lakini Waisiraeli walipopata nguvu wakawashurutisha Wakanaani kuwafanyia kazi za kitumwa, lakini kufukuza hawakuwafukuza.[#Yos. 16:10.]

14Kisha wana wa Yosefu wakamwambia Yosua kwamba: Mbona umetupigia kura mara moja tu na kutupatia fungu moja tu, liwe letu, nasi tu watu wengi, kwa kuwa Bwana ametubariki mpaka sasa!

15Yosua akawaambia: Kama ninyi m watu wengi, haya pandeni kwenye misitu kuikata, mjipatie pa kukaa huko katika nchi ya Waperizi na katika nchi ya Majitu, ikiwa milima ya Efuraimu inawasonga, isiwatoshe.

16Ndipo, wana wa Yosefu waliposema: Milima hii haitutoshi kweli; lakini Wakanaani wote wanaokaa bondeni kwa Beti-Seani na katika vijiji vyake nao wanaokaa bondeni kwa Izireeli wako na magari ya chuma ya kupigia vita.

17Ndipo, Yosua alipowaambia wao wa mlango wa Yosefu, wao Wamanase na Waefuraimu, kwamba: Ninyi mkiwa watu wengi wenye nguvu kubwa, hamtapata kwa kura nchi moja tu, iwe yenu.

18Kwani nchi yote ya milima nayo ni yako; kweli ni yenye misitu, lakini huko ndiko, utakakoweza kujipatia pa kukaa wa kuikata, kwani mwisho, itakapotokea kuwa wazi, itakuwa yenu. Kwani Wakanaani mtawafukuza, ijapo wawe wenye magari ya chuma ya kupigia vita, tena ijapo nguvu zao zaidi.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania